Mwandishi:
Dkt. Salome A, MD
Mhariri:
Dkt. Mangwella S, MD
11 Desemba 2021, 15:11:12
Presha sugu kwa mjamzito
Shinikizo la juu la damu ni miongoni mwa magonjwa yanayojitokeza sana wakati wa ujauzito, na humaanisha kupanda kwa shinikizo la damu ambapo shinikizo la sistoliki kwa dayastoliki ni sawa na 140/90 mmhg au zaidi.
Aina za shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito
Kuna aina nne za magonjwa ya shinikizo la damu la juu wakati wa ujauzito ambazo ni;
Shinikizo la juu la damu bila protini kwenye mkojo
Shinikizo la juu la damu lenye protini kwenye mkojo bila/na kifafa cha mimba
Shinikizo la juu la damu sugu
Shinikizo la juu la damu sugu linaloambatana na protini kwenye mkojo.
Katika makala hii tutazungumzia zaidi kuhusu shinikizo la damu la juu sugu.
Shinikizo sugu la damu
Hufahamika pia kama presha ya kupanda iliyo sugu. Shinikizo la damu la juu sugu kwa mjamzito humaanisha kupanda kwa shinikizo la damu kwa kiwango cha 140/90 mmgh au zaidi kabla ya kuwa mjamzito au wakati wa ujauzito kabla ya wiki 20 za umri wa mimba,na shinikizo kuendelea kuwa juu wiki 12 baada ya kujifungua. Aina hii ya shinikizo la juu la damu haina uhusiano wowote na ujauzito, na huwapata wanawake ambao tayari wana tatizo la shinikizo la juu la damu hata kabla ya ujauzito au wale wanaopata tatizo hili kutokana na sababu mbali mbali wakiwa tayari ni wajawazito kwa mfano magonjwa ya figo, kisukari nk na wakati mwingine huwa hakuna sababu yoyote inayoweza kugundulika kitaalamu.
Epidemiolojia
Shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito ni tatizo kubwa na inakadiriwa kuwa asilimia 10 ya wajawazito huwa na shinikizo la juu la damu ambapo asilia 5 husababishwa na shinikizo la juu la damu sugu. Athari nyingi za shinikizo la juu la damu sugu hutokea endapo shinikizo litakuwa juu sana na huweza kusababisha aina nyingine za shinikizo la juu la damu zinazohusiana na ujauzito.
Ni nini sababu ya shinikizo la juu la damu sugu kwa mjamzito?
Kama ilivyoainishwa hapo awali aina hii ya shinikizo la juu la damu hutokea hata kabla ya ujauzito, hata hivyo asilimia kubwa ya wagonjwa huwa hawana kisababishi maalum na endapo mjamzito atagundulika na tatizo hili baada ya wiki 2 uchunguzi zaidi hutakiwa kufanyika ili kubaini visababishi kama vile;
Kisukari
Magonjwa sugu ya figo
Magonjwa ya moyo
Obeziti nk
Dalili na viashiria vya shinikizo la juu la damu sugu kwa mjamzito
Asilimia kubwa ya wagonjwa huwa hawaoneshi dalili yoyote na mara nyingi hugundulika kupitia vipimo vya shinikizo la damu, zifuatazo ni dalili zinazoonekana sana.
Maumivu ya kichwa
Kuhisi mapigo ya moyo
Kuhisi kizunguzungu
Kutokuona vizuri
Kuvimba miguu
Aidha dalili na viashiria tajwa hapo juu huambata na dalili zingine za maradhi/ugonjwa ulipoelekea shinikizo la juu la damu.
Madhara ya shinikizo la juu la damu sugu kwa mjamzito
Madhara na athari hutegemea kiwango cha shinikizo la damu na muda ambao shinikizo la damu limekuwa juu bila kudhibitiwa ili liwe katika kiwango kinachotakiwa kwa muda mrefu. Kwa wajawazito ambao shinikizo la damu limedhibitiwa na liko katika kiwango kinachotakiwa hupata madhara kidogo au kutokupata kabisa madhara ya shinikizo la damu la juu sugu.
Madhara ya shinikizo la juu la damu sugu kwa mjamzito
Huweza kusababisha shinikizo sugu linaloelekea kifafa chamimba.
Kung’oka kwa kondo la nyuma kabla ya muda wake
Moyo kupanuka
Figo kufeli
Kiharusi
HELLP syndrome
Ugonjwa wa ubongo
Madhara ya shinikizo la juu la damu sugu kwa mtoto
Kuzaliwa njiti
Kudumaa akiwa tumboni
Kufia tumboni
Vipimo kwa mjamzito mwenye shinikizo la juu la damu sugu
Vipimo hufanyika ili kubaini athari za ugonjwa katika mwili na kuangalia maendeleo ya mtoto kwa ujumla, na wakati mwingine kubaini chanzo cha kupanda kwa shinikizo la damu hususani kwa wajawazito wanaogundulika kabla ya wiki 20 za umri wa mimba.
Vifuatavyo ni vipimo vya msingi kwa mjamzito mwenye shinikizo la juu la damu sugu;
Kipimo cha picha ya damu
Ultrasound ya moyo
Kipimo cha figo
Kipimo cha ini
Ultrasound ya uzazi
Matibabu ya shinikizo la juu la damu sugu kwa mjamzito
Dawa zinazotumika kwa mjamzito
Zipo dawa nyingi zinazo punguza shinikizo la juu la damu, hataivyo si dawa zote zinafaa kutumika wakati wa ujauzito. Baadhi ya dawa husababisha watoto kudumaa wakiwa tumboni na kuzaliwa na kasoro za kimaumbile.Dawa zilizofanyiwa utafiti na kuonekana ni salama kwa mjamzito ni Methyldopa, Nifedipine na labetalol .
Methyldopa inapendekezwa kutumika kama dawa ya kwanza kabla ya kuongeza dawa nyingine, mgonjwa huanzishiwa dozi cha chini hadi dozi ya juu kulingana na namna ambavyo shinikizo lake la damu linavyoshuka kwa dozi. Shinikizo la damu linaposhindikana kushuka baada ya kufika dozi ya juu ya Methyldopa basi dawa zizngine huongwezwa.
Kwa mwanamke ambaye ana na shinikizo la juu la damu na yupo kwenye matibabu hubadilishiwa dawa mara tu anapogundulika kuwa ni mjamzito na kuanza kutumia dawa salama zinazopendekezwa.
Matibabu kulingana na kiwango cha shinikizo la damu
Kwa mgonjwa mwenye shinikizo la juu la damu kwa kiwango kidogo na cha kati (shinikizo la juu kati ya 140-159 mmhg au shinikizo la chini 90-109 mmhg).
Huweza kutibiwa kwa mapumziko,na kupunguza kiwango cha chumvi na mafuta katika chakula endapo amegundulika kwa mara ya kwanza, wengi hurejea katika shinikizo la damu la kawaida na inaposhindikana huanzishiwa dawa.Kwa yule ambaye alikuwa na ugonjwa kabla ya ujauzito huendelea na dawa zinazopendekezwa.
Mgonjwa huendelea kufuatiliwa katika kliniki ya ujauzito kuangalia maendeleo ya mama na mtoto .
Kwa mgonjwa mwenye shinikizo lililopanda sana (shinikizo juu 160 mmhg au zaidi na shinikizo la chini 110 mmhg au zaidi)
Endapo amegundulika kwa mara ya kwanza huanzishiwa dawa, na yule aliyekuwa na ugonjwa kabla ya ujauzito huendelea na dawa.Dawa huanzishwa moja baada ya nyingine kuanzia dozi ya chini hadi dozi ya juu, lengo ni kuhakikisha na kuhakikisha shinikizo la damu linakuwa kati ya 130-150 mmhg kwa shinikizo la juu, na shinikizo la chini kati ya 90-100 mmhg.
Mgonjwa huendelea kufuatiliwa kliniki kila baada ya wiki mbili mpaka anapofika wiki ya 34 na kasha kila wiki hadi wiki ya 38 ambapo anatakiwa kuwa amejifungua.
Kwa mgonjwa ambaye shinikizo la damu limepanda kwa zaidi ya 180/110 mmhg hutibiwa kama dharura ambapo dawa aina nyingi huanzishwa, na endapo hali ya mama inazidi kuwa mbaya ujauzito husitishwa bila kujali umri wa mimba kwa wiki.
Unawezaje kujikinga na shinikizo la juu la damu sugu?
Ili kuepuka shinikizo la juu la damu na shinikizo la juu la damu sugu wakati wa ujauzito, wanawake wote ambao wapo katika umri wa kubeba mimba wanapaswa kufanya yafuatayo;
Kuwa na uzito unaoshauriwa kiafya
Kuepuka vyakula taka na Kula mlo wa kiafya
Kuepuka chumvi ya mezani
Kufanya mazoezi
Kuacha pombe na sigara
Kuwa na kawaida ya kupima shinikizo la damu
ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
24 Desemba 2021, 10:37:47
Rejea za dawa
Alessia Mammaro et al. Hypertensive Disorders of Pregnancy. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3279097/. Imechukuliwa 07.12.2021
Lara A. Friel. Hypetension in Pregnancy. https://www.msdmanuals.com/professional/gynecology-and-obstetrics/pregnancy-complicated-by-disease/hypertension-in-pregnancy. Imechukuliwa 07.12.2021
Muhimbili National Hospital (MNH). TREATMENT GUIDELINES Obstetric and Gynaecological Disorders. Department of Obstetrics and Gynaecology AUGUST, 2019. (P.38)