
Kuwashwa pekee sio dalili ya moja kwa moja ya kuwa una maambukizi ya virusi vya UKIMWI (VVU), lakini VVU vinaweza kusababisha kuwashwa katika hali fulani kutokana na athari zake kwenye mfumo wa kinga. Kwa kawaida watu waishio na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI hupata harara, na magonjwa ya ngozi yanayopelekea kuwashwa mwili. Makala hii imeorodhesha baadhi ya visababishi vikuu vya kuwashwa mwili kwa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU.
Magonjwa ya ngozi yanayohusiana na VVU
VVU hudhoofisha kinga ya mwili, na kufanya mtu awe katika hatari ya magonjwa ya ngozi kama:
Upele wa VVU – Upele mwekundu, unaowasha, unaoweza kuenea mwilini, mara nyingi huonekana wiki chache baada ya maambukizi.
Seborrheic dermatitis – Husababisha ngozi kuwa na magamba na kuwasha, hasa kwenye uso na kichwa.
Soriasis – Ugonjwa unaweza kuwa mkali zaidi kwa watu waishio na maambukizi ya VVU, na kusababisha vipele vyenye magamba yenye kuwasha.
Magonjwa nyemelezi
Watu wenye VVU wako katika hatari kubwa ya kupata maambukizi yanayosababisha kuwashwa, kutokanana mwili kuvamiwa na vimelea nyemelezi wakati kinga ya mwili ipo chini, baadhi ya magonjwa hayo ni kama;
Maambukizi ya fangasi (mfano, kandidiasis, fangasi wa ngozi).
Maambukizi ya bakteria (mfano, folikulaitiz).
Skabiz au homa ya chawa, huwa kali zaidi kwa watu wenye kinga dhaifu.
Maudhi ya dawa za VVU
Baadhi ya dawa za kupunguza makali ya VVU zinaweza kusababisha muwasho kama athari ya mzio au madhara ya dawa. Mfano wa dawa hizo ni;
Nevirapine (NVP) – Inajulikana kusababisha upele unaowasha kwa baadhi ya wagonjwa.
Abacavir (ABC) – Inaweza kusababisha athari ya mzio inayoambatana na kuwashwa.
Efavirenz (EFV) – Baadhi ya watu hupata upele na kuwashwa kama athari ya dawa.
Lini Unapaswa Kumwona Daktari unapohisi unawashwa kutokana na UKIMWI?
Unapaswa kuonana na daktari au kupima VVU ikiwa una:
Upele usioeleweka au kuwashwa kwa muda mrefu.
Dalili zingine za VVU, kama homa, kuvimba tezi limfu, jasho la usiku, kupungua uzito, au uchovu mkali.
Historia ya kujihusisha na ngono isiyo salama au matumizi ya sindano za pamoja za madawa ya kulevya.
Hitimisho
Kuwashwa pekee sio dalili ya moja kwa moja ya VVU, lakini ikiwa kuna dalili nyingine au hatari za maambukizi, inashauriwa kupima VVU. Ikiwa una wasiwasi, tafuta msaada wa daktari kwa ushauri na uchunguzi wa kina.
Rejea za mada hii
Roland M. Itchy skin in HIV. Newsline People AIDS Coalit N Y. 1998 Mar:21-5. PMID: 11367452.
Gelfand JM, Rudikoff D. Evaluation and treatment of itching in HIV-infected patients. Mt Sinai J Med. 2001 Sep-Oct;68(4-5):298-308. PMID: 11514917.
Singh F, Rudikoff D. HIV-associated pruritus: etiology and management. Am J Clin Dermatol. 2003;4(3):177-88. doi: 10.2165/00128071-200304030-00004. PMID: 12627993.
Tschachler E, Bergstresser PR, Stingl G. HIV-related skin diseases. Lancet. 1996; 348(9028):659-663.
Lemos BD, et al. Pathologic nodal evaluation improves prognostic accuracy in Merkel cell carcinoma: analysis of 5823 cases as the basis of the first consensus staging system. Am Acad Dermatol. 2010;63(5):751-761.
Coopman SA, et al. Cutaneous disease and drug reactions in HIV infection. N Engl J Med. 1993;328(23): 1670-1674.
Kaushik SB, et al. Chronic pruritus in HIV-positive patients in the southeastern United States: its prevalence and effect on quality of life. J Am Acad Dermatol. 2014;70(4):659-664.7.
Davidovici BB, et al. Psoriasis and systemic inflammatory diseases: potential mechanistic links between skin disease and co-morbid conditions. J Invest Dermatol. 2010;130(7):1785-1796.
8.Morar N, et al. HIV-associated psoriasis: pathogenesis, clinical features, and management. Lancet Infect Dis. 2010;10(7): 470-478.
Cedeno-Laurent F, et al. New insights into HIV-1-primary skin disorders. JIntAIDS Soc. 2011. ;14:5.