Mwandishi:
Dkt. Mangwella S, MD
Mhariri:
Dkt. Benjamin L, MD
31 Julai 2021 12:08:58
Ujauzito uliopitiliza tarehe
Ujauzito kupitiliza umri hufahamika kwa majina mengine ya ‘ujauzito uliopitiliza tarehe’ au ‘uliopitiliza muda’, hutokea endapo mjamzito hajajifungua katika tarehe ya matarajio ya kujifungua baada ya kutimiza wiki 40 kamili au siku 280 za ujauzito.
Mama huwa na furaha sana anapokaribia tarehe ya kujifungua kwa kuwa huwa na matarajio makubwa ya kumwona mtoto aliyembeba kwa miezi tisa. Hata hivyo mama huweza kupata msongo au kuhofu kubwa kama atapitiliza tarehe za makadilio. Kama hakuna shida yoyote kwenye ujauzito, hupaswi kuwa na wasiwasi kama tarehe zimepitiliza. Ujauzito uliopitiliza umri ni tofauti na 'ujauzito uliopita muda' ambao huelezewa kuwa ni ujauzito uliopitiliza wiki 42 kamili za ujauzito au uliopitiliza siku 294 za ujauzito. Licha ya kufananaujauzito uliopita muda huwa na madhara zaidi kuliko ujauzito uliopitiliza tarehe.
Wakati gani ujauzito utaitwa umepitiliza siku zake?
Kama ujauzito utaendelea na kutimiza wiki 40 kamili za ujauzito, huitwa ‘ujauzito uliotimiza muda’ na kama mama atajifungua kabla ya kutimiza wiki 37 kamili za ujauzito, itaitwa ‘ujauzito usiotimiza muda’ na ujauzito uliopitiliza wiki 42 kamili huitwa ‘ujauzito uliopitiliza muda’, ‘ujauzito wa muda mrefu’ ‘ujauzito mrefu’n.k. Kujifungua kabla ya muda au baada ya muda huweza sababisha madhara kwa mtoto na mama.
Usahihi wa makalilio ya tarehe ya kujifungua
Inakadiliwa wanawake 60 kati ya 100 hujifungua kabla ya tarehe ya matarajio yakujifungua.
Wanawake 35 kati ya 100 hupata uchungu asili ndani ya wiki mbili baada ya muda wa ujifungua.
Wanawake 5 kati ya 100 huweza kuchukua muda mrefu zaidi ya wiki mbili kupata uchungu
Taarifa hizi zinathibitisha kuwa, njia za makadilio ya tarehe ya kujifungua huwa hazina ufanisi wa asilimia 100.
Sababu za ujauzito kupitiliza tarehe ya kujifungua
Mara nyingi hakuna sababu inayofahamika kusababisha ujauzito kupitiliza muda, hata hivyo sababu za kijeni au kurithi huambatana sana. Wajawazito wenye historia ya kupitiliza tarehe ya kujifungua katika ujauzito uliopita, wanaweza kupitiliza tarehe hizo katika ujauzito huu.
Je kuna madhara ya kujifungua baada ya wiki 40 za ujauzito?
Kujifungua baada ya wiki 40 za ujauzito mara nyingi huwa hakumdhuru mtoto wala mama. Hata hivyo ili kuwa kwenye usalama zaidi, mkunga au daktari watafanya uchunguzi wa mama na mtoto na kama hana shida yoyote unaweza kuanzishiwa uchungu ndani ya muda wa wiki mbili.
Je ujauzito kupitiliza tatehe ni tatizo?
Wiki la kwanza baada ya kutimiza wiki 40 kamili za ujauzito, hakuna hatari kubwa ya kupata madhara kwa mama na mtoto kama wana afya njema, naam hata baada ya wiki moja kupitiliza, hakuna ongezeko la mtoto kupatwa na lolote licha ya kuongezeka kwa vihatarishi vya;
Kondo la nyuma kuacha kufanya kazi zake
Ujauzito kupata maambukizi
Mtoto mkubwa
Mtoto kuacha kukua tomboni
Mtoto kuvuta kinyesi chake
Matatizo kwa mama
Matatizo wakati wa kujifungua ( kutokwa na damu nyingi, kuchanika msamba, shingo ya kizazi)
Kujifungua kwa upasuaji
Hatari zinazoambatana na ujauzito kupitiliza zaidi wiki mbili
Mara nyingi watoto huzaliwa ndani ya wiki mbili baada ya kutimiza wiki 40 za ujauzito. Kama ujauzito utapitiliza wiki tatu hadi nne , ujauzito huu utakuwa na hatari kubwa ya mtoto kufia tumboni. Hata hivyo mara nyingi hatari hii huwa haitokei kutokana na mama kuanzishiwa uchungu kwa njia za kitabibu mara atakapotimiza wiki 42 za ujauzito.
Tarehe ya kujifungua hutambuliwaje?
Ni muhimu mama ufahamu tarehe ya makadilio ya kujifungua ili kufanya maamuzi mbalimbali mfano ya lini uchukue likizo ya mateniti, ujifungulie wapi na kwa namna gani, nani aje kukusaidia baada ya kujifungua n.k. Licha ya kuwa na umuhimu wa kufahamu hayo, njia mbalimbali zinazotumika kukadilia tarehe ya kujifungua hazina majibu ya uhakika wala ufanisi wa asilimia 100. Njia kuu mbili zinazotumika kukadilia tarehe ya kujifungua ni;
Makadilio ya tarehe ya mwisho kuona hedhi
Kipimo cha picha ya mawimbi sauti ( ultrasound)
Kutambua tarehe ya kujifungua kwa tarehe ya mwisho kuona hedhi
Muda wa kubeba ujauzito hukadiliwa kuwa wiki 40 kamili au siku 280 licha ya ujauzito chache kufikisha wiki hizi 40 . Siku ya kwanza ya wiki 40 za ujauzito huhesabiwa kuanza siku yako ya kwanza kuona hedhi ya mwisho. Makadilio haya ya kutumia tarehe hata hivyo si ya kutegemewa sana kwa sababu mara nyingi wajawazito huwa hawakumbuki siku halisi. Baadhi ya wajawazito huendelea kuona hedhi nyepesi mwanzaoni baada ya kupata ujauzito, hii inaweza kupelekea ugumu wa kutambua ujauzito uliingia tarehe ngapi. Wanawake huwa hawana siku za hedhi zinazofanana yaani wiki 4 au siku 28 ambazo wengi hutumia kuhesabu tarehe ya matazamio, hii inaweza changia pia kupata tarehe ya kujifungua ambayo si sahihi kama mahesababu yakifanyika kwa kutumia siku 28. Kutokana na vipingamizi vingi vinavyoweza kuathiri tarehe ya ya makadilio ya kujifungua, wataalamu wa afya hukadilia kwa kutumia kipimo cha picha ya mawimbi ya sauti kilichofanyika mwanzoni mwa ujauzito ili kupata tarehe ya matarajio ya kujifungua yenye uhakika zaidi.
Kutambua tarehe ya kujifungua kwa kipimo cha picha ya mawimbi sauti
Kipimo cha ultrasound hufanyika kwa kutumia mawimbi sauti yanayoelekezwa kwa mtoto kisha kutengeneza picha halisi ya mtoto. Kama kipimo hiki kikifanyika kipindi cha kwanza cha ujauzito huwa na uwezo wa kutambua tarehe ya makadilio ya kujifungua yenye uhakika zaidi ingawa huweza kuwa na utofauti wa muda wa siku 3 hadi wiki moja. Ni muhimu sana mama mjammzito kufanya kipimo hiki mwanzoni kabisa mwa ujauzito na kutunza majibu yake kwa matumizi ya baadae.
Mambo mengine yanayoweza kuonekana kwenye picha ya mawimbi sauti
Licha ya kuwa na uwezo wa kutambua tarehe ya makadilio ya kujifungua na umri wa ujauzito katika wiki, picha ya mawimbi sauti ya ujauzito huweza kutambua hali ya afya ya mtoto ikiwa pamoja na;
Kuona maendeleo ya ukuaji wa viungo mbalimbali
Kuchunguza mapigo ya moyo ya mtoto
Kuangalia sehemu kondo la nyuma lilipojishikiza katika kizazi
Kupima uzito wa mtoto
Kutambua madhaifu ya kimaumbile ya mtoto
Namna gani maendeleo ya mtoto hutambuliwa?
Kufanyiwa uchunguzi wa tumbo la ujauzito wakati wa kliniki na mkunga au daktari huweza kutambua maendeleo ya mtoto tumboni. Kama tarehe ya kujifungua zimepitiliza unaweza kupangiwa tarehe nyingine ya kuhudhuria kliniki ili kufanyiwa uchunguzi kama vile kipimo cha mapigo ya moyo ya mtoto na kipimo cha picha mawimbi sauti ya ujauzito. Kipimo cha mapigo ya moyo hutumika kuchunguza hali ya mapigo ya moyo ya mtoto na kile cha picha ya mawimbi sauti hutumika kuchunguza uzito wa mtoto, kiasi cha maji kwenye chupa ya uzazi n.k. Daktari pia atakupima kama una dalili za maambukizi mfano endapo kuna ishara ya kuvuja kwa maji ya chupa ya uzazi n.k Kipimo kingine kinachofanyika ni kuhesababu idadi ya mapigo ya mtoto kwenye kuta za uzazi wakati anacheza Hata hivyo kama ujauzito una afya njema na hakuna kihatarishi cha kujifungua, daktari wako anaweza kukushauria uanzishiwe uchungu ili ujifungue.
Wakati gani uchungu huanzishwa kwa ujauzito uliopitiliza muda?
Maamuzi ya uchungu kuanzishwa au kutoanzishwa yanabakia kwa mama mjamzito baada ya kupatiwa ushauri wa kina na daktari. Mambo yanayoweza athiri kuanzishiwa uchungu ni;
Idadi ya wiki zilizopitiliza
Umri wa mama mjamzito
Idadi ya uzazo alionao
Hali ya uvutaji wa sigara
Idadi ya alama za bishop
Uzito wa mjamzito
Uzito wa mtoto tumboni
Hali ya mtoto tumboni
Kiasi cha maji ya chupa ya uzazi
Daktari atashauri kuanzishwa kwa uchungu kama ujauzito unahatari ya kupata madhara na kama madhara hayo sio makubwa kiasi cha kuhitaji kujifungua kwa upasuaji. Hata kama hakuna dalili ya madhara, kuanzishiwa uchungu ni jambo litakalofikiriwa kwanza kama ujauzito umeshatimiza wiki 40 kamili. Tafiti zinaonyesha kuanzisha uchungu kwa ujauzito uliopitiliza wiki moja hupunguza hatari ya mtoto kufia tumboni licha ya hatari hiyo kuwa ndogo kwa kiasi cha watoto watatu kwa kila ujauzito elfu moja kama uchungu haukuanzishwa.
Idadi ya wiki zilizopitiliza
Inashauriwa katika tafiti nyingi kuanzisha uchungu baada ya ujauzito kupitiliza wiki 41 ili kuepika madhara kwa mama na mtoto, hata hivyo ni lazima kuanzishwa kwa uchungu kama ujauzito umepitiliza zaidi ya wiki 42 ili baada ya kufanya vipimo kuthibitisha kuwa unaweza kujifungua kwa njia ya kawaida.
Umri wa mama mjamzito
Mama kuwa na umri mkubwa zaidi ya miaka 35 au chini ya miaka 18 ni kitaweza kumfanya daktari kuacha kuanzisha uchungu u ili kujifungua kwa njia ya upasuaji.
Idadi ya uzazo wa mama
Kwa mama mjamzito mwenye uzao zaidi ya mmoja, mafanikio ya kuanzishiwa uchungu hupelekea kujifungua kirahisi na salama kuliko wanawake wenye uzao wa kwanza ambapo kuanzishiwa uchungu huweza ambatana na maudhi mbalimbali kama kuvimba kwa mlango wa kizazi n.k. Hatari ya kuchanika kizazi huongezeka kwa wajawazito wenye zao zaidi ya tano.
Hali ya mtoto tumboni
Kama hali ya mtoto tumboni ni nzuri( anacheza vema na mapigo ya moyo yapo kawaida), daktari na mkunga watakuwa na uhakika kuwa utajifungua mtoto kwa usalama, lakini kama mapigo ya moyo ya mtoto hayaendi vema, utashauriwa kujifungua kwa njia ya upasuaji kwa kuwa itakuwa salama zaidi ya kujifungua kwa njia ya kawaida.
Kiasi cha maji ya chupa ya uzazi
Kuwa na kiasi cha kawaida cha maji kwenye chupa ya uzazi yaani AFI zaidi ya srntimita 27 kutaleta mafanikio ya kuanzishiwa uchungu na kujifungua mtoto salama. Kuanzishiwa uchungu wakati una kiasi kidogo cha maji kwenye chupa ya uzazi huambatana na matatizo mbalimbali kwa mtoto.
Uzito wa mtoto tumboni
Mtoto kuwa na uzito kati ya kilo 2.5 hadi 3.9 huambatana na mafanikio ya kujifungua vema baada ya kuanzishiwa uchungu. Kuwa na uzito zaidi ya kilo 4 huambtanana na matatizo ya kujifungua kwa njia ya uke kama vile, kukwama bega la mtoto, mtindio wa ubongo kwa mtoto, mama kutokwa na damu nyingi, fistula kwa mama n.k. Utapimwa uzito wa mtoto wako kabla ya kuanzishiwa uchungu, kama utakuwa zaidi ya kilo 4 utashauriwa kujifungua kwa njia ya upasuaji.
Jumla ya alama za bishop
Kuwa na alama za Bishop chini ya 7 huambatana na kujifungu kwa njia ya upasuaji na kama utajifungua kwa kuanzishiwa uchungu, mata nyingi mtoto atahitaji uangalizi maalumu, hata hivyo kuwa na alama zaidi ya 7 huleta huongeza uhakika zaidi wa mafanikio ya kujifungua muda mfupi baada ya kuanzishiwa uchungu na kupata matokeo mazuri kwa mama na mtoto. Maelezo zaidi kuhusu kipimo cha alama za Bishop, soma sehemu nyingine kwenye tovuti hii ya ulyclinic.
Faida za kuanzisha uchungu baada ya ujauzito kupitiliza muda
Kuanzisha uchungu baada ya ujauzito kupitiliza muda huwa na faida ambazo ni;
Kupunguza hatari ya mtoto kufia tumboni
Kupunguza matatizo ya uchungu na kujifungua kwa mama na mtoto
Kupunguza hatari ya kutokwa na damu nyingi
Kupunguza hatari ya mtoto kupata maambukizi tumboni
Mambo gani ufanye ili kuanzisha uchungu asili?
Kuna njia nyingi asili za kuanzisha uchungu kama vile kufanya matembezi marefu, kushiriki ngono, kutomasa chuchu, kutumia dawa asili kama mafuta ya nyonyo n.k. baadhi ya njia zimeelezewa kwenye aya inayofuata.
Kunzisha uchungu kwa kufanya ngono
Njia ya ngono hutumia nadharia ya kwamba, mwanamke anapofika kileleni na kumwagiwa manii, shingo ya kizazi hulegea na kufunguka na hivyo huamsha uchungu. Tafiti zimefanyika na kuonyesha kuwa njia hii haina ufanisi mkubwa.
Kuanzisha uchungu kwa kutomasa chuchu
Tafiti iliyofanyika kwa wanawake 400 wenye ujauzito uliopitiliza muda ambapo kundi moja walitomasa chuchu na jingine hawakutomasa chuchu ilionyesha kuwa.
Bila kutomasa chuchu- wanawake 8 kati ya 100 ambao hawakutomasa chuchu hujifungua ndani ya masaa 72
Kwa kutomasa chuchu- wanawake 39 kati ya 100 hupata uchungu ndani ya masaa 72
Faida za kutomasa chuchu
Mbali na kuwa na faida ya kuanzisha uchungu kwa wanawake wasio na tatizo la kiafya, kutomasa chuchu huwa na faida ya kupunguza hatari ya mama mjamzito kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua.
Kuna njia nyingine asili za kuanzisha uchungu?
Kuna njia nyingine nyingi ambazo hutumiwa na wajawazito kuanziha uchungu kama vile, kunywa dawa za asili za kuanzisha uchungu, kunywa chai yenye majani mengi ya chai, kunywa mafuta au juisi ya mbegu za nyonyo. Baadhi ya njia zinaripotiwa kufanya kazi, hata hivyo kabla ya kutumia njia hizo unashauriwa kuwasiliana na mkunga au daktari wako ili akushauri kama ni salama kulingana na afya yako na mtoto tumboni.
Njia za kitabibu za kuanzisha uchungu
Kuna njia nyingi za kitabibu za kuanzisha uchungu kwa wamama waliopitiliza siku zao. Njia hizo ni;
Kufungua kuandaa shingo ya uzazi
Kupasua chupa ya uzazi
Kutumia dawa za kuanzisha uchungu
Kufungua shingo ya uzazi
Njia ya kwanza ya kuanzisha uchungu ni kuifayia shingo ya kizazi maandalizi ya kuwa tayari kupitisha mtoto kabla ya uchugu kuanza. Mwili unapojiandaa kujifungua, hutoa homoni ya prostaglandin inayoandaa shingo ya kizazi kwakuifanya iwe laini na kufunguka. Dawa zenye homon ya prostaglandin hutumika kulainisha na kufungua njia ya uzazi, fomu inaweza kuwa kidonge au mafuta yanayowekwa ukeni na mtaalamu wa afya. Njia nyingine inayotumika ni kuingiza mrija unaojazwa maji ili uweze kutanua shingo ya kizazi au kutumia dawa za kuanzisha uchungu kama oxytocin kwa kunywa, kuweka kwenye mishipa au ukeni.
Kupasua chupa ya uzazi
Mara uchungu unapoanza kwa njia zilizotajwa hapo juu, chupa ya uzazi inaweza kupasuliwa ili kuongeza kasi ya uchungu.
Maudhi ya kuanzishiwa uchungu
Njia nyingi za kitabibu za kuanzisha uchungu huwa hazina maudhi, hata hivyo kama yakitokea huwa ni; Maudhi ya dawa jamii ya prostaglandin;
Kichefuchefu
Kutapika
Kuharisha
Kutuwama kwa maji mwilini ( kutokana na oxytocin)
Kushuka kwa kiwango cha sodiamu kwenye damu
Ni maumivu gani utapata ya kuanzishiwa uchungu?
Baadhi ya wanawake huhofia kuwa kuanzishiwa uchungu kutawaletea maumivu makali, hata hivyo wanawake waliojifungua kwa njia asili huripoti kuwa na maumivu makali zaidi kuliko wale walioanzishiwa uchungu. Hii inaweza kusababishwa na shauku kuu ya kupata mtoto kwa wanawake wenye ujauzito uliopitiliza muda. Kuanzishwa kwa uchungu hakumaanishi siku zote kuwa uchungu utakuwa wa muda mfupi, baadhi ya wanawake huchukua muda mrefu mpaka kujifungua. Uchunguzi wa karibu utafanyika kwa wanawake walioanzishiwa uchungu ili kuangalia hali ya afya ya mtoto tumboni na vihatarishi vingine vinavyoweza kubadili mtazamo wa matibabu.
Je kuanzisha uchugu ni jambo la dharura?
Hapana! Kuanzisha uchungu si jambo linalopaswa kuwa la dharura, unapaswa siku zote kumpa ushirikiano mkunga au daktari wako ili mshauriane kuhusu njia gani ni salama, faida na hasara na ni wakati gani sahihi kuanzishiwa uchungu.
ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
29 Septemba 2021 18:52:10
Rejea za dawa
Abele H, Bartz C, Franz M, Fischer T, Gembruch U, Gonser M et al. S1-Leitlinie: Vorgehen bei Terminüberschreitung und Übertragung. AWMF-Registernr.: 015-065. February 2014.
Alfirevic Z, et al. Oral misoprostol for induction of labour. Cochrane Database Syst Rev 2014; (6): CD001338. 3. Alfirevic Z, et al. Which method is best for the induction of labour? A systematic review, network meta-analysis and cost-effectiveness analysis. Health Technol Assess 2016; 20(65): 1-584
Chen W, et al. A systematic review and network meta-analysis comparing the use of Foley catheters, misoprostol, and dinoprostone for cervical ripening in the induction of labour. BJOG 2016; 123(3): 346-354
Chen W, et al. Meta-analysis of Foley catheter plus misoprostol versus misoprostol alone for cervical ripening. Int J Gynaecol Obstet 2015; 129(3): 193-198
Gülmezoglu AM, et al. Induction of labour for improving birth outcomes for women at or beyond term. Cochrane Database Syst Rev 2012; (6): CD00494
Heimstad R, et al. Women's experiences and attitudes towards expectant management and induction of labor for post-term pregnancy. Acta Obstet Gynecol Scand 2007; 86(8): 950-956
Kavanagh J, et al. Breast stimulation for cervical ripening and induction of labour. Cochrane Database Syst Rev 2005; (3): CD003392.
Kelly AJ, et al. Castor oil, bath and/or enema for cervical priming and induction of labour. Cochrane Database Syst Rev 2013; (7): CD003099
M.Galal, et al. Postterm pregnancyhttps://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3991404/. Imechukuliwa 27.07.2021.
Nishi D, et al. Hypnosis for induction of labour. Cochrane Database Syst Rev 2014; (8): CD010852
Nuutila M, et al. Women's anticipations of and experiences with induction of labor. Acta Obstet Gynecol Scand 1999; 78(8): 704-709
Shetty A, et al. Women's perceptions, expectations and satisfaction with induced labour - a questionnaire-based study. Eur J Obstet Gynecol Reprod Biol 2005; 123(1): 56-61
Smith CA, et al. Acupuncture or acupressure for induction of labour. Cochrane Database Syst Rev 2017; (10): CD002962 15. Smith CA, et al. Aromatherapy for pain management in labour. Cochrane Database Syst Rev 2011; (7): CD009215
Thomas J, et al. Vaginal prostaglandin (PGE2 and PGF2a) for induction of labour at term. Cochrane Database Syst Rev 2014; (6): CD003101
Errol R Norwitz, et al.Patient education: Postterm pregnancy (Beyond the Basics). https://www.uptodate.com/contents/postterm-pregnancy-beyond-the-basics. Imechukuliwa 27.07.2021
Nuri Peker, et al. Factors Affecting Labor Induction in Late-Term Pregnancies. https://www.researchgate.net/publication/321534801_Factors_Affecting_Labor_Induction_in_Late-Term_Pregnancies. Imechukuliwa 27.07.2021
Sanchez-Ramos L, et al. Labor induction versus expectant management for postterm pregnancies: a systematic review with meta-analysis. Obstet Gynecol 2003;101(6):1312-8. https://doi.org/10.1097/00006250-200306000-00029. Imechukuliwa 28.07.2021
Heuser C, et al. Non-anomalous stillbirth by gestational age: trends differ based on method of epidemiologic calculation. J Matern Fetal Neonatal Med 2010;23(7):720-4. https://doi.org/10.3109/14767050903387086. Imechukuliwa 28.07.2021
Kaimal AJ, et al. Cost-effectiveness of elective induction of labor at 41 weeks in nulliparous women. Am J Obstet Gynecol 2011;204(2):137.e1-9. https://doi.org/10.1016/j.ajog.2010.08.012. Imechukuliwa 28.07.2021