
Vipele na vinundu katika sehemu za siri vinaweza kusababishwa na hali mbalimbali, ikiwemo maambukizi ya bakteria, fangasi, virusi, athari za mzio, au magonjwa sugu ya ngozi kama hidradenitis suppurativa. Dalili hizi zinaweza kuwa kali, kuenea kwa kasi, na hata kusababisha madhara makubwa ikiwa hazitatibiwa kwa wakati.
Kutokana na kuwa na visababishi vya aina mbalimbali, ni muhimu kutambua chanzo cha tatizo kabla ya kuanza matibabu. Matibabu yanaweza kuwa kwa kutumia dawa za kupaka moja kwa moja kwenye tatizo, dawa za kumeza, au hata upasuaji kwa vipele au vinundu vikubwa. Hapa chini kuna orodha ya baadhi ya dawa na matibabu yanayotumiwa kwa ajili ya vipele na vinundu sehemu za siri:
Dawa za kupaka
Zifuatazo ni baadhi ya dawa za kupaka kwa ajili ya kuondoa vipele sehemu za siri;
Krimu za antibiotiki
Hutumiwa kutibu maambukizi ya bakteria kwenye ngozi. Antibiotiki hizi huzuia ukuaji wa bakteria na kusaidia kuzuia ueneaji wa maambukizi. Mfano wa dawa hizi ni:
Mupirocin – Hutumika kutibu maambukizi kwenye vinyweleo kama folikulaitiz na majipu.
Clindamycin Hasa kwa vipele vinavohusiana na chunusi au ugonjwa wa hidradenitis suppurativa.
Tahadhari:Â Epuka kutumia krimu hizi kwa muda mrefu bila ushauri wa daktari ili kuzuia usugu wa bakteria kwenye dawa.
Retinoid ya Kupaka
Hutumiwa kusaidia kuzibua matundu ya ngozi, kupunguza mafuta kupita kiasi, na kuboresha mzunguko wa seli za ngozi. Zinatumika zaidi kwa vipele vinavyotokana na chunusi. Mfano wa retinoid:
Tretinoin – Huboresha usafi wa ngozi na kuzuia kuziba kwa matundu ya ngozi.
Adapalene – Huboresha usafi wa ngozi na kuzuia kuziba kwa matundu ya ngozi, faida yake ni kuwa na madhara machache ya muwasho kuliko tretinoin.
Tahadhari:Â DAwa jamii ya retinoid zinaweza kusababisha ngozi kuwa nyeti kwenye mwanga wa jua, hivyo inashauriwa kutumia krimu za kukinga ngozi dhiti ya mwanga wa jua wakati wa matumizi ili kuepuka kuharibika ngozi.
Kortikosteroid za kupaka
NI jawa jamii ya steroid, hupunguza uvimbe, wekundu, na muwasho unaosababishwa na mzio au hali sugu za ngozi kama izima. Mfano wa Kortikosteroid ni;
Hydrocortisone- Hutumika kwa uvimbe mdogo.
Betamethasone – Hutumika kwa dalili kali zaidi.
Tahadhari:Â Usitumie dawa jamii ya steroid kwa muda mrefu au kwa maambukizi ya bakteria au fangasi bila ushauri wa daktari, kwani zinaweza kuzidisha tatizo.
Dawa za Kumeza
Zifuatazo ni dawa za kumeza kwa ajili ya kuondoa vipele sehemu za siri;
Antibiotiki za kumeza
Zinafaa kwa maambukizi makali au yaliyodumu kwa muda mrefu. Dawa hizi huua bakteria popote walipo mwilini. Baadhi ya dawa hizo ni:
Doxycycline/Minocycline – Hutumika kwa chunusi kali na ugonjwa wa hidradenitis suppurativa.
Amoxicillin-clavulanate – Inafaa kwa majipu au maambukizi ya ngozi yenye usaha.
Cefalexin – Ni dawa mbadala kwa maambukizi ya ngozi.
Tahadhari:Â Ni muhimu kutumia antibiotiki kwa muda uliopendekezwa na daktari ili kuzuia usugu wa bakteria kwa dawa.
Homoni za kumeza (Kwa Wanawake)
Vidonge vya uzazi wa mpango vinaweza kusaidia kwa vipele au vinundu vinavyosababishwa na mabadiliko ya homoni. Mfano wake ni
Ethinyl estradiol + Drospirenone – Ni nzuri kwa chunusi sugu maeneo ya siri zinazohusiana na mabadiliko ya homoni.
Tahadhari:Â Vidonge vya uzazi wa mpango vinaweza kuwa na madhara kama maumivu ya kichwa au mabadiliko ya mzunguko wa hedhi, hivyo ni muhimu kupata ushauri wa daktari kabla ya kutumia.
Isotretinoin (Roaccutane)
Kwa chunusi sugu na vipele ambavyo haviitikii matibabu mengine, isotretinoin inaweza kusaidia kupunguza uzalishaji wa mafuta kwenye ngozi.
Tahadhari:
Dawa hii ina madhara makubwa kama ukavu wa ngozi na midomo, na inaweza kuathiri ini.
Wanawake wanaopanga ujauzito hawapaswi kutumia isotretinoin kwani inaweza kusababisha kasoro kwa mtoto.
Inapaswa kutumika chini ya uangalizi wa daktari.
Matibabu Mengine
Dawa za fangasi
Ikiwa vipele au vinundu vimesababishwa na maambukizi ya fangasi (kama kandidiasis au tinea kruris), dawa za fangasi zinaweza kutumika. Mfano wake ni;
Clotrimazole (ya krimu) – Ni nzuri kwa maambukizi madogo ya fangasi.
Fluconazole (ya kumeza) – NI nzuri kwa maambukizi makali ya fangasi wa sehemu za siri.
Tahadhari:Â Tumia dawa za fangasi kwa muda wote uliopendekezwa hata kama dalili zimepotea mapema, ili kuzuia kurudi kwa maambukizi.
Dawa za virusi- Kwa Maambukizi ya Virusi
Ikiwa vinundu au vipele vimesababishwa na virusi kama herpes simplex, dawa za kupambana na virusi zinaweza kutumika. Mfano wa dawa hizo ni;
Acyclovir/Valacyclovir – Hutumika kudhibiti na kupunguza dalili za vipele vya herpes
Tahadhari:Â Dawa hizi haziwezi kuponya ugonjwa wa herpes, lakini husaidia kupunguza urefu na ukali wa mlipuko wa dalili.
Ukamuaji wa Usaha
Kwa majipu makubwa au vinundu vilivyojaa usaha, daktari anaweza kufanya utaratibu wa kuyatoboa na kutoa usaha ili kupunguza maumivu na kuharakisha uponyaji.
Tahadhari:Â Usijaribu kutoboa jipu au kipele mwenyewe nyumbani, kwani unaweza kusababisha maambukizi makubwa zaidi.
Wakati gani wa kumwona daktari unapokuwa na vipele sehemu za siri?
Ni muhimu kutafuta msaada wa kitabibu haraka ikiwa unakabiliwa na hali na dalili hatari zinazohitaji matibabu ya haraka kama vile;
Kuwa na uvimbe mkubwa unaozidi kuongezeka haraka au unahisi ni mgumu sana.
Kupata maumivu makali ambayo hayapungui hata baada ya kutumia dawa za kupunguza maumivu.
Uwepo wa usaha mwingi, majipu makubwa au vidonda vinavyovuja damu.
Kuwa na dalili za maambukizi makali, kama homa, baridi, uchovu, au mwili kuuma.
Vidonda vinavyochukua muda mrefu kupona au vinaendelea kurudi baada ya matibabu.
Mabadiliko ya ngozi kama wekundu unaozidi kuenea au vidonda vinavyoanza kuwa na harufu mbaya.
Kushuka kwa kinga ya mwili (kwa mfano, ikiwa una kisukari, VVU, au unatumia dawa zinazopunguza kinga ya mwili).
Kuvimba kwa tezi za limfu kwenye kinena au kwapani.
Hitimisho
Matibabu ya vipele na vinundu katika sehemu za siri yanapaswa kufanyika chini ya uangalizi wa mtaalamu wa afya ili kuhakikisha kuwa chanzo cha tatizo kimegunduliwa na kutibiwa ipasavyo. Kujitibu bila ushauri wa daktari kunaweza kuzidisha tatizo au kusababisha madhara makubwa.
Rejea za mada hii
González-López MA. Hidradenitis suppurativa. Med Clin (Barc). 2024 Feb 23;162(4):182-189.
Stancic BH, et al. The Role of Intra-Follicular Shear Forces in Hidradenitis Suppurativa. Skin Pharmacol Physiol. 2023;36(6):302-303.
Mintoff D, et al. Differences in hidradenitis suppurativa patterns of cutaneous involvement between sexes: Insights from a cross-sectional study. Hum Immunol. 2024 Mar;85(2):110764.
Scala E,et al. Hidradenitis Suppurativa: Where We Are and Where We Are Going. Cells. 2021 Aug 15;10(8)
Singh S, Desai K, Gillern S. Management of Pilonidal Disease and Hidradenitis Suppurativa. Surg Clin North Am. 2024 Jun;104(3):503-515.
Seivright J, et al. Pediatric hidradenitis suppurativa: epidemiology, disease presentation, and treatments. J Dermatolog Treat. 2022 Jun;33(4):2391-2393.
Altmeyer P, et al. Pseudocondylomata of the vulva. Geburtshilfe Frauenheilkd. 1981;41(11):783–786. doi: 10.1055/s-2008-1036990.
Anderson SR. Benign vulvovaginal cysts. Diagn Histopathol. 2017;23(1):14–18.
Apostolis CA, et al. Atypical presentation of a vaginal epithelial inclusion cyst. J Minim Invasive Gynecol. 2012;19(5):654–657. doi: 10.1016/j.jmig.2012.03.027.
Bachmann GA, et al. Diagnosis and treatment of atrophic vaginitis. Am Fam Physician. 2000;61(10):3090–3096.
Yan HM, et al. Gut microbiota alterations in moderate to severe acne vulgaris patients. J Dermatol. 2018 Oct;45(10):1166-1171.
Juhl CR, et al. Dairy Intake and Acne Vulgaris: A Systematic Review and Meta-Analysis of 78,529 Children, Adolescents, and Young Adults. Nutrients. 2018 Aug 09;10(8)