top of page
Mwandishi:
Dkt. Benjamin L, MD
Mhariri:
Dkt. Salome A, MD

Dawa za kuzuia maambukizi ya VVU baada ya hatari

10 Julai 2023 19:04:14
Image-empty-state.png

Hufahamika kwa jina la PEP, huzuia maambukizi baada ya kuwa kwenye kihatarishi.ndani ya masaa 72. Kabla ya kutumia dawa hizi utafanyiwa vipimo kuangalia kama una maambukizi ya virusi vya UKIMWI.


UKIMWI ni ugonjwa unaosababishwa na Virusi Vya UKIMWI ama VVU, neno hili ni kifupi cha Upungufu wa KInga MWIlini. Mtu anapata maambukizi ya ukimwi kwa njia mbalimbali ambazo ni,

 

  • Kujamiana na mtu aliyeathirika bila kutumia kinga- inaweza kuwa uume kwa uke, midomo, njia ya haja kubwa n.k.

  • Kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, wakati wa kujifungua

  • Kutumia sindano na mtu aliye na VVU

  • Kuongezewa damu ya mtu aliyeathirika na VVU

  • Kugusana kidonda kwa kidonda na mtu aliyeathirika na VVU

  • Busu la kubadilishana mate na mwathirika endapo kuna vidonda mdomoni kwa wawili na wao busiana

 

Mbali na maelezo ya hapo juu kwa ufupi, wafanyakazi wa Afya, watu waliobakwa au kujeruhiwa kwenye ajali kisha damu ya majeruhi mmoja kuchanganyika na kidonda cha majeruhis mwingine hupelekea kupata maambukizi ya VVU endapo mmoja ni mwathirika. Wafanyakazi wa Afya wanapokuwa wana wahudumia waathirika wa VVU wakati wa upasuaji endapo wasipokuwa makini wanaweza kujichoma na sindano hizo, kurukiwa na majimaji au damu na wale waliobakwa wanaweza kupata maambukizi ya UKIMWI

 

Endapo umejikuta upo hatarini je kuna dawa kutumia ili kuepuka kupata UKIMWI?

 

Jibu ni ndio

Zipo dawa za kutumia ili kukukinga kupata maambukizi ya VVU mara baada ya kukutana na kihatarishi, dawa hizi huitwa PEP

 

Dhumuni la makala hii ni kukueleza kuhusu dawa zitakazokuzuia kupata maambukizi ya VVU endapo umeshakutana na vihatarishi vilivyoorodheshwa hapo juu. Soma kuhusu dawa za kukukinga kupata maambukizi endapo unajua unaenda kwenye kihatarishi cha kupata maambukizi ya VVY bofya hapa

 

Kina nani wanapaswa kupata dawa hizi?

 

Si kila mtu anapaswa kutumia(kupewa) dawa hizi, dawa hutolewa ndani ya masaa 72 tu toka umekutana na kihatarishi na pia lazima usiwe na maambukizi ya VVU kabla ya kuanzishiwa dawa hizi. Watu au hali zifuatazo zitakulazimu kutumia dawa za PEP ili kujikinga na kupata UKIMWI;

 

  • Watu waliokutana na majimaji ya mwili kama mate yenye damu, maziwa ya mama, uteute wa sehemu za siri, uteute wa uti wa mgongo, ute wa chupa ya uzazi wakati wa mama kujifungua, ute wa peritoniamu, ute wa magoti, ute wa perikadio ute wa mapafu

  • Kugusana maeneo ya ngozi laini kama uke, midomo au uume kwa kufanya mapenzi, kurukiwa na maji maji kwenye macho, mdomoni au puani

  • Kuongezewa damu

 

Watu wasiostahili kupata dawa za PEP licha ya kuwa na kihaarishi ni;

 

  • Mtu ambaye tayari anajifahamu kuwa na maambukizi ya VVU

  • Endapo chanzo hakina maambukizi ya VVU

  • Endapo umekutana na majimaji ya machozi, mate yasiyo na damu, mkojo na jasho la mtu mwenye VVU

 

Dawa zinazotumika kama PEP ni muunganiko wa dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI(ARVs) tafiti zinaonyesha inatakiwa kuwa na makundi mawili ya dawa endapo tafiti zinaoyesha hakuna usugu wa kirusi kwenye dawa katika maeneo hayo au dawa aina tatu zinapaswa kutumika endapo kwenye eneo hilo kuna usugu wa kirusi cha UKIMWI dhidi ya dawa za ARVs

 

Dawa mchanganyiko

Dawa kwa vijana na watu wazima ni;

  • TDF+ 3TC (au FTC) kwa vijana na watu wazima(hutumika kama msingi wa tiba)

  • LPV/r+ ATV/r huwa dawa nyongeza kwenye dawa msingi wa tiba endapo dawa ya tatu inahitajika. Mbadala wake ni EFV, RAL au DRV/r

 

Kwa watoto chini ya umri wa miaka 10 dawa zinazotumika ni;

 

  • ZDV + 3TC- kama msingi wa dawa mbili.mbadala wake ni ABC+3TC(FTC)

  • LPV/r hushauriwa kama dawa ya tatu endapo kuna umuhimu wa kutumia dawa 3. Mbadala wake ni ATV/r, RAL, EFV na NVP

 

Dawa hutumiwa kwa muda gani?

 

Dawa hizi hutumiwa kwa muda wa siku 28 kila siku bila kukosa.kabla ya kupewa dawa hizi utapata dalasi la namna ya kuzingatia kunywa dawa hizi ili usiziache.

ONYO: Usitumie dawa yoyote bila ushauri wa daktari. Dawa zinaweza kuleta madhara mwilini na pia matumizi ya baadhi ya dawa pasipo ushauri na vipimo husababisha  vimelea kuwa sugu dhidi ya dawa hiyo.
ULY clinic inakushauri kuwasiliana na daktari wako unapotaka kuchukua maamuzi yoyote yanayohusu afya yako.
Wasiliana na daktari/Mfamasia wa ULY clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kupiga simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
10 Julai 2023 19:06:35
1. WHO.https://www.who.int/hiv/pub/prophylaxis/02.pdf. Imechukuliwa 07.07.2020
Guidelines Review Committee, World Health Organization. Antiretroviral therapy for HIV infection in adults and adolescents recommendations for a public health approach. Geneva, Switzerland: WHO, 2006.

2. World Health Organization. Guidelines on post exposure prophylaxis for HIV. Recommendations for a public health approach. Geneva, Switzerland: WHO, 2014.

3. Guyatt GH, Oxman AD, Kunz R, Vist GE, Falck-Ytter Y, Schünemann HJ; GRADE Working Group. What is “quality of evidence” and why is it important to clinicians? BMJ 2008; 336:995–8. 5. World Health Organization. Consolidated guidelines on the use of antiretroviral drugs for treating and preventing HIV infection: recommendations for a public health approach. Geneva, Switzerland: WHO, 2013
bottom of page