Makala hii imezungumzia kuhusu amoxicillin kwenye kipengele chaa magonjwa yanayotibibika na dawa, maudhi ya dawa, Usugu wa vimelea kwenye dawa, na Wakati gani wa kumwona daktari na na tahadhari za kuepuka matumizi ya dawa hii.
Amoxicillin inatibu nini?
Amoxicillin ni dawa ya antibiotiki iliyopo kwenye kundi la penicillin, dawa hii ina wigo mpana wa kutibu maambukizi mbalimbali ya bakteria wanaodhuriwa na dawa. Katika makala magonjwa yanayotibika kwa amoxicillin yameandikwa kwa kuzingatia ogani na mfumo ulioathirika ambayo ni;
Maambukizi ya mfumo wa hewa – Hutibu magonjwa kama nimonia, bronkaitisi, sinusitisi, tonsilitisi.
Maambukizi ya sikio – Hutibu otitis ya sikio la kati hasa kwa watoto.
Maambukizi ya njia ya mkojo (U.T.I) – huua vimelea kama E. coli na bakteria wengine wanaosababisha UTI
Maambukizi ya mfumo wa chakula – Huua bakteria Helicobacter pylori (anayesababisha vidonda vya tumbo pamoja, hivyo hutumika pamoja na dawa zingine katika matibabu ya vidonda vya tumbo).
Maambukizi ya Ngozi na Tishu laini – hutibu magonjwa kama impetigo, sellulitiz.
Maambukizi ya meno – hutibu magonjwa kama jipu kwenye jino, periodontitisi.
Via vya uzazi – hutumika kwa baadhi ya kesi kutibu magonjwa ya zinaa kutokana na maambukizi ya klamidia na kisonono (gono), kulingana na kiwango cha usugu wa bakteria.
Maudhi madogo ya Amoxicillin
Maudhi madogo au madhara madogo ya kutumia Amoxicillin yanaweza kujumuisha:
Kichefuchefu na kutapika
Kuharisha
Maumivu ya tumbo
Upele au kuwashwa
Maumivu ya kichwa
Maudhi makali Amoxicillin

Matumizi ya amoxicillin yanaweza kuambatana na maudhi makali (madhara) ambayo yatakufanya uhitaji huduma ya haraka. Baadhi ya maudhi yanayotokea sana ni pamoja na;
Mzio Mkali ( mzio wa anafailaksis) – hutokea na dalili ya kuvimba mwili- koo-njia ya hewa, kushindwa kupumua, upele mkali.
Sindromu ya Stevens-Johnson (nadra kutokea lakini ni hatari) – huonekana na mabadiliko makubwa ya ngozi yanayoambatana na malengelenge na kubanduka kwa ngozi.
Kuharisha kwa Sababu ya Clostridium difficile – huweza kusababisha hali kali ya kuharisha kutokana na michomo kwenye utumbo mpaka(kolaitiz).
Uharibifu wa Ini – huonekana na dalili ya manjano ya ngozi na macho, kuongezeka kwa vimeng’enya vya ini kwenye damu.
Kifafa – mara chache, hasa kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo au wanaotumia dozi kubwa.
Usugu wa bakteria kwa Amoxicillin
Amoxicillin inapoteza ufanisi wake kutokana na usugu wa bakteria kwenye dawa, hasa katika vimelea na maambukizi yafuatayo;
Maambukizi ya Mfumo wa Hewa:Â Kutokana na bakteria Streptococcus pneumoniae- anaonyesha kuwa sugu kwenye dawa.
Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI):Â Kutokana na kimelea E. coli- anaonyesha usugu wa 10-50% kulingana na eneo.
Maambukizi ya H. pylori: Usugu ni mkubwa katika nchi nyingi, hivyo huhitajika kutumia dawa za mchanganyiko ili kukabiliana na maambukizi hayo.
Wakati gani umwone Daktari ikiwa unatumia Amoxicillin?
Tafuta msaada wa matibabu wa haraka ikiwa unapata dalili zifuatazo baada ya kutumia amoxicillin;
Mzio mkali – Unaoambatana na kushindwa kupumua, kuvimba kwa uso au midomo.
Hali kali ya kuharisha (Inayoambayana na damu au kuharisha kunakodumu zaidi ya siku 3) – kwa kuwa huwa dalili ya maambukizi makali ya utumbo.
Mabadiliko makubwa ya ngozi – yanayoonekana kama malengelenge, kubanduka kwa ngozi, harara na upele mkali wenye maumivu.
Manjano ya ngozi au macho – huashiria dalili za tatizo kwenye ini.
Kutapika mara kwa mara, kuchanganyikiwa, au kifafa – dalili za sumu mwilini.
Tahadhari na Hali zinazopaswa kuepuka matumizi ya Amoxicillin
Endapo una hali zifuatazo, unapaswa kuepuka kutumia amoxicillin, hali hizo ni;
Mzio wa dawa jamii ya Penicillin – unaweza kusababisha mzio mkali ( mzio wa anafailaksis).
Historia ya mwitikio mkali wa ngozi kwenye dawa mfano umewahi kupatwa na Sindromu ya Stevens-Johnson – epuka amoxicillin.
Magonjwa ya Figo – dozi inapaswa kurekebishwa kulingana na ufanisi wa figo.
Magonjwa ya Ini – dawa inapaswa kutumiwa kwa uangalifu na ufuatiliaji wa ini, ufuatiliaji utafanywa na mtaalamu wa afya.
Mononukleosis kutokana na maambukizi ya kirusi Epstein-Barr Virus - EBV – kuna hatari kubwa ya kupata upele mkali.
Ujauzito na Unyonyeshaji – kwa ujumla ni salama, lakini inapaswa kutumiwa kwa ushauri wa daktari.
Hitimisho
Amoxicillin ni antibiotiki inayotumika sana kwa maambukizi ya bakteria, lakini inapaswa kutumiwa kwa tahadhari kutokana na usugu wa bakteria na hatari ya mzio mkali. Ikiwa unapata madhara yoyote makubwa, wasiliana na daktari mara moja.
Rejea za mada hii
Shulman ST, et al., Infectious Diseases Society of America. Clinical practice guideline for the diagnosis and management of group A streptococcal pharyngitis: 2012 update by the Infectious Diseases Society of America. Clin Infect Dis. 2012 Nov 15;55(10):e86-102.
Matsumoto H, et al. Current and Future Treatment of Helicobacter pylori Infections. Adv Exp Med Biol. 2019;1149:211-225.
Chow AW, et al., Infectious Diseases Society of America. IDSA clinical practice guideline for acute bacterial rhinosinusitis in children and adults. Clin Infect Dis. 2012 Apr;54(8):e72-e112.
Rosenfeld RM, et al. Clinical practice guideline (update): adult sinusitis. Otolaryngol Head Neck Surg. 2015 Apr;152(2 Suppl):S1-S39.
Sartelli M, et al. 2018 WSES/SIS-E consensus conference: recommendations for the management of skin and soft-tissue infections. World J Emerg Surg. 2018;13:58.
Tan CW, Chlebicki MP. Urinary tract infections in adults. Singapore Med J. 2016 Sep;57(9):485-90.
Hendricks KA, et al., Workgroup on Anthrax Clinical Guidelines. Centers for disease control and prevention expert panel meetings on prevention and treatment of anthrax in adults. Emerg Infect Dis. 2014 Feb;20(2).
Chomel B. Lyme disease. Rev Sci Tech. 2015 Aug;34(2):569-76. [PubMed]