Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
Dkt. Mangwella S, MD
Ijumaa, 17 Desemba 2021

Chia
Chia ni mbegu zinazotoka katika mmea unaoitwa Salvia hispanica, mmea huu hupatikana sehemu nyingi duniani. Mbegu hizi vimepata umaarufu sana maeneo mengi duniani kuwa ni mbegu zenye faida nyingi kiafya. Mbegu hizi ambazo huwa na uwezo wa kuyeyuka zinapowekwa kwenye majimaji huhitaji kutumiwa kwa muda mrefu kidogo ili kupata faida zake. Makala hii imezungumzia kuhusu faida za kiafya za mbegu hizi.
Virutubisho vinavyopatikana kwenye mbegu za chia ni vipi?
Mbegu ya chia ina virutubisho muhimu oamoja na nishati, baadhi ya virutubisho ilivyonavyo kwa wingi ni;
Nyuzinyuzi
Nishati
Protini
Mafuta ya omega 3
Madini Kalisiamu
Madini manganese
Madini fosforusi
Madini zinki
Madini potasiamu
Vitamin B1,B2 na B3
Ifahamike kuwa vijiko viwili vya chakula vya mbegu hii vina nishati ya kalori 101, chia pia huwa haina protini ya gluten hivyo huwa nzuri kwa wagonjwa wenye aleji na protini hii inayopatikana kwenye ngano n.k.
Faida za kiafya za chia
Faida za kiafya za mbegu ya chia zinaletwa na nyuzinyuzi na virutubisho vilivyomo kwenye mbegu hizi, makala hii imezungumzia faida katika mifumo mbalimbali.
Hutengeneza mazingira mazuri ya umeng’enyaji wa chakula
Kwa kuwa huwa na nyuzinyuzi nyingi, mbegu hizi hufanya shughuli ya umengenyaji wa chakula ifanyike vema mwilini. Hata hivyo chia huwa na uwezo wa kufyonza maji kwa wingi hivyo kukitumia kwenye chakula itakufanya ushibe mapema zaidi. Kwa wale wanaopunguza uzito mbegu hizi ni nzuri kuzitumia kutokana na kufanya ushibe haraka na pa kupata haja laini.
Mbegu hizi pia huwa chakula kizuri cha bakteria marafiki katika utumbo wako, bakteria hawa hutumia chakula hiki na huwa na afya njema. Bakteria hawa wakiwa na afya njema hufanya mfumo wako wa umeng’enyaji uchakula usiwe na matatizo .
Hupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo
Tafiti chache zimeonyesha kuwa mbegu za chia zina uwezo wa kupunguza shinikizo la juu la damu hivyo kupelekea kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo. Hata hvyo tafiti nyingi zaidi zinahitajika kufanyika ili kutambua umuhimu wa mbegu hizi katika kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo.
Huimarisha mifupa
Protini na madini ya kalisiamu, fosforasi, magnesium husaidia sana kwenye afya ya mifupa. Vijiko viwili vya mbegu za chia huwa na kiwango cha asilimia 18 ya madini ya kalisiamu ambao ni muhimu kwa kuimarisha mifupa yako, mtu mwenye upungufu wa madini haya anaweza kuyapata kiasi cha kutosha kwa kula mbegu hizi.
Tafiti zinaonyesha kuwa mbegu hizi huwa na kemikali ya phytic acid ambayo huweza kuzuia ufyonzaji wa madini ya kalisiamu kwa kiasi kidogo.
Kurekebisha kiwango cha sukari kwenye damu
Tafiti kwa zilizofanyika kwa wanyama zinaonyesha kuwa matumizi ya mbegu za chia yanaongeza uwezo wa mwili kutumia sukari kwa kupunguza upinzani wa mwili dhidi ya homoni insulin inayohusika kuondoa sukari kwenye damu. Matumizi ya mbegu hizi huzuia sukari kupanda kwa kiasi kikubwa kwenye damu.
Tafiti zilizofanyika kwa binadamu zinaonyesha kuwa, kiwango cha sukari huwa cha chini endapo mtu akitumia mkate pamoja na mbegu za chia ukilinganisha na mtu ambaye amekula mkate tu bila mbegu hizi.
Hupunguza kiwango cha kiashiria cha uvimbe kwenye damu kwa jina la C-reactive protein (CRP)
Kutokana na tafiti zilizofanyika kwa wagonjwa wa kisukari waliotumia gramu 37 za mbegu hizi za chia kwa siku kwa muda wa miezi mitatu tu, kiwango cha CRP kilionekana kupungua kwenye damu mara dufu zaidi kuliko kwa wale ambao hawakutumia. Kiwango cha CRP huwa kikubwa kwa watu wanaovuta sigara, wasiofanya mazoezi na kutokula vema. CRP hufahamika kuhusiana na saratani na magonjwa mbalimbali ya moyo na mfumo wa tumbo. Hata hivyo faida za kupunguza CRP bado hazifahamiki vizuri, tafiti zinahitajika kufanyika zaidi kutambua faida hizo mwilini.
Matumizi ya kiwango cha juu ya mbegu hizi hupunguza kuamka kwa dalili za ugonjwa wa diverticulosis, sababu ikifahamika kuwa hufyonzaji maji kwenye utumbo na kufanya haja kubwa iwe laini na itoke kirahisi.
Huwa na mafuta ya ya omega-3
Huwa na kiwango kikubwa cha mafuta ya omega 3 aina ya linoleic na alpha-linolenic (ALA) acid ambayo ni vigumu sana kutumiwa na mwili wa binadamu, utahitaji kula lita tano ili utapte kiwango sawa ambacho unaweza kukipata kutoka kwenye vyakula vingine kwa siku.
Mafuta ya omega 3 kutoka kwenye vyanzo vingine (mimea na viumbe wa baharini mfano samaki n.k) huwa na umuhimu mwilini. Tafiti zinaonyesha mafuta ya omega 3 huweza kupunguza kiwango cha kolestro kwenye damu na hivyo kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo. Inashauriwa kutegemea mafuta ya omega -3 kutoka kwenye vyanzo vingine zaidi kuliko kwenye mbegu za chia kwa sababu licha ya kuwa na mafuta haya kwa wingi mwili wako hauna uwezo wa kuyatumia.
Huupa mwili nguvu
Vijiko viwili vya mbegu za chia huwa na kiwango cha nishati za kalori 101. Nishati hii ni muhimu mwilini. Kwa wale wanaotaka kupunguza uzito, kutumia mbegu hizi kwenye maji ya moto wakati wa asuhuhi kabla ya kunywa chai na wakati wa mchana kabla ya kula chakula kutakufanya ujihisi umeshiba na kula kidogo hivyo kuwa kama nyenzo nzuri ya kukufanya ufikie malengo ya kupunguza uzito
Namna ya kutumia mbegu za chia kupata faida za kiafya
Unaweza kutumia mbegu hizi kwa kuweka kwenye vyakula mbalimbali, inashauriwa utumie vijiko viwili mara mbili kwa siku ili kupata faida zake. Tumia mbegu hizi kwa;
Kuwekwa kwenye uji
Kuwekwa kwenye juisi isiyochujwa
Kutumia kwenye mikate iliyokwisha okwa
Unaweza kuzinyunyizia kwenye chakula kingine kama maziwa mtindi, mboga za majani zilizopikwa au wali uliopikwa
Unaweza kutumia kuongeza uzito mchuzi wa chakula chako
Unaweza kutumia kama mbadala wa mayai
Imeboreshwa,
17 Desemba 2021, 06:25:12
Bofya hapa kusoma zaidi kuhusu namna ya kuandaa vyakula mbalimbali vinavyoweza kukukinga dhidi ya magonjwa ya shinikizo la damu la juu na Kisukari, pia kuupa mwili wako uwezo wa kudhibiti magonjwa ya kisukari na shinikizo la juu la damu(presha).
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Rejea za mada hii
Healthline. 22 High Fiber Foods You Should Eat. https://www.healthline.com/nutrition/22-high-fiber-foods. Imechuukuliwa 26.11.2020
Francisco Guarner etal. Gut flora in health and disease. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pubmed/12583961. Imechuukuliwa 26.11.2020
Vladimir Vuksan etal. Supplementation of conventional therapy with the novel grain Salba (Salvia hispanica L.) improves major and emerging cardiovascular risk factors in type 2 diabetes: results of a randomized controlled trial. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pubmed/17686832. Imechuukuliwa 26.11.2020
Janet K Snell-Bergeon etal. Hypoglycemia, diabetes, and cardiovascular disease. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pubmed/22650225. Imechuukuliwa 26.11.2020
Antonio Ceriello, MD. Postprandial Glucose Levels Are a Clinically Important Treatment Target. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC2909084/. Imechuukuliwa 26.11.2020
V Vuksan etal. Reduction in postprandial glucose excursion and prolongation of satiety: possible explanation of the long-term effects of whole grain Salba (Salvia Hispanica L.). https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pubmed/20087375. Imechuukuliwa 26.11.2020
H Ho etal. Effect of whole and ground Salba seeds (Salvia Hispanica L.) on postprandial glycemia in healthy volunteers: a randomized controlled, dose-response trial. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pubmed/23778782. Imechuukuliwa 26.11.2020
Chia seed. The nutrition source. https://www.hsph.harvard.edu/nutritionsource/food-features/chia-seeds/. Imechuukuliwa 26.11.2020
What are the benefits of chia seeds? https://www.medicalnewstoday.com/articles/291334#. Imechuukuliwa 26.11.2020
Is Eating Chia and Flax Enough to Meet Your Daily Omega-3 Needs?. https://www.nordicnaturals.com/healthy-science/is-eating-chia-and-flax-enough-to-meet-your-daily-omega-3-needs/. Imechuukuliwa 26.11.2020