top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Mangwella S, MD, Dkt. Salome A, M.D

21 Julai 2023, 15:09:32

Image-empty-state.png

Dalili za uchungu wiki ya 41

Wiki ya 41 ya ujauzito uumbaji wa mtoto unakuwa umekamilika na mtoto anaweza kuishi bila shida akizaliwa. Uzito wake inakadiliwa kuwa kati ya kilo 3.6 hadi 4 na urefu wa nchi 20.4, mzingo wa kichwa chake huwa sawa na mzingo wa tumbo. Dalili za awali za uchungu na uchungu wa kweli unaweza kuanza wakati wowote ndani ya masaa 72.


Mama huendelea kupata dalili mbalimbali za ujauzito ikiwa pamoja na kubana kwa misuli ya miguu, hofu kubwa ya kupitiliza tarehe ya kujifungua, kuvimba maeneo mbalimbali ya mwili, ongezeko la hisia ya mgandamizo kwenye nyonga n.k. Dalili ya kupumua kwa shida hupungua kwa sababu mtoto anaaza kushuka. Kimo cha mimba wakati huu huweza kuwa kidogo kuliko umri wa mimba katika wiki kwa sababu ya mtoto kushuka.


Dalili za uchungu wiki ya 41

Miongoni mwa dalili za uchungu katika wiki ya 41 ni kama zifuatazo;


Kujongea kwa misuli ya tumbo la chini

Kwenye wiki hii ya 41 mjamzito anaweza kupata dalili ya kubana kwa tumbo la uzazi kwa kiasi inayopotea na isiyo na maumivu makali na kutokea bila mpangilio wa kueleweka. Kubana huku huwa ishara ya majaribio ya tumbo la uzazi kujiandaa na uchungu wa kweli.


Kukosa usingizi

Mama anaweza kukosa usingizi pia na kuwa na shauku kubwa, maumivu au uchovu.


Kuwashwa tumbo

Kuwashwa tumbo la chini kutokana na kutanuka kwa misuli na ngozi mtoto anapokuwa ansendelea kushuka kwenye nyonga.


Kuharisha

Kwenye wiki hii, kuharisha kunaweza kuwa dalili mojawapo ya kuashiria ishara ya homoni za uchungu kuwepo nyingi katika mwili wako na pia mgandamuzo wa mtoto kwenye kuta za matumbo.


Kuzibuka kwa kifuniko cha shingo ya kizazi

Kutokwa na makamasi mengi ukeni yanayoweza kuwa ya rangi ya maji, pinki, au kuwa na michirizi yad amu. Dalili hii ni kiashiria cha kutoka kwa kifuniko cha shingo ya kizazi ambacho huzuia vimelea kutoka ukeni kuingia kwenye kizazi. 


Makamasi yanaweza kutoka kwa dakika chache, masaa au siku kadhaa kabla ya uchungu kuanza. Dalili hii huwa haigunduliwi na wanawake wengi.


Maumivu ya mgongo

Maumivu mara nyingi huwa ya mgongo wa chini yaani katika maeneo ya kiuno, ambayo huwa endelevu na huwa makali ya kutovumilika kwenye hatua za mwisho za uchungu. Maumivu haya yanahusishwa kusababishwa na mgandamizo kwenye via na mishipa ya fahamu ya mfuko wa matumbo(peritoniamu) kutokana na unaoletwa na kukua kwa kizazi.


Hisia za kujisaidia

Ni ishara ya mgandamizo kwenye matumbo na kibofu cha mkojo hivyo kupelekea hisia za kutaka kujisaidia. Hi pia humaanisha mtoto anajongea uelekeo wa kutoka nje ya kizazi kwa jina jingine mtoto kushuka. Mara nyingi hizia hizi huletwa na mgandamizo wa kichwa cha mtoto kwenye maeneo tajwa.


Kupasuka kwa chupa ya uzazi

Kati ya wanawake 10, mjamzito mmoja hupata dalili hii ambayo hutokea sana nyumbani wakati umelala. Baadhi ya nyakati chupa ya uzazi hupasuka kwenye uchungu na wakati mwingine hupasuliwa kwneye hatua ya pili ya uchungu.


Baadhi ya nyakahu huwa ni vigumu kutofautisha kati ya mkojo na maji ya chupa ya uzazi. Hata hivyo kupasuka kwa chupa ya uzazi huambatana na maji mengi yanayochuruzika kwenye mapaja kama mtu amesimama na huwa meupe, hayana harufu na hutoka mengi kwa ghafla au kuendelea kumwagika taratibu.


Kama ukipata dalili hii hakikisha kuwa si mkojo kwa kunusa, na kama ikionekana si mkojo unapaswa kuzingatia utoshiriki ngono au kutumia pedi ya kuchomeka ukeni au kufanya chochote kinachoweza kuingiza bakteria ukeni. Wakati huu onana na mtoa huduma ya afya. 


Maji yakiwa na rangi tofauti na maji au harufu huweza kuashiria, maambukizi, au kuchanganyika  na choo cha mtoto.


Mabadiliko ya urefu na upana wa shingo ya kizazi

Shingo ya kizazi huwa fupi na nyembamba. Hii ni ishara kwamba sehemu ya chini ya kizazi inajiandaa kwa ajili ya kutoa mtoto kwa kuwa shingo kuwa nyembamba hufanya iweze kutanuka kirahisi Zaidi. Dalili hii hupimwa na mtaalamu wa afya kwa kutia vidole viwili ukeni ili kuifikia shingo ya kizazi.


Ongezeko kipenyo cha shingo ya kizazi

Kuongezeka kwa kipenyo cha shingo ya kizazi ni dalili inayoashiria kufunguka kwa njia ya uzazi ili kichwa cha mtoto. Kizio cha kipimo hiki ni sentimita na kipenyo cha mwisho cha kutanuka ni sentimita 10. Dalili hii huwezi kuifahamu mwenyewe, mtaalamu wa afya hupima shingo ya kizazi kupitia uke kutumia vidole viwili kila baada ya masaa 2 hadi 4 ikitegemea hatua ya uchungu uliyonayo. Hatua za awali za uchungu huweza kuchukua muda kabla ya kwenda kuwa uchungu wa kujifungua


Je, ni salama kujifungua wiki ya 41?

Katika kipindi hiki, unakuwa umebakisha siku chache kabla ya kujifungua. Ingawa mtoto anakuwa amekamilika uumbaji wa viungo na mifumo mingi, wakati huu endapo mimba itaendelea, mtoto huendelea kuongezeka uzito na kuimarika kwa mfumo wa upumuaji na fahamu.


Endapo uchungu utatokea, daktari ataruhusu uendelee na baada ya kujifungua unaweza kuwekwa chini ya uangalizi maalumu kwa masaa machache kadhaa kabla ya kuruhusiwa nyumbani wewe na mwanao.


Wakati huu kama uchungu haujaanza unaweza kufanya mazoezi ya kulea uchungu na kutumia chai ya majani ya chai kwa wingi. Pia unaweza kushiriki ngono ili kupelekea uchungu kutokea. Inashauriwa usitumie dawa za kuamsha uchungu mpaka uchungu utakapoanza wenyewe ili kuepuka madhara.


Kama uchungu hautaanza wenyewe na kukaonekana hatari ya kutoanza mapema, daktari ataagiza kipimo cha picha sauti ya tumbo kuangalia hali ya mtoto tumboni pamoja na kiasi cha maji katika chupa ya uzazi ili kuhakikisha kuwa anendelea vema wakatu uchungu unasubiriwa.

ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

21 Julai 2023, 15:36:46

Rejea za dawa

  1. Pregnancy week by week. Week 41. https://www.thebump.com/pregnancy-week-by-week/41-weeks-pregnant. Imechukuliwa 20.07.2023

  2. Hutchison J, et al. Stages of Labor. 2023 Jan 30. In: StatPearls [Internet]. Treasure Island (FL): StatPearls Publishing; 2023 Jan–. PMID: 31335010.

  3. Melzack R, et al. Low-back pain during labor. Am J Obstet Gynecol. 1987 Apr;156(4):901-5. doi: 10.1016/0002-9378(87)90349-8. PMID: 2953242.

  4. Signs and Symptoms of Labor. https://americanpregnancy.org/healthy-pregnancy/labor-and-birth/signs-of-labor/. Imechukuliwa 18.07.2023

  5. William’s Obstetrics Twenty-Second Ed. Cunningham, F. Gary, et al, Ch. 17.

  6. NHS. Pregnancy signs. https://www.nhs.uk/pregnancy/labour-and-birth/signs-of-labour/signs-that-labour-has-begun/. Imechukuliwa 18.07.2023

  7. Cleveland clinic. 8 Signs That Labor Is 24 to 48 Hours Away. https://www.google.com/search?q=labor+symptoms&client. Imechukuliwa 18.07.2023

  8. NCBI. Stages of labor. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK544290/#:. Imechukuliwa 18.07.2023

bottom of page