Mwandishi:
Dkt. Sospeter M, MD
Mhariri:
Dkt. Lugonda B, MD
11 Mei 2020 18:40:18
Ranitidine
Ranitidine ni dawa inayozuia uzalishaji wa tindikali kutoka kwenye seli za ukuta wa tumbo. Dawa hii iliyopo kwenye kundi la dawa inayozuia risepta za histamine (H2), huzuia homoni ya histamine ambayo huchochea kutengenezwa kwa tindikali tumboni ili isishiriki katika kazi hiyo.
Hivyo dawa hii hutumika kutibu matatizo mbalimbali yanayotokana na tindikali ya tumboni.
Majina ya kibiashara ya Ranitidine
Majina mengine ya dawah ii;
Zantac
Raticina
Gastrosedol
Microtid
Ptinolin
Fomula ya kikemikali
Fomula ya kikemikali ya Ranitidine ni C13H22N4O3S
Jina la kisayansi (IUPAC)
Jina la kisayansi la Ranitidine ni (E)-1-N'-[2-[[5-[(dimethylamino)methyl]furan-2-yl]methylsulfanyl]ethyl]-1-N-methyl-2-nitroethene-1,1-diamine
Ranitidine hutibu nini?
Dawa hii hutumiika katika kutibu hali zifuatazo:-
Vidonda vya tumbo
Kiungulia
Kucheua tindikali
Kutibu michubuko kwenye koo la chakula vilivyo sababishwa na michubuko ya tindikali (kiungulia).
Husaidia kuzuia damu kuvuja kwenye njia ya juu ya mfumo wa chakula (upper GI bleeding).
Hutumiwa wakati mgonjwa akipewa dawa ya usingizi kwa dharura ili kuzuia mgonjwa asipaliwe na tindikali kutoka tumboni.
Kutibu sindromu ya Zollinger-Ellison
Dozi na fomu ya Ranitidine
Dozi za ranitidine hupatikana kama
Vidonge vyenye;
Miligramu 75
Miligramu 150
Miligramu 300
Tembe yenye
Miligramu 75
Miligramu 150
Miligramu 300
Dozi ya kimiminika yenye
Miligramu 15/mililita
Dozi ya sindano yenye;
Miligramu 25/mililita
Namna ya kutumia Ranitidine
Tumia kama utakavyo elekezwa na daktari.
Matumizi yanategemea ugonjwa na hali ya mgonjwa.
Dawa hii inaweza kutumiwa pamoja na au bila chakula.
Epuka matumizi ya sigara wakati wa kutumia ranitidine.
Ufanyaji kazi wa Ranitidine
Dawa hii huzuia risepta za homoni histamine(H2) kupokea homoni hii ya histamine ili ifanye kazi ya kushurutisha seli za gastrin kuzalisga tindikali. Kuzuiwa huku husababisha kupungua kwa uzalishaji wa tindikali tumboni.
Ufyonzwaji wa Ranitidine
Dawa hii hufyonzwa kwa asilimia asilimia 50 ikiwa ikimezwa, lakini kiwango hiki kinaweza kufikia asilimia 90 -100 ikiwa ikichomwa kwenye msuli.
Nusu maisha ya Ranitidine
Huanza kufanya kazi saa 1 baada ya kumezwa.
Hufanya kazi kwa saa 4-6 baada ya kufyonzwa.
Hufika kilele cha kufanya kazi saa 2-3 kama ikimezwa, na kilele hicho hufikiwa kwa dakika 15 ikiwa ikichomwa kwenye msuli.
Umetaboli wa Ranitidine
Ranitidine hufanyiwa umetaboli kwenye ini ili iweze kufanya kazi na kuondolewa sumu.
Sehemu kubwa ya mazao ya umetaboli na dawa ambayo haijabadilika hutolewa kwa njia ya mkojo.
Maudhi madogo ya ranitidine
Maumivu ya Kichwa
Kizunguzungu
Kutopata choo
Homa
Mwili kufa ganzi
Kuchoka
Kuwashwa
Mdomo kukauka
Kichefuchefu
Tumbo kuuma
Kuchanganyikiwa hususani kwa wazee.
Mara chache inaweza kupunguza uwezo wa kufanya tendo kwa wanaume.
Wagonjwa wasiopaswa kutumia Ranitidine
Marufuku kwa wagonjwa wenye mzio na dawa ya ranitidine.
Tahadhari wakati wakutumia ranitidine
Matumizi ya ranitidine kwa wazee na wenye shida ya figo dawa hii inaweza kusababisha yafuatayo:-
Kuchanganyikiwa
Kuona maruweruwe
Kupata degedge
Mwili kukosa nguvu
Angalizo kwa watumiaji wa Ranitidine
Kwa wagonjwa wenye saratani ya tumbo, kupata nafuu wakati anatumia dawa hii haimaanishi kua saratani imetibka.
Dawa hii isiposaidia kutibu kiungulia baada ya majuma 6-8 ni vyema daktari akafikiria juu ya kutumia dawa za kundi la proton pumps inhibitors kama dawa mbadala pamoja na vipimo zaidi.
Matumizi ya muda mrefu yanaweza kusababisha upungfu wa vitamini B 12.
Dawa hii itumike kwa tahadhari kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo na ini.Ufuatiliaji wa karibu unahitajika kwa wagonjwa hawa.
Muingiliano na dawa nyingine
Ranitidine hupendelewa zaidi ya cimetidine ikiwa mgonjwa anatumia warafin au theophllyne kwakua ranitidine haiathiri utendaji kazi wa dawa hizi kama ilivyo cimetidine.
Ranitidine hupunguza ufanisi wa dawa zifuatazo;
Ketoconazole
Itraconazole
Digoxin
Dawa za chumvi zenye madini ya chuma
Erlotinib
Dasatinib.
Dawa zifuatozo hupunguza ufyonzwaji wa ranitidine:-
Sodium bicarbonate
Calcium carbonate
Magnesium dihydroxide
Magnesium carbonate
Magnesium trisilicate
Aluminium hydroxide
Metoclopramide
Uvutaji wa sigara hupunguza kwa kiasi kikubwa ufyonzwaji wa ranitidine hivyo ni vyema kuepuka matumizi ya sigara.
Ranitidine huongeza kiwango cha nifedipine kwenye damu kwa asilimia 30
Ranitidine huongeza kiwango cha diazepam kwenye damu.
Ranitidine na chakula
Ufyonzwaji wa ranitidine hauathiriwi na chakula hivyo dawa hii inaweza kumezwa na chakula ama pasipo chakula.
Ranitidine kwa ujauzito
Dawa hii inaweza kutumika japo kuwa uwezekano wa kutumia dawa salama Zaidi upo.
Ranitidine kwa anayenyonyesha
Ranitidine huingia kwenye maziwa ya mama na hivyo ni vyema kuepuka kuitumia wakati wa kunyonyesha na kutumia dawa salama zaidi. Ikibidi kuitumia basi tahathari lazima zichukuliwe.
ONYO: Usitumie dawa yoyote bila ushauri wa daktari. Dawa zinaweza kuleta madhara mwilini na pia matumizi ya baadhi ya dawa pasipo ushauri na vipimo husababisha vimelea kuwa sugu dhidi ya dawa hiyo.
ULY clinic inakushauri kuwasiliana na daktari wako unapotaka kuchukua maamuzi yoyote yanayohusu afya yako.
Wasiliana na daktari/Mfamasia wa ULY clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kupiga simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
23 Julai 2023 16:55:55
Rejea za mada hii:-