Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
Dkt. Sospeter B, MD
10 Desemba 2020 19:33:57
Fangasi kwenye ulimi na kinywa
Maambukizi ya fangasi kwenye ulimi hufahamika kitiba kwa jina la oral thrush au oral candidiasis, maambukizi haya husababishwa na fangasi wanaoitwa candida albicans. Fangasi huyu makazi yake ni ndani ya uke na mdomo ya binadamu, hata hivyo kuna baadhi ya sababu zinaweza kusababisha fangasi kuongezeka maradufu kisha kusababisha mwonekano wa dalili za maambukizi kwenye midomo na ulimi
Fangasi wanapoongezeka kwenye mdomo husababisha mwonekano wa weupe kama maziwa kwenye kuta za midomo na ulimi pamoja na fizi, wakati mwingine sakafu na paa la mdomo pia hupata weupe unaofanana na maziwa.
Visababishi
Kisababishi kikuu cha kupata fangasi wa kinywa ni kushuka kwa kinga mwilini, kinga zinaweza kushuka kutokana na maambukizi ya bakteria au virusi kwenye kinywa au kwenye damu. Kiwango kidogo cha kinga mwilini kinaweza kusababishwa pia na matatizo ya kuzaliwa. (soma kuhusu upungufu wa kingwa mwilini kwenye makala za ULY CLINIC kuelewa zaidi)
Watoto wanapozaliwa pia huweza kupata maambukizi ya fangasi kwenye kinywa wakati wanapita katika tundu la uzazi tundu la uzazi
Kina nani hupata tatizo hili?
Fangasi wa kinywa na ulimi hutokea sana kwa watoto wadogo na watu wazima ambao kinga za mwili zimepungua sana kutokana na sababu mbalimbali. Licha ya kutokea kwa watu wenye kinga za mwili zilizo chini, tafiti zinaonyesha kuwa watu wenye kinga za mwili katika kiwango cha kawaida pia kwa nadra wanaweza kupata tatizo hili.
Vihatarishi
Vihatarishi vya kupata tatizo hili ni;
Kuvaa vidani kwenye meno
Kuugua kisukari
Kuugua saratani
Kuugua UKIMWI
Kutumia dawa jamii ya antibiotics na corticosteroids ambazo hushusha kinga mwilini au kuua bakteria walinzi wa kinywa.
Kutumia dawa zinazokausha mate kinywani
Kuvuta sigara
Dalili
Awali fangasi wanapokuwa wanaendelea kukua, unaweza usipate dalili yoyote ile, jinsi fangasi wanavyoongezeka unaweza kupata dalili kati ya zifuatazo;
Kuwa na mabaka au utando wenye rangi nyeupe kwenye kuta za ndani ya mdomo wako, kwenye paa la mdomo na sakafu au kwenye fizi na maeneo mengine yam domo.
Mwonekano wa mabaka yaliyoinuka yanayofanana na maziwa mgando
Kuwashwa na kubadilika rangi kwa kinywa
Kushindwa kula kwa sababu unapokuwa unakula au kumeza unapata maumivu ya kinywa
Kutokwa damu kiasi kutoka kwenye mdomo endapo unajikwangua kutoa fangasi
Kuonekana kwa mipasuko na wekundu kwenye kona za midomo
Kupoteza ladha ya chakula
Maumivu ya fizi
Kutokwa na mate yanayofanana na maziwa(mate meupe)
Kusambaa kwa fangasi kwenye kinywa na sehemu za ndani zaidi ya kinywa kwa wagonjwa wene UKIMWI, saratani au wenye kinga za mwili zilizo chini.
Kulialia kwa watoto na kushindwa kunyonya vema
Vipimo
Mara nyingi tatizo hutambuliwa kwa kuangaliwa tu na daktari wako hivyo hakuna uhaja wa kufanya kipimo. Endapo kuna uhaja wa vipimo, vipimo vifuatavyo vinaweza kufanyika;
Kipimo cha culture
Kipimo cha damu
Matibabu
Matibabu ya fangasi wa mdomoni na kwenye ulimi huhusisha matumizi ya dawa za kuua fangasi zinazoitwa antifangus kwa muda wa siku 7 hadi 14. Dawa zinazoweza kutumika mifano yake huwa ni luconazole, itraconazole, clotrimazole, miconazole, anidulafungin, caspofungin, micafungin , amphotericin B au nystatin. Maambukizi sugu au makali huhitaji matumizi ya dawa kwa njia ya sindano. Endapo huponi fangasi baada ya kutumia dawa, unaweza kuhitaji kubadilishiwa dawa. Soma zaidi kuhusu matumizi ya dawa hizi kwenye sehemu ya matibabu ya fangasi wa ulimi au kinywani kwenye makala za ULY CLINIC.
Madhara ya fangasi mdomoni
Kusambaa kwa maambukizi kwenye damu na maeneo mengine ya mwili. Kusambaa huku huweza kuleta dalili za hatari, hutokea sana kwa watu wenye kinga za mwili zilizo chini mfano wagonjwa wenye maambukizi ya VVU na kisukari.
Kinga
Ili kujikinga au kupunguza hatari ya kupata maambukizi ya fangasi kwenye kinywa fanya mambo yafuatayo;
Safisha kinywa chako kwa kupiga mswaki na dawa ya meno kila unapotaka kulala na mara baada ya kula angalau mara mbili kwa siku
Endapo unatumia dawa jamii ya corticosteroid iwe ya kunywa au kuvuta, hakikisha pia unapiga mswaki kwa dawa na maji mengi ili kusafisha kinywa chako
Kagua vidani unavyovaa kinywani, visafishe kila siku
Hudhuria kliniki ya kinywa kwa jinsi ulivyopangiwa na daktari wako kwa uchunguzi
Usile vyakula vyenye sukari kwa wingi, hivi hufanya fangasi wakue zaidi. Endapo umetumia vyakula vyenye sukari, hakikisha unapiga mswaki mara moja.
Kwa mgonjwa wa kisukari. dhibiti kiwango cha sukari, hakikisha kinakuwa kwenye kiwango cha kawaida kinachoshauriwa na daktari wako.
Pata matibabu ya fangasi wa maeneo ya uke
Endapo una tatizo la kukaukiwa mate, hakikisha unapata matibabu, kunywa maji ya kutosha na mara kwa mara.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeboreshwa,
19 Julai 2023 19:54:12
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
​
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada
1. Candida infections of the mouth, throat, and esophagus. https://www.cdc.gov/fungal/diseases/candidiasis/thrush/index.html. Imechukuliwa 10.12.2020
2. Candidiasis (mucocutaneous). Merck Manual Professional Version. http://www.merckmanuals.com/en-pr/professional/dermatologic-disorders/fungal-skin-infections/candidiasis-mucocutaneous. Imechukuliwa 10.12.2020
3. Kauffman CA. Clinical manifestations of oropharyngeal and esophageal candidiasis. https://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 10.12.2020
4. Kauffman CA. Overview of candida infections. https://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 10.12.2020
5. Kauffman CA. Treatment of oropharyngeal and esophageal candidiasis. https://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 10.12.2020
6. Onishi A, et al. Interventions for the management of esophageal candidiasis in immunocompromised patients. Cochrane Database of Systematic Reviews. http://onlinelibrary.wiley.com/wol1/doi/10.1002/14651858.CD011938/abstract. Imechukuliwa 10.12.2020
7. Oral candidiasis (yeast infection). American Academy of Oral and Maxillofacial Pathology. http://www.aaomp.bizland.com/public/oral-candidiasis.php. Imechukuliwa 10.12.2020
8. Oropharyngeal/esophageal candidiasis ("thrush"). Centers for Disease Control and Prevention. https://www.cdc.gov/fungal/diseases/candidiasis/thrush/. Imechukuliwa 10.12.2020
9. Buchacz K, Lau B, Jing Y, Bosch R, Abraham AG, Gil MJ, et al. Incidence of AIDS-defining opportunistic infections in a multicohort analysis of HIV-infected persons in the United States and Canada, 2000-2010 external icon. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/pmid/27559122/. Imechukuliwa 10.12.2020
10. Lynch DP. Oral candidiasis. History, classification, and clinical presentation. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pubmed/9522103. Imechukuliwa 10.12.2020
11. Candidiasis. https://www.msdmanuals.com/home/infections/fungal-infections/candidiasis. Imechukuliwa 10.12.2020