Swali la msingi
Doctor samahani mimi mimba ilitoka lakini ajabu damu zinamwagika bila mpangilio, naweza kutumia siku kazaa au zaidi na saa nyingine inakata kabisa kama siku 2 au 3 halafu ikaendelea kutoka, nataka kujua tatizo nini tafadhali? Sasa hii ni mwezi mwengine toka mimba kutoka imerudi shida ile ile kama mwezi ulopita.
Majibu

Pole sana kwa hali unayopitia. Kutokwa na damu bila mpangilio baada ya mimba kuharibika inaweza kuwa dalili ya mambo kadhaa, ambayo baadhi yake vimeelezewa katika makala hii.
Visababishi vya damu kutoka pasipo mpangilio baada ya mimba kutoka
Kusalia kwa tishu za ujauzito kwenye mji wa mimba
Ikiwa mabaki ya kijusi bado yapo kwenye mji wa mimba, yanaweza kusababisha damu kuendelea kutoka mara kwa mara. Mabli na damu, unaweza pia kupata dalili ya maumivu ya tumbo au homa ikiwa kuna maambukizi.
Mabadiliko ya homoni
Baada ya mimba kutoka, mwili unahitaji muda kurejea kwenye hali yake ya kawaida, hivyo ikiwa homoni bado hazijarejea kwenye hali yake ya awali, hali hii inaweza kusababisha damu kutoka kwa vipindi visivyo vya kawaida.
Maambukizi ya ukuta wa dani wa uzazi
Maambukizi kwenye mji wa mimba yanaweza kusababisha damu kutoka bila mpangilio, homa, na maumivu ya tumbo.
Madhaifu ya mji wa mimba
Polipu au uvimbe unaonin'ginia kwenye ukuta wa mji wa mimba unaweza kusababisha damu kutoka mara kwa mara.
Nini cha Kufanya?
Muone daktari haraka kwa uchunguzi wa mji wa mimba kwa kutumia kipimo cha ultrasound ili kuhakikisha hakuna mabaki ya ujauzito kwenye kizazi na kugundua kama kuna uvimbe. Daktari anaweza kukushauri;
Kufanya vipimo vya damu (kama Homoni ya ujauzito na homoni za uzazi) ili kusaidia kutambua kama mwili wako unarudi katika hali ya kawaida.
Kukushauri utumie antibiotiki kama maambukizi yameonekana.
Kusafishwa kizazi kwa upasuaji mdogo ikiwa una mabaki ya ujauzito kwenye mji wa mimba.
Kumbuka
Usiache kumwona daktari mapema kwani kutokwa na damu kwa muda mrefu kunaweza kusababisha upungufu wa damu na matatizo mengine ya afya.
Rejea za madda hii:
American College of Obstetricians and Gynecologists (ACOG). (2021). Early Pregnancy Loss: Miscarriage and Molar Pregnancy. Imechukuliwa 02.04.2025 kutoka www.acog.org.
World Health Organization (WHO). (2018). Management of Post-Miscarriage Complications. Geneva: WHO. Retrieved on April 2, 2025.
Royal College of Obstetricians and Gynaecologists (RCOG). (2016). Recurrent Miscarriage: Causes, Evaluation, and Management. Imechukuliwa 02.04.2025 kutoka www.rcog.org.uk.
Mayo Clinic. (2022). Miscarriage Symptoms and Causes. Retrieved on April 2, 2025, from www.mayoclinic.org.
National Institutes of Health (NIH). (2019). Abnormal Uterine Bleeding after Pregnancy Loss: Causes and Treatments. Imechukuliwa 02.04.2025.