Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
Dkt. Sospeter B, MD
5 Aprili 2021, 19:55:31
Kushuka kiwango cha sukari kwenye damu
Kushuka kwa sukari mwilini (au kuishiwa na sukari) hufahamika kwa neno la kitatibu kama “hypoglycemia” lenye maana ya kushuka kwa kiwango cha sukari kwenye damu kwa kiwango ambacho si cha kawaida.
Kutokana na sababu mbali mbali, ni kawaida kwa kiwango cha sukari katika damu hupanda na hushuka kwa siku nzima, ingawa si rahisi kugundua kwa kuwa mabadiliko hayo hayana mashiko. Hata hivyo, kiwango cha sukari kinaposhuka chini ya miligramu 70 kwa kila desilita (70mg/dl) au uniti ya millimoles 3.9 kwa kwa lita (3.9mmol/L) kwa mujibu wa kipimo cha sukari, dalili huonekana na tatizo hili lisipochukuliwa hatua huleta madhara makubwa hata kupelekea kifo.
Kushuka kwa sukari si ugonjwa bali ni ishara ya tatizo fulani la kiafya ndani ya mwili, na dalili hii hutokea mara chache kwa watu wazima na watoto walio na umri wa zaidi ya miaka 10, na mara nyingi huwapata watu wenye kisukari aina ya kwanza.
Dalili
Dalili za kushuka kwa sukari hazitofautiani kati ya watu wenye kisukari na wasio na kisukari ambazo huwa ni;
Dalili za awali
Dalili za hatari
Dalili za kushuka kwa sukari baada ya kutoka usingizini
Dalili za awali
Kuhisi njaa
Kichefuchefu
Kutetemeka mwili
Kutokwa na jasho
Kupauka kwa rangi ya ngozi ya uso na kuwa kama mtu aliyepungukiwa na damu
Mapigo ya moyo kwenda mbio
Kutokuona vema (kuona ukungu)
Kuhisi kizunguzungu
Mwili kuishiwa nguvu
Kuchanganyikiwa
Kuhisi vitu vinatembea au kupata ganzi kwenye midomo, ulimi au mashavu
Dalili za hatari
Kuhisi uoga na kuwa mkali
Kuoteza umakini
Kushindwa kuongea
Kupata degedege
Matatizo ya mgongeo wa misuli
Kuzimia n.k
Dalili za kushuka kwa sukari baada ya kutoka usingizini
Kushuka kwa sukari huweza kutokea pia mtu akiwa usingizini, dalili zake ni;
Kupiga kelele au kupata jinamizi
Kulowana kwa shuka au nguo kwa sababu ya jasho
Kuhisi uchovu baada ya kuamka
Kuwa mkali baada ya kuamka
Kuchanganyikiwa baada ya kuamka
Visababishi
Sababu za kushuka kwa sukari hutofautianana kati ya mtu mwenye kisukari na asiye na kisukari, hii inatengeneza makundi mawili ambayo ni;
Visababishi kwa mtu asiye na kisukari
Visababishi kwa mtu mwenye kisukari
Visababishi kwa mtu mwenye kisukari
Matumizi ya dawa za kisukari
Kushuka kwa sukari huweza tokea kama madhara ya matumizi ya dawa za kisukari, haswa matumizi ya dawa aina ya insulin. Kuchoma dozi kubwa au kuchoma kwenye misuli badala ya chini ya ngozi, husababisha dawa kufanya kazi kwa haraka zaidi hivyo kushusha sukari katika damu
Dawa za kunywa pia kama glimepiride, chlorpropamide n.k husababisha kongosho kuongeza uzalishwaji wa insulin na inaopelekea kushuka kwa sukari mara dufu zaidi.
Kutokula kwa wakati, kula kidogo au kutokula kabisa
Kula vyakula vyenye kiwango kidogo cha wanga bila kupunguza dozi ya insulin
Mazoezi; aina, muda na wakati gani mazoezi hufanyika huathiri kiwango cha sukari.
Matumizi ya pombe
Visababishi kwa watu wasio na kisukari
Aina mbili za kushuka kwa sukri hutokea kwa watu wazima wasio na kisukari ni;
Kushuka kwa sukari baada ya kula
Kushuka kwa sukari wakati wa mfungo
a. Kushuka kwa sukari baada ya kula
Hutokea ndani ya masaa manne baada ya kula.Aina hii huthibitika kitaalamu endapo dalili za kushuka kwa sukari zimetokea wakati kiwango cha sukari katika damu ni chini ya 70 mg/dl (3.9mmol/L), baada ya kula.
Kisababishi cha aina hii bado haifahamiki vizuri japo watafiti wengi wanasema kwamba huhusiana na kuongezeka kwa baadhi ya watu kiwango cha homoni aina ya epinephrine ambayo husababisha dalili za kushuka kwa sukari.
Wanasayansi wengine wanahusianisha na upungufu wa uzalishwajiwa homoni aina ya glucagon kufuatia kula chakula.
b. Kushuka kwa sukari wakati wa mfungo
Huambatana na matatizo ya kiafya. Huthibitishwa kitaalamu pale endapo kiwango cha sukari katika damu kipo chini ya 50 mg/dl (2.8mmol/L) kufuatia mfungo wa usiku mzima, katikati ya milo mikuu au baada ya kufanya mazoezi.
Visababishi
Matumizi ya baadhi ya dawa mfano dawa za kisukari, dozi kubwa ya aspirin, dawa zenye sulfa, pentamide na quinine
Matumizi yaliyokithiri ya pombe
Magonjwa ya ini
Magonjwa ya figo
Uvimbe kwenye kongosho (insulinoma)
Magonjwa sugu kama saratani
Upungufu wa homoni aina ya cortisol, growth hormone, glucagon au epinephrine
Mazoezi makali au ya muda mrefu
Kinga
Kwa mtu ambaye yuko katika hatari ya kupata tatizo la kushuka kwa sukari, na hasa mgonjwa wa kisukari unashauriwa kufanya mambo yafuatayo,
Kula kidogo kidogo na mara nyingi , walau mara tatu kwa siku
Kula vyakula vyenye wanga usiokobolewa
Wasiliana na daktari wake kuhusu dawa za kisukari unazotumia
Kupima kiwango cha sukari mara kwa mara
Kuepuka kunywa pombe bila kula
Kutembea na chakula cha tahadhari
Pima kiwango chako cha sukari na kula pale ambapo kiwango cha sukari kipo chini
Kula chakula cha wanga kabla ya kufanya mazoezi
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeboreshwa,
19 Julai 2023, 19:53:55
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada
1. Hypoglycemia in Adults. https://www.reliasmedia.com/articles/78107-hypoglycemia-in-adults. Imechukuliwa 05.04.2021
2. Low Blood Sugar (Hypoglycemia). https://www.healthline.com/health/hypoglycemia#symptoms. Imechukuliwa 05.04.2021
3. American diabetes association. Hypoglycemia (Low Blood sugar). https://www.diabetes.org/healthy-living/medication-treatments/blood-glucose-testing-and-control/hypoglycemia. Imechukuliwa 05.04.2021
4. All about hypoglycemia (low blood sugar). https://www.medicalnewstoday.com/articles/166815#takeaway. Imechukuliwa 05.04.2021
5. Blood Sugar Level Ranges. https://www.diabetes.co.uk/diabetes_care/blood-sugar-level-ranges.html. Imechukuliwa 05.04.2021
6. Learn first aid for someone who is having a diabetic emergency . https://www.redcross.org.uk/first-aid/learn-first-aid/diabetic-emergency. Imechukuliwa 05.04.2021
7. Hypoglycemia in adults without diabetes mellitus: Clinical manifestations, diagnosis, and causes. https://www.uptodate.com/contents/hypoglycemia-in-adults-without-diabetes-mellitus-clinical-manifestations-diagnosis-and-causes#H22. Imechukuliwa 05.04.2021
8. Centre for disease control and prevention. Manage Blood Sugar. https://www.cdc.gov/diabetes/managing/manage-blood-sugar.html. Imechukuliwa 05.04.2021
9. M L Virally, et al. Hypoglycemia in adults. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/10633872/. Imechukuliwa 05.04.2021