Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
Dkt. Sospeter B, MD
4 Juni 2021 11:49:55
Msongo
Ili mwili upate msongo, lazima kuwe na kiamshi, ambacho huitwa kichocheo. Kuna aina nyingi za vichocheo vinavyoweza kusababisha msongo kama vile mahangaiko/mapambano ya kufanikiwa, kulemewa na kazi, kipato duni, malumbano ndani ya mahusiano au familia na mambo mengine yasiyoorodheshwa hapa.
Msongo huwa na faida pamoja na hasara, msongo mfupi humsaidia binadamu kukabiliana na vichocheo mbalimbali, mfano endapo umepatwa na jambo la kushitusha ghafla, msongo huamsha homoni za msongo(adrenaline n.k) zinazokusaidia upate nguvu na kuweza kukimbia au kupigana(kukabiliana na tatizo uso kwa uso). Msongo sugu huambatana na magonjwa mbalimbali mwilini ambayo yameorodheshwa kwenye Makala hii.
Tafiti zinaonyesha zaidi ya asilimia 80 ya magonjwa yanayowapata binadamu hutokana na msongo. Baadhi ya magonjwa yanayoweza kutokea kutokana na msongo ni magonjwa ya mishipa ya damu, kisukari, shinikizo la juu la damu, saratani, vidonda vya tumbo n.k.
Kwa sababu binadamu wa uri, rangi na jinsia yoyote hupata msongo na kuna hatari ya kupata msongo sugu, inapaswa kila mtu kutambua mbinu mbalimbali za kufanya ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Mahusiano ya msongo na magonjwa
Uhusiano wa msongo na kutokea kwa magonjwa ni tata, ikimaanisha hutegemea mtu na mtu na sababu mbalimbali kama sababu za kijeni, njia ya kukabiliana na msongo, aina ya utu na msaadamtu anapata kwenye jamii yake. Mtu anapopata kichocheo kwa kawaida, hujipima endapo kipo ndani ya uwezo wake au la. Endapo kichocheo kipo ndani ya uwezo wa mtu kikabiliana nacho, hukifanyia kazi na kikaisha, isipokuwa endapo kipo nje ya uwezo basi hupelekea mtu huyu kupata msongo wa muda mrefu na madhara kuonekana.
Kutokana na maelezo haya, inamaanisha kuwa kichocheo kinachopelekea msongo wenye madhara kwa mtu mmoja kinaweza kisisababishe madhara kwa mtu mwingine na pia namna mtu anavyoitikia kukabiliana na kichocheo huchangia kutokea au kutotokea kwa madhara ya msongo.
Mabadiliko mwilini dhidi ya kichocheo cha msongo
Mwiitikio wa mwili kwenye kichocheo cha msongo hupelekea kutokea kwa mabadiliko ya kifiziolojia, na kitabia. Mwitikio wa kifiziolojia hutokea kupitia njia mbalimbali ikiwa ni kuamshwa kwa mfumo wa neva wa simpathetiki, kuamka kwa muhimili wa hypothalamus-pituitari- adreno(HPA) na ujasiri wa kupigana au kukimbia.
Kuamka kwa HPA na mfumo wa neva wa simpathetiki hupelekea tezi za adreno zinazopatikaka juu ya figo kuzalisha kwa wingi homoni cortisol. Homoni cortisol huwa na madhara mengi ya kifiziolojia kama vile kuchochea uzalishaji wa homoni ya adrenaline na noradrenaline, kupunguza uzalishaji wa homoni insulin, kuongeza uzalishaji wa sukari, kupunguza mwitikio wa kinga dhidi ya michomo na kupunguza kasi ya kupona kwa majeraha.
Mwitikio huu awali huwa na malengo mazuri tu ya kupunguza majeraha, hata hivyo endapo utakuwa sugu( wa muda mrefu) mwili huanza kupata magonjwa kama sonona, kupungua kwa ufahamu, kinga za mwili na magonjwa ya moyo n.k
Dalili
Dalili za msongo hutegemea sehemu ya mwili iliyoathiriwa, kuna dalili za awali na dalili sugu ambazo hutokea kwenye msongo wa muda mrefu. Kila dalili inayotokea huashiria madhara ya mabadiliko ndani ya mifumo mbalimbali ya mwili yanayotokana na uzaliswhaji wa muda mrefu wa homoni za msongo.
Dalili za kihisia
Kukasirika haraka, kuchanganyikiwa na kuwa na hisia za kubadilika
Hisia za kutindikiwa kama vile kuona huna uwezo tena wa kudhibiti kitu Fulani, au kutaka kudhibiti kitu Fulani lakini
Kutokuwa na utulivu au kushindwa kutuliza akili
Kujihisi hufai, mpweke, usiye na thamani na mwenye mawazo mengi
Kujitenga na watu
Dalili za mabadiliko ya mwili
Kuishiwa nguvu
Maumivu ya kichwa
Mvurugiko wat umbo mfano choo kigumu, kuharisha na kichefuchefu
Maumivu , kubana na kuchomachoma kwa misuli
Maumivu ya kifua na mapigo ya moyo kwenda haraka
Kukosa usingizi
Kuugua mafua mara kwa mara na kupata maambukizi
Kukosa hamu au uwezo wa kufanya tendo la ndoa
Kukauka midomo na kushidnwa kumeza chakula
Kukaza kwa taya na kusagana kwa meno
Dalili kwenye mfumo wa fahamu
Kuwa na hofu endelevu
Mawazo yasiyotulivu
Kusahau
Kutokuwa na mpangilio wa mawazo
Kushindwa kutulia kwenye wazo kichwani
Kushindwa kuhukumu mawazo
Kuwa na mawazo hasi au kuona upande hasi tu
Dalili za kitabia
Mabadiliko ya hamu ya kula( kutokula au kula sana)
Kuahilisha mambo au kuepuka majukumu
Ongezeko la utumiaji wa pombe, dawa za kulevya au sigara
Ongezeko zaidi la tabia za kineva kama vile kula kucha, kutetemeka na kutembea tembea bila sababu
Madhara ya muda mrefu wa msongo
Msongo wa muda mfupi si hali ya kutia hofu, endapo msongo unadumu zaidi ya muda wa miezi mitatu inatakiwa jamii itambue na kumsaidia mtu huyu kumuepusha na madhara makubwa yanayoweza kujitokeza. Madhara hayo baadhi yake ni,
Magonjwa ya akili
Sonona,
Hofu iliyopitiliza
Madhaifu ya ki utu
Magonjwa ya mfumo wa mishipa ya damu na moyo
Magonjwa wa moyo
Shinikizo la juu la damu(presha ya kupanda)
Mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida
Mshituko wa moyo
Kuharusi
Mabadiliko ya mwili
Kuongezeka uzito na matatizo mengine ya unene
Matatizo ya hedhi
Kuona hedhi kidogo
Kutoona hedhi kabisa
Hedhi kuwa yenye damu nyingi
Hedhi yenye maumivu makalai
Matatizo uzazi
Ugumba kwa wanaume
Kuwahi mwaga shahawa wakati wa tendo
Kukosa hamu ya kujamiana kwa wanaume na wanawake
Madhaifu ya ngozi
Kuota kwa chunusi
Ugonjwa wa soriasis
Ezima
Kupoteza nywele
Magonjwa ya mfumo wa chakula
Kucheua tindikali
Michomo tumboni
Vidonda vya michomo kwenye utumbo mpana
Ghasia kwenye utumbo mpana
Namna ya kujikinga na msongo
Kula na kunywa maji ya kutosha.
Watu wengi hujaribu kupunguza msongo kwa kutumia dawa za kulevya au kunywa pombe zaidi ya kawaida, kitendo hiki huharibu afya ya mtu zaidi na pia huwa hakisababishi kukabiliana na msongo. Ni vema ukiwa na msongo, unywe maji ya kutosha na mlo kamili ambao utakusaidia kukabiliana na msongo. Usitumie kahawa kwani inahusika kukuletea msongo mkubwa zaidi.
Fanya mazoezi yenye utaratibu
Mazoezi huwa na umuhimu kwenye afya ya mwili wako amoja na nguvu ya kupunguza msongo. Mazoezi mazuri si yale ya mashindano bali ni kama mazoezi ya viungo vya mwili, kunyanyua uzito, kujinyoosha pamoja na yoga. Mazoezi ya aerobic pia yanayohusisha kukimbia, kuogelea, kulima n.k husaidia mwili kujitengenezea homoni ya endorphin kwa wingi, homon inayosaidia kupunguza msongo, kukufanya uwe na mawazo chanya na kukupa usingizi mzuri.
Usitumie tumbaku na mazao yake
Watu watumiao 9tumbaku) sigara hupata pumziko la msongo wa muda mfupi, hata hivyo nicotine iliyo kwenye sigara huamsha na kufanya tatizo liwe kubwa zaidi mara baada ya kuacha. Dawa hizi pia hufanya mwili uwe mtumwa wa dawa hizo na ni ngumu kuziacha.
Soma na fanya matendo ya kupumzisha mwili na akili yako
Kupata muda wa kupumzika kila siku hulinda mwili wako dhidi ya madhara ya msongo. Unaweza kutumia njia mbalimbali za kupumzisha mwili wako kama vile kupumua kwa kina, kupumzisha misuli kwa muda mrefu, kutengeneza picha ya vitu kwenye akili na kutafakari kwa kina.
Punguza vichocheo vya msongo
Maisha yako yanaweza kujawa na mahitaji mengi na matamanio mengi na ukawa na muda kidogo sana wa kupumzika, hata hivyo mara nyingi mahitaji haya ni yale ambayo sisi wenyewe tumeyachagua na hutuangaisha. Unaweza kujipa muda mwingi binafsi kwa kupunguza au kupanga muda wako vema na kupata muda wa kufanya kazi na muda wa kuwa na muda mwenyewe. Weka malengo yako na weka mipango ya kufikia malengo kisha fuata mpango mmoja baada ya mwingine kufikia malengo. Usitumie nguvu nyingi kupata mafanikio kwani mafanikio huja taratibu hatua kwa hatua.
Tambua kwanini upo duniani
Kutambua kwanini unaishi, na nini unataka katika maisha yako kutafanya uishi maisha yako ya kipekee na yasiyotegemea mvuto wa watu wengine. Kuishi maisha yaliyo madhumuni ya maisha yako duniani hufungua furaha, kuridhika na kujiamini wakati wote bila kuyumbishwa na mambo yanayopita.
Weka malengo yenye uhalisia
Ni vema na ni sawa kuwa si lazima kupata asilimia 100 ya matamanio yako katika maisha mara moja, hata hivyo unapoweka malengo fuata mipango uliyoiweka kutimiza malengo yako. Kubali vitu ambavyo unaweza kuvidhibiti na ambavyo usivyoweza kuvidhibiti.
Jisifie au jipongezekwa mafanikio uliyoyafikia
Unapohisi umelemewa na mzigo wa maisha, jikumbushe kuwa kuna mambo mengi umeshafanya katika maisha na unaendelea kufanya vema. Hii itaamsha kujikubali na kuondoa msongo wa mawazo.
Ongea na daktari wa akili
Kuongea na daktari wa magonjwa ya akili endapo unaona hupati msaada kwa njia zote zilizoorodheshwa hapa kutakusaidia kukupa mwanga wa nini ufanye. Wasiliana na daktari siku zote endapo unaishi dalili zozote zile za msongo. Endapo pia kuna ndugu yako ana dalili hizi ni vema ukamsaidia kupata msaada wa daktari.
Pata msaada wa kiroho.
Onana na imamu au mchungaji wako kwa ushauri kuhusu mambo ya kiroho. Hii itasaidia kukupa Amani moyoni na kupunguza au kuondoa msongo wa mawazo. Shiriki maombi, jiamini na jiombee mwenyewe
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeboreshwa,
19 Julai 2023 19:53:55
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
​
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada
1. Physiology, Stress Reaction. Brianna Chu, et al. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK541120/. Imechukuliwa 04.06.2021
2. Life Event, Stress and Illness. Mohd. Razali Salleh. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3341916/. Imechukuliwa 03.06.2021
3. Habib Yaribeygi, et al. The impact of stress on body function: A review. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC5579396/. Imechukuliwa 02.06.2021
4. Bruce McEwen et al. stress and your health. https://academic.oup.com/jcem/article/91/2/E2/2843213. Imechukuliwa 04.06.2021
5. American Institute of Stress: "Effects of Stress.". https://www.stress.org/. Imechukuliwa 04.06.2021
6. Manage stress. https://health.gov/myhealthfinder/topics/health-conditions/heart-health/manage-stress. Imechukuliwa 04.06.2021
7. Get enough sleep. https://health.gov/myhealthfinder/topics/everyday-healthy-living/mental-health-and-relationships/get-enough-sleep. Imechukuliwa 04.06.2021