top of page

Mwandishi:

Dkt. Salome A, MD

Mhariri:

Dkt. Mangwella S, MD

21 Novemba 2021, 11:13:25

Image-empty-state.png

Upungufu wa damu kwa mjamzito

Upungufu wa damu humaanisha kupungua kwa kiwango cha chembe nyekundu za damu au kupungua kwa protini ya hemoglobin (protini inayopatikana katika chembe nyekundu za damu) chini ya kiwango cha kawaida, kulingana na umri na jinsia ya mtu.


Kiwango cha chembe nyekundu za damu pamoja na protini haemoglobin hutofautiana kati ya mtu na mtu kulingana na umri, jinsia, muinuko wa makazi kutoka usawa wa bahari na hali ya ujauzito. Upungufu wa damu huwapata zaidi watoto chini ya miaka mitano na wajawazito, inakadiriwa kuwa asilimia 36.5 ya wajawazito ulimwenguni kote hupata tatizo la upungufu wadamu.


Upungufu wa damu wakati wa ujauzito hupelekea athari mbalimbali kwa mama na mtoto kama vile kujifungua kabla ya mimba kukomaa, kuzaa mtoto mwenye uzito mdogo, kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua nk.


Kipimo cha upungufu wa damu kwa mjamzito ni kipi?


Wakati wa ujauzito upungufu wa damu humaanisha kiwango cha hemoglobin chini ya gramu 11 katika desilita ya damu wakati wa kipindi cha kwanza na cha tatu cha ujauzito, na chini ya chini ya gramu 10.5 katika desilita ya damu wakati wa kipindi cha pili cha ujauzito.


Kwanini wajawazito wanapata upungufu wa damu?


Wajawazito wapo katika hatari zaidi ya kupata upungufu wa damu kutokana na sababu mbalimbali kabla ya kupata ujauzito na katika kipindi cha ujauzito, pia yapo mabadiliko ya kifiziolojia yanayotokea katika mfumo wa moyo na mishipa ya damu yanayosababisha mjamzito kuwa na kiwango kidogo cha damu ukilinganisha na watu wengine (hali hii haina madhara yoyote). Wajawazito hupata upungufu wa damu unaotokana na upungufu wa madini chuma na folic acid.


Visababishi vya upungufu wa damu kwa mjamzito


Zipo sababu nyingi zinazopelekea upungufu wa damu wakati wa ujauzito. Katika nchi zilizo ukanda wa jangwa la sahara sababu zinachangia sana ni;


  • Lishe duni inayokosa virutubisho muhimu katika utengenezwaji wa damu( mfano folic acid na madini chuma)

  • Maambukizi ya malaria

  • Minyoo.


Aina za upungufu wa damu


Aina za upungufu wa damu kulingana na kiwango cha haemoglobin

Upungufu wa damu umegawanyika katika makundi kadha wa kadha kwa kufuata sababu flani, katika makala hii tutaangalia zaidi makundi ya upungufu wa damu kwa mujibu wa kiwango cha protini ya hemoglobin katika chembe nyekundu za damu.

Haemoglobin hupatikana ndani ya chembe nyekundu za damu, imeundwa kwa protini na madini chuma kwahiyo madini chuma ni muhimu sana katika utengenezwaji wa chembe nyekundu za damu.

Zifuatazo ni aina za upungufu wa damu kulingana na kiwango cha hemoglobin


  • Upungufu kiasi wa damu – kiwango cha hemoglobin kati ya 9 hadi 10.5 g/dl

  • Upugufu wa kati wa damu - kiwango cha hemoglobin kati ya 7 hadi 8.9 g/dl

  • Upungufu wa wastani - kiwango cha hemoglobin chini ya 7 g/dl

  • Upungufu mkali - kiwango cha hemoglobin chini ya 4 g/dl


Visababishi


Visababishi vya upungufu wa damu wakati wa ujauzito


Zipo sababu nyingi zinazopelekea uungufu wa damu wakati wa ujauzito, wakati wa ujauzito

Sababu nyingi ni zile zinazopelekea upungufu wa madini chuma na folic acid.


Zifuatazo ni baadhi ya sababu zinazohusishwa sana na upungufu wa damu wakati wa ujauzito;


Ongezekola matumizi ya virutubisho vinavyosaidia katika utengenezwaji wa damu

Virutubisho vinavyosaidia katika kazi hii muhimu ni;



Wakati wa ujauzito matumizi ya virutubishi hivi katika mwili huongezeka ili kukidhi mahitaji ya mama na mtoto aliye tumboni na kupelekea upungufu wa damu. Aidha ujauzito wa mapacha na kubeba mimba mara kwa mara kunaongeza zaidi uhitaji wa virutubisho hivo.


Lishe duni

Lishe duni huweza kusababishwa na ukosefu wa chakula hasa chenye virutubisho vya kuongeza damu au kutokula vizuri kunakosababishwa na hali ya ujauzito kwa mfano hali ya kutapika sana, kukosa hamu ya kula au kubagua vyakula.


Kuvuja au kutokwa na damu

Inaweza kuwa kabla ya kupata ujauzito au wakati wa ujauzito, husababisha upungufu wa madini chuma hivyo kiwango cha damu kushuka. Husababishwa na mambo yafuatayo;


  • Minyoo ambao hufyonza damu katika matumbo lakini pia husababisha kupungua kwa ufyonzwaji wa madini chuma yanayoatikana katika chakula

  • Historia ya kutokwa na damu katika mimba zilizopita

  • Kujifungua mara kwa mara bila kuwa na muda wa kutosha wa kupumzika

  • Damu nyingi ya hedhi kabla ya kupata ujauzito

  • Kutokwa na damu wakati wa ujauzito baada ya wiki 28 au wakati wa kujifungua


Maambukizi

Maambukizi yanayosababisha sana upungufu wa damu wakati wa ujauzito ni malaria, minyoo na ukimwi


Dalili


Dalili na viashiria vya upungufu wa damu wakati wa ujauzito


Hazitofautiani na watu wengine na hutegemea kiwango cha damu kilichopungua na kisababishi, wakati mwingine mgonjwa haoneshi dalili wala viashiria vyovyote na hujulikana ana upungufu wa damu kupitia vipimo wakati wa kliniki.


Zifuatazo ni baadhi ya dalili na viashiria vya upungufu wa damu zinazoonekana sana kwa wajawazito;


  • Kuhisi kuchoka hata bila kufanya kazi yoyote

  • Kuhisi kizunguzungu

  • Maumivu ya kichwa

  • Mapigo ya moyo kwenda mbio

  • Kuvimba miguu

  • Kuwa mweupe kwenye macho, ulimi na viganjani

  • Manjano

  • Kutokwa na vidonda kwenye midomo

  • Kula udongo

  • Dalili za moyo kufeli


Madhara


Athari za upungufu wa damu wakati wa ujauzito


Kwa mama

  • Kupata magonjwa ya shinikizo la damu wakati wa ujauzito

  • Kupata uchungu kabla ya mimba kukomaa

  • Kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua

  • Kukosa maziwa ya kutosha wakati wa kunyonyesha

  • Kupata maambukizi kirahisi hasa baada ya kujifungua

  • Moyo kufeli (inaweza kusababisha kifo cha ghafla hasa wakati wa kujifungua)


Kwa mtoto

  • Kudumaa akiwa tumboni

  • Kuzaliwa na uzito mdogo

  • Kuzaliwa njiti

  • Kufia tumboni

  • Matatizo ya ukuaji hasa wa akili anapokuwa mkubwa


Vipimo


Vipimo vya kufanya kwa mjamzito mwenye upungufu wa damu


Lengo la kufanya vipimo ni kubaini chanzo cha upungufu na kiwango cha damu ili kupanga aina ya matibabu, vipimo hufanyika kulingana na dalili na viashiria alivyonanvyo mgonjwa pamoja na sababu ya upungufu wa damu.


Vifuatavyo ni baadhi ya vipimo vinavyoweza kufanyika;


Kipimo cha picha nzima ya damu


Ni kipimo kinachopima damu kwa ujumla wake yaani chembe nyeupe, chembe nyekundu na chembe sahani. Husaidia kujua aina ya upungufu wa damu, sababu ya upungufu wa damu na kiwango cha damu.


Peripheral blood smear


Ni kipimo kinachosaidia kugundua aina ya upungufu wa damu na maradhi mbalimbali ya damu, damu huwekwa katika filamu ya glasi na kuchunguzwa kupitia hadubini.


Kundi la damu na uoanishaji wa damu


Hufanyika endapo mgonjwa atahitajika kuongezwa damu, damu ya mgonjwa na ya mchangiaji huoanishwa kama zinaendana kwa kuangalia magrupu na protini zinazoatikana kwenye chembe nyekundu za damu.


Kipimo chauwepo wa damu kwenye haja kubwa


Hutumika kubaini minyoo ambao hufyonza damu na kusababisha upungufu wa damu


Kumbuka;


Vipimo ni vingi na hufanyika kulingana na hali ya mgonjwa


Matibabu


Matibabu ya upungufu wa damu wakati wa ujauzito hutegemea mambo makuu manne ambayo ni;


  • Chanzo cha upungufu wa damu

  • Umri wa mimba (je zimebaki wiki ngapi kabla ya kujifungua?)

  • Kiwango cha upungufu wa damu na

  • Athari za upungufu wa damu alizonazo mgonjwa kwa wakati huo (mfano moyo kufeli)


Lengo ni kupandisha kiwango cha damu kufikia kile cha kawaida, kutibu chanzo na athari za muda mfupi za upungufu wa damu ambazo huatarisha maisha. Kwa ujumla wake matibabu ya upungufu wa damu yapo ya aina mbili, kupewa vidonge vya kuongeza damu na kuongezwa damu. Uchaguzi wa matibabu unategemea mambo tajwa haop juu kama ifuatavyo


Dawa za kuongeza damu

Dawa za kuongeza damu huwa na virutubisho vya madini chuma na folic acid na hujulikana kama FEFO, mjamzito anpaaswa kunywa dawa hizi mpaka miezi mitatu baada ya kujifungua ili kuweka akiba ya mdini chuma katika mwili. Lakini pia hupewa ushauri wa lishe na vyakula vyenye virutubisho vinavyosaidia kuongeza damu.


Hutolewa kwa wajawazito wenye upungufu wa kiwango kidogo, kiwango cha kati na kiwango kikubwa cha upungufu wa damu ambao umri wa ujauzito ni chini ya wiki 37, sambamba na dawa hizo chanzo hubainiwa na kutibiwa. Mjamzito hutibiwa kama mgonjwa wa nje na kiwango chake cha damu hufuatiliwa kwa kufanya kipimo cha wingi wa damu kila anapokwenda kliniki ya ujauzito.


Mjamzito aliye na kiwango cha kati na kiwango kikubwa cha upungufu wa damu ambae mimba yake imefikisha wiki 37 au zaidi hulazwa na kupatiwa matibabu akiwa hospitali ili kuweza kuwa na ufuatiliaji wa karibu na wakati mwingine huongezwa damu kwa mafano akihitajiwa kujifungua kwa njia ya uasuaji, hii hufanyika ili kuepuka matatizo yatokanayo na upungufu wa damu wakati wa kujifungua.


Kuongezwa damu

Mjamzito atahitajika kuongezwa damu endapo ana vigezo vifuatavyo;


  • Kiwango kikubwa cha upungufu wa damu kwa mimba iliyofikisha wiki 37

  • Kiwango kikubwa cha upungufu wa damu na kuonesha dalili na viashiria vya upungufu wa damu katika kipindi chochote cha ujauzito

  • Kiwango kikubwa sana cha upungufu wa damu katika kipindi chochote cha ujauzito

  • Upungufu wa damu wa damu unaosababishwa na kutokwa damu nyingi baada ya wiki 28 au baada ya kujifungua

  • Kufeli kwa matibabu ya dawa za kuongeza damu

  • Baada ya kuongezwa damu mgonjwa huendelea kutumia dawa za kuongeza damu hadi muda wa miezi mitatu baada ya kijifungua.


Matibabu mengine hutegemea hali ya mgonjwa na athari za upungufu wa damu alizonazo kwa wakati huo.


Kinga


Ili kuzuia upungufu wa damu wakati wa ujauzito unaweza kufanya mambo yafuatayo


Kuanza kliniki ya ujauzito mapema na kuhudhuria kama ilivyopangwa

Kila mwanamke anashauriwa kuanza kliniki mara tu anapohisi ana ujauzito, kuanza kliniki mapema husaidia kugundua baadhi ya sababu zinazopelekea upungufu wa damu. Pia huduma mbali mbali hutolewa klininki wa wajawazito kuzuia upungufu wa damu kama vile


  • Kufanyiwa vipimo mbali mbali ikiwamo wingi wa damu na ukimwi na kuanzishiwa matibabu

  • Kupewa dawa za minyoo

  • Kupewa dawa za malaria na vyandarua vilivyowekwa dawa

  • Kupewa dawa za kuongeza damu (FEFO)


Elimu ya lishe

Wajawazito wanapaswa kupewa elimu juu ya ulaji wa vyakula sahihi vyenye virutubisho vinavyochochea uzalishwaji wa damu yaani madini chuma na folic acid

Folic acid hupatikana katika chakula katika muundo wa folate, vyakula vifuatavyo vinakiwango kikubwa cha folate mfano;


  • Mboga za majani zenye kijani iliyokolea

  • Matunda na juisi za matunda

  • Karanga

  • Maharagwe

  • Maziwa

  • Mayai nk.


Madini chuma hupatikana kwa wingi kwenye nyama na vyakula vya baharini na kiwango kidogo kwenye mboga za mjani, maharaagwe na nafaka zilizoongezwa virutubisho vya madini chuma.


Matumizi ya uzazi wa mpango

Matumizi sahihi ya uzazi wa mpango husaidia kuzuia upungufu wa damu unaotokana na kuzaa mara kwa mara bila kuwa na muda wa kupumzika walau miaka miwili baada ya kujifungua. Uzazi wa mpango humuwezesha mama kurudisha afya yake na kuwa na akiba nzuri ya madini chuma katika mwili kabla ya kubeba mimba nyingine.


Elimu ya lishe na matumizi ya virutubishi vya kuongeza damu kabla ya ujauzito

Hii itasaidia kuhakikisha wanawake walio katika umri wa kubeba mimba wanakuwa na akiba ya kutosha ya madini chuma na folic acid kabla ya kupata ujauzito.

ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

21 Novemba 2021, 12:14:27

Rejea za dawa

  1. Muhimbili national hospital (mnh). Treatment guidelines obstetric and gynaecological disorders. Department of obstetrics and gynaecology august, 2019. (p.43-45)

  2. Dc dutta’s textbook of obstetrics. Seventh edition: november 2013 (p. 260-264)

  3. Who. Anaemia in women and children.

  4. Https://www.who.int/data/gho/data/themes/toics/anaemia_in_women_and_children

  5. Bruno f. Sunguya et al. High burden of anaemia among pregnant women in tanzania: a call to address its determinants.https://nutritionj.biomedicentral.com/articles/1.11/s12937-21-72-0. Imechukuliwa 20.11.2021

  6. Lara a. Friel. Anemia in pregnacy.https://www.msdmanuals.com/ professional/ gynaecology-and- obstetrics/pregnancy-complicated-by-disease/anemia-in-preagnacy

  7. Folate – health professional fact sheet.https://ods.od.gov/factsheets/folate- healthprofessional/. Imechukuliwa 20.11.2021

  8. Iron - health professional fact sheet – nih office of dietary suplements https://ods.od.nih.gov/factsheets/iron- healthprofessional/. Imechukuliwa 20.11.2021

bottom of page