Mwandishi:
Dkt. Sospeter M, MD
Mhariri:
Dkt. Lugonda B, MD
24 Aprili 2020, 16:28:04
Metoprolol
Metoprolol ni dawa inayotumika kutibu shinikizo la juu la damu, angina na kupunguza hatari ya kifo inayotokana na infaksheni ya mayokadia.
Majina ya kibiashara
Metoprolol hufahamika kwa majina mengine ya kibiashara kama;
Dutoprol
Kapspargo
Lopresor
Lopressor
Lopressor Hct
Toprol
Kundi la dawa
Metoprolol ipo kwenye kundi la dawa linaloitwa beta bloka.
Ufyonzwaji wa Metoprolol
Metoprolol hufyonzwa vyema kwenye mfumo wa chakula na huingia kwenye mzunguko wa damu, kiwango cha juu kabisa kwenye damu hufikiwa ndani ya saa 1 mara baada ya kunywa dawa.
Metoprolol na chakula
Tumia dawa hii pamoja na chakula ili kuongeza ufyonzaji wak. Unaweza kutumia Metoprolol pamoja na chakula au mara baada ya kula.
Muda wa kuanza kufanya kazi na nusu maisha ya Metoprolol
Madhara ya kitiba ya Metoprolol huanza kuonekana ndani ya saa 1kwa dawa ya kunywa ikitegemea dozi ya dawa na ndani ya dakika 20 kwa dawa ya kuchoma kwenye mishipa. Metoprolol hudumu kwenye damu kwa angalau kwa masaa 3-12 baada ya kunywa tembe ya dawa.
Umetaboli wa Metoprolol
Dawa hii hufanyiwa metabolizimu kwenye ini na asilimia 50 tu ya dawa mama huweza kupita kama ilivyo kwenda kwenye mzunguko wa damu mara baada ya kupita kwenye ini.
Utoaji Metoprolol mwilini
Mwili hutoa Metoprolol kwenye mzunguko wa damu asilimia 95 kwa njia ya mkojo.
Fomu na uzito wa Metoprolol
Metoprolol hupatikana katika fomu ya maji au kidonge chenye uzito wa;
25mg
50mg
100mg na
200mg
Namna Metoprolol inavyofanya kazi yake
Dawa jamii ya beta bloka ikiwa pamoja na Metoprolol hufanya kazi zifuatvyo ili kupunguza shinikizo la damu la juu;
Hufanya kazi kwa kuzuia ufanyaji kazi wa homoni epinefrini na kusisimuliwa kwa seli za beta adrenejik zilizo kwenye mishipa ya damu.
Kwa kufanya hivi hupunguza mapigo ya moyo, shinikizo la damu na upunguza mzigo wa damu kwenye Moyo na kuruhusu mzunguko wa damu kuwa mzuri mwilini
Dawa kundi moja na Metoprolol
Dawa hii ipo katika kundi sawa na dawa zifuatazo:
Acebutolol (Sectral)
Betaxolol (Kerlone)
Bisoprolol (Zebeta, Ziac)
Carteolol (Cartrol)
Carvedilol (Coreg)
Labetalol (Normodyne, Trandate)
Nadolol (Corgard)
Nebivolol (Bystolic)
Penbutolol (Levatol)
Pindolol (Visken)
Propanolol (Inderal)
Sotalol (Betapace)
Timolol (Blocadren)
Metoprolol inatibu nini?
Metoprolol hutumika katika matibabu ya;
Shinikizo la juu la damu
Magonjwa ya mishipa ya damu ya moyo kama Angina na Infaksheni ya mayokadia
Moyo ulioferi
Hutumika kupunguza hali ya kifo kutokana na infaksheni ya mayokadia
Mwingiliano wa Metoprolol na dawa zingine
Dawa hii haipaswi kutumika pamoja na dawa zifuatazo kutokana na kuwa na mwingiliano mkali;
Acebutolol
Betaxolol
Bisoprolol
Carvedilol
Celiprolol
Clonidine
Digoxin
Diltiazem
Esmolol
Labetalol
Lofexidine
Metoprolol
Nadolol
Nebivolol
Penbutolol
Pindolol
Propranolol
Rivastigmine
Saquinavir
Sotalol
Timolol
Verapamil
Wagonjwa wasiopaswa kutumia Metoprolol
Metoprolol haipaswi kutumika kwa wagonjwa wenye mzio dawa hii au dawa zingine jamii ya Beta bloka
Angalizo la Metoprolol
Dawa hii inapaswa kutumika kwa tahadhari kwa wagonjwa wafuatao;
Wagonjwa wenye haipathairodizim
Wagonjwa wenye shida ya figo
Wagonjwa wenye shida ya Ini
Wagonjwa wenye shida ya Moyo kuferi
Wagonjwa wenye umri mkubwa
Metoprolol na ujauzito
Metroprolol inahauriwa kutumika kama hakuna dawa nyingine salama wakati wa ujauzito.
Metoprolol kipindi cha kunyonyesha
Metoprolol huingia kwenye maziwa ya mama anayenyonyesha kiasi kidogo hivyo itumike kwa uangalifu kwa mama anayenyonyesha.
Madhara ya Metoprolol
Baadhi ya maudhi madogo ya dawa hii ni pamoja na :
Kizunguzungu
Maumivi ya kichwa
Msongo wa mawazo
Kuharisha
Konstipesheni
Tumbo kujaa gesi
Kichomi
Kutapika
Kutoka jasho isivyo kawaida
Kutokwa na vipele
Miguu kuwa baridi
Kuchoka mwili
Je, kama umesahau dozi ya Metoprolol ufanyaje?
Kama umesahau kutumia dozi yako ya Metoprolol, tumia mara pale utakapokumbuka. Kama muda wa dozi inayofuata umekaribia sana, subiri muda ufike ili utumie dozi hiyo kisha kuendelea kama ulivyoshauriwa na daktari wako.
ONYO: Usitumie dawa yoyote bila ushauri wa daktari. Dawa zinaweza kuleta madhara mwilini na pia matumizi ya baadhi ya dawa pasipo ushauri na vipimo husababisha vimelea kuwa sugu dhidi ya dawa hiyo.
ULY clinic inakushauri kuwasiliana na daktari wako unapotaka kuchukua maamuzi yoyote yanayohusu afya yako.
Wasiliana na daktari/Mfamasia wa ULY clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kupiga simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
5 Novemba 2021, 20:23:56
Rejea za mada hii:-