Utangulizi

Uchungu wa kujifungua ni mchakato wa misuli ya kizazi kusinyaa na kutanuka ili kumsukuma mtoto na kondo la nyuma nje ya ulimwengu kupitia mlango wa uzazi, kusinyaa na kuachia huko huleta hisia za kukaza (mkazo) na kuachia kwa tumbo la uzazi. Kutambua dalili za uchungu ni muhimu kwa wajawazito ili kuhakikisha wanapata huduma ya matibabu kwa wakati unaofaa na kujifungua salama.
Dalili za uchungu kwa mama mjamzito huwa na jina jingine la dalili za uchungu wa kujifungua au uchungu wa kweli kwa mama mjamzito.
Dalili za uchungu wa kujifungua
Zifuatazo ni dalili za uchungu kwa mama mjamzito;
Hisia za mikazo yenye mpangilio maalumu na yenye maumivu
Mikazo ya mji wa mimba huwa ya mara kwa mara, yenye nguvu na huongezeka jinsi muda unavyokwenda. Wakati mikazo hii inatokea, inakuwa vigumu kwa mama kuzungumza au kutembea kwa kuwa huambatana na maumivu makali ya tumbo la uzazi. Mikazo ya tumbo hutokana na kubana na kuachia kwa misuli ya mfuko wa uzazi
Kutoka kwa ute mzito wenye damu ukeni
Uchafu wa ute mzito uliochanganyika na damu hutoka ukeni, hii humaanisha mlango wa kizazi umeanza kufunguka na kupungua unene.
Kupasuka kwa Chupa ya Maji
Hutokea na ishara ya kutoka kwa maji mengi au matone ya polepole ukeni, hii inaweza kutokea kabla au wakati wa uchungu wa kweli.
Maumivu ya mgongo na hisia za mgandamizo ndani ya nyonga
Maumivu ya chini ya mgongo yanayoendelea yanayoambatana na hisia ya ongezeko la mganamizo mkubwa via ndani ya nyonga. Hii huashiria kuwa mtoto yuko tayari kushuka kuelekea kwenye tundu la uke.
Hisia ya kwenda haja kubwa
Mikazo ya tumbo na via vya uzazi husukuma kinyesi katika utumbo na kumsabaishia mama kupata hisia hii ya kwenda haja kubwa na wakati mwingine kusababisha kutokwa kwa haja kubwa. Mgandamizo pia hupelekea kukojoa mara kwa mara au kupata hisia za kukojoa mara kwa mara.
Wakati wa kuwasiliana na Daktari mjamzito anapopata dalili za uchungu?
Mwone daktari mara moja kwa kufika kituo cha afya kwa uchunguzi na kujifungua salama endapo unapata dalili zifuatazo zinazoashiria uchungu wa kujifungua (uchungu wa kweli);
Mikazo ya mara kwa mara
Ikiwa mikazo inatokea kila dakika 5, inachukua sekunde 60 kila moja na inadumu kwa saa moja mfululizo, unapaswa kwenda hospitalini.
Kupungua kucheza kwa mtoto tumboni
Ikiwa unahisi mtoto hacheki au kucheza kwake kumepungua, tafuta huduma ya matibabu haraka
Kutokwa na damu ukeni
Ikiwa unapata damu nyingi au damu yenye rangi nyekundu kali, wasiliana na daktari mara moja.
Kupasuka kwa chupa ya uzazi
Ikiwa maji yanayotoka yana rangi ya kijani au kahawia, hii huashiria mtoto amejisaidia tumboni na hivyo unahitaji matibabu ya dharura kunusuru uhai wake na hivyo unapaswa kwenda hospitali mara moja.
Hitimisho
Ni muhimu kuhudhuria kliniki kwa uangalizi wa ujauzito wako na kuwasiliana na daktari kuhusu dalili zozote zisizo za kawaida. Kutambua ishara za uchungu na kupata huduma ya matibabu kwa wakati husaidia kuhakikisha unajifungua salama na kupata mtoto mwenye afya njema.
Rejea za mada hii
Preller M, et al. Myosin structure, allostery, and mechano-chemistry. Structure. 2013 Nov 05;21(11):1911-22.
Garfield RE, et al. Physiology and electrical activity of uterine contractions. Semin Cell Dev Biol. 2007 Jun;18(3):289-95.
Ohkubo T, et al. Identification and electrophysiological characteristics of isoforms of T-type calcium channel Ca(v)3.2 expressed in pregnant human uterus. Cell Physiol Biochem. 2005;16(4-6):245-54.
Ravanos K, et al. Factors implicated in the initiation of human parturition in term and preterm labor: a review. Gynecol Endocrinol. 2015;31(9):679-83.
Kao CY, et al. Ionic currents in the uterine smooth muscle. J Physiol. 1975 Mar;246(1):1-36.
Wray S, Burdyga T, et al. Progress in understanding electro-mechanical signalling in the myometrium. Acta Physiol (Oxf). 2015 Feb;213(2):417-31.
Lefebvre DL, et al. Myometrial transcriptional regulation of the gap junction gene, connexin-43. Reprod Fertil Dev. 1995;7(3):603-11.
Adams Waldorf KM, et al. Uterine overdistention induces preterm labor mediated by inflammation: observations in pregnant women and nonhuman primates. Am J Obstet Gynecol. 2015 Dec;213(6):830.e1-830.e19.
Park JS, et al. Role of cytokines in preterm labor and birth. Minerva Ginecol. 2005 Aug;57(4):349-66.
Bakker R, et al. The role of prostaglandins E1 and E2, dinoprostone, and misoprostol in cervical ripening and the induction of labor: a mechanistic approach. Arch Gynecol Obstet. 2017 Aug;296(2):167-179.