Tetekuwanga ni ugonjwa unaosababshwa na kirusi Varicella zoster AU kirusi tetekuwanga. Ugonjwa huu husababisha harara ndogo na malenge kwenye ngozi yanayoambatana na muwasho.
Dalili za tetekuwanga
Tetekuwanga huonekana siku 10 hadi 21 baada ya kupata maambukizi. Dalili kuu ya ugonjwa huu huwa ni malengelenge madogo yanayowasha na hudumu kwa muda wa siku 5 hadi 10. Dalili zingine zinazoonekana siku 1 hadi 2 kabla ya kuona vipele ni;
Homa
Kukosa hamu ya kula
Maumivu ya kichwa
Kuchoka
Hali ya kuhisi haupo sawa
Hatua za dalili za harara
Mara baada ya vipele kutokea kwenye ngozi hupitia hatua tatu;
Vipele vidogo ambavyo hupasuka siku chache baadae
Malenge madogo yanayotokea siku moja kisha kupasuka
Magamba yanayofunika malenge yaliyopasuka na huchukua siku chache kupona
Vipele vipya huendelea kuonekana kila baada ya siku kadhaa, hivyo mgonjwa anaweza kuwa na vipele, malenge na magamba kwa wakati mmoja.
Maambukizi na kusambaza kwa tetekuwanga
Masaa 48 kabla ya kuonyesha dalili, unaweza kuambukiza watu wengine ugonjwa huu na utaendelea kuambukiza mpaka pale vipele vinapotengeneza magamba.
Ugonjwa huu husambaa kirahisi sana kwa watu ambao hawajapata chanjo ya virusi hivi na ugonjwa unaweza kuathiri watu wengi kwa wakati mmoja. Kwa sasa chanjo inawalinda watoto dhidi ya maambukizi haya.
Njia za kusambaa kwa ugonjwa ni pamoja na;
Kugusana na majimaji ya kikohozi au chafya
Kushika kitu chenye virusi( Vitu ambavyo vimetumiwa na mgonjwa) kama nguo, vyombo n.k
Kushika malengelege ya mgonjwa au mkanda wa jeshi
Ukali wa ugonjwa
Ugonjwa mara nyingi huwa wa kiasi kwa watoto wenye afya njema. Hata hivyo unaweza kutokea kwenye mwili mzima. Malenge huweza kutokea pia kohoni na kwenye tishu za ndani ya yurethra, njia ya haja kubwa na tundu la uke.
Wakati gani wa kumwona daktari
Kama unafikiria kuwa mwanao ana tetekuwanga, wasiliana na daktari wako mara moja. Mara nyingi ugonjwa huu hutambulika kwa dalili na viashiria tu zinazoonekana kwenye mwili wa mtu. Unaweza kuhitaji dawa za kusaidia kupunguza uzalianaji wa virusi au kitibiwa shida zingine ambazo zinasababishwa na tetekuwanga. Ili kuepuka kuambukiza watu wengine, unaweza kupatiwa matibabu nyumbani.
Nini ufanye unapowasiliana na daktari
Kabla ya kuwasiliana na daktari hakikisha unamweleza
Kama upele unasambaa kwenye macho
Kama upele unakuwa wa moto au kuuma
Kama unaishi na watu ambao hawakupata chanjo ya ugonjwa
Kama kuna mjamzito ndani ya nyumba
Kama unaishi na mtu anayetumia dawa zinazoshusha kinga ya mwili
Vihatarishi vya kupata ugonjwa wa tetekuwanga
Vifuatavyo ni vihararishi vya kupata ugonjwa wa tetekuwanga
Kutopata chanjo ya ugonjwa
Kutougua tetekuwanga kabla
Kama umepata chanjo au ulishawahi ugua ugonjwa huu, kama ukipata tena ugonjwa utakuwa na dalili za wastani za kuwa na malenge machache, hata hivyo ni mara chache kupata ugonjwa kwa mara nyingine.
Madhara tetekuwanga
Tetekuwanga mara nyingi ni ugonjwa unaosababisha dalili za wastani. Hata hivyo unaweza kuwa mkali na kupelekea matatizo mengine ya kiafya kama;
Maambukizi kwenye ngozi, mifupa na damu yanayosababishwa na bakteria
Kuishiwa maji mwilini
Nimonia na magonjwa mengine ya mapafu
Kuvimba kwa ubongo
Sindromu ya sumu kutokana na bakteria
Ugonjwa wa Reyes kama mtoto akipewa aspirini
Kifo kwa nadra sana
Nani yupo kwenye hatari ya kupata tetekuwanga?
Watu waliohatarini kupata madhara ya tetekuwanga ni kama wafuatao;
Vichanga na watoto chini ya umri wa mwaka mmoja ambao hawajapata chanjo
Vijana wa umri wa miaka 11 hadi 19 na watu wazima
Wajawazito ambao hawakuwahi kuugua tetekuwanga
Wavuta sigara
Wagonjwa wa saratani au UKIMWI au wanaotumia dawa za kushusha kinga ya mwili
Wagonjwa wenye magonjwa sugu kama pumu, wanaotumia dawa za kushusha kinga ya mwili, au waliofanyiwa upandikizaji wa ogani mwilini na kutumia dawa za kushusha kinga ya mwili.
Kinga ya tetekuwanga
Kupata chanjo ya kirusi cha tetekuwanga ni njia nzuri ya kujikinga na ugonjwa na hata kama ukipata kwa mara nyingine ugonjwa hautakuwa mkali.
Utambuzi wa tetekuwanga
Mara nyingi htuambuliwa kwa dalili na viashiria vinavyoonekana kwenye mwili wa mtoto kwa kuangalia.
Matibabu ya tetekuwanga
Ugonjwa huu mara nyingi hauhitaji tiba kwa watoto wenye afya njema. Baadhi ya watoto wanaweza kupewa dawa za kupunguza mzio ili kupunguza dalili ya muwasho. Hata hivyo mara nyingi matibabu hayahitajiki na ugonjwa unabidi uendelee na kuisha wenyewe.
Matibabu kwa watu wenye hatari ya madhara
Kwa waliohatarini kupata madhara ya ugonjwa kama vile watu wenye upungufu wa kinga kutokana na sababu yoyote wanaweza kuhitaji matibabu ya dawa za kupunguza makali ya kirusi cha tetekuwanga. Dawa zinazotumika mara nyingi huwa ni acyclovir (Zovirax, Sitavig). Hufanya kazi vema kama zikitumika madaa 24 baada ya kuona harara kwa mara ya kwanza.
Dawa valacyclovir (Valtrex) na famciclovir, huweza kupunguza ukali wa ugonjwa pia, hata hivyo zinaweza zisiwe sahihi kwa kila mtu. Unaweza kushauriwa kupata chanjo pia kama itaonekana inafaa kuzuia hatari ya maambukizi mengine.
Matibabu ya nyumbani ya tetekuwanga
Unaweza kufanya mambo yafuatayo kudhibiti dalili za tetekuwanga nyumbani.
Acha kujikuna- kujikuna hupunguza kasi ya kupona na kuongeza hatari ya vidonda sambamba na maambukizi ya bakteria kwenye damu.
Punguza muwasho na homa kwa kufanya mambo yafuatayo:
Kuoga maji ya baridi yaliyotiwa magadisoda, aluminum acetate au shayiri
Kupaka losheni kalamine kwenye eneo linalowasha
Kutumia dawa za kupunguza mzio kama diphenhydramine (Benadryl)- wasiliana na daktari kwanza.
Kutumia parasetamol kwa ajili ya homa
Ongea na daktari wako kama unaweza kutumia dawa zingine kama ibuprofen (Advil, Motrin IB) n.k
Rejea za mada hii
Centers for Disease Control and Prevention. Chickenpox (varicella). https://www.cdc.gov/chickenpox/about/index.html. Imechukuliwa 23.10.2024
Centers for Disease Control and Prevention. Chickenpox (varicella): Vaccination. https://www.cdc.gov/chickenpox/vaccination.html. Imechukuliwa 23.10.2024
Chickenpox. Newyork state. https://www.health.ny.gov/diseases/communicable/chickenpox/fact_sheet.htm#:. Imechukuliwa 23.10.2024
Centers for Disease Control and Prevention. Chickenpox (varicella): Prevention and treatment. https://www.cdc.gov/chickenpox/about/prevention-treatment.html. Imechukuliwa 23.10.2024
Centers for Disease Control and Prevention. Guidelines for vaccinating pregnant women. https://www.cdc.gov/vaccines/pregnancy/hcp-toolkit/guidelines.html. Imechukuliwa 23.10.2024
Centers for Disease Control and Prevention. Shingles vaccination. https://www.cdc.gov/vaccines/vpd/shingles/public/shingrix/index.html. Imechukuliwa 23.10.2024
Centers for Disease Control and Prevention. Types of chickenpox vaccine. https://www.cdc.gov/vaccines/vpd/varicella/public/index.html. Imechukuliwa 23.10.2024
Centers for Disease Control and Prevention. Varicella (chickenpox). In: CDC Yellowbook 2018: Health Information for International Travel. New York, N.Y.: Oxford University Press; 2018. http://global.oup.com/. Imechukuliwa 23.10.2024
Chickenpox vaccination: What everyone should know. https://www.cdc.gov/vaccines/vpd/varicella/public/index.html. Imechukuliwa 23.10.2024
Longo DL, et al., eds. Varicella-zoster virus infections. In: Harrison's Principles of Internal Medicine. 20th ed. New York, N.Y.: The McGraw-Hill Companies; 2018. https://accessmedicine.mhmedical.com. Imechukuliwa 23.10.2024
Merck Manual Professional Version. Chickenpox (varicella). https://www.merckmanuals.com/professional/infectious-diseases/herpesviruses/chickenpox. Imechukuliwa 23.10.2024
Papadakis MA, et al., eds. Viral and rickettsial infections. In: Current Medical Diagnosis & Treatment 2019. 58th ed. New York, N.Y.: McGraw-Hill Education; 2019. https://accessmedicine.mhmedical.com. Imechukuliwa 23.10.2024
ULY CLINIC. Kirusi variella zoster. https://www.ulyclinic.com/virusi/kirusi-varicella-zosta. Imechukuliwa 23.10.2024