Wanawake wengi wamekuwa wakijiuliza kuhusu maswali mbalimba yanayohusu matumizi ya p2 kabla ngono, maaswali hayo ambayo yamejibiwa na makala hii ni;
Jana nilimeza p2 leo nikakutana na mwanaume je naweza kupata mimba
Juzi nilimeza p2 leo nikakutana na mwanaume je naweza kupata mimba
Je P2 inazuia mimba ikitumika kabla ya kushiriki ngono bila kinga?
Maelezo ya kina

Kabla ya kujibu maswali haya mwishoni mwa makala hii, ni vema kufahamu namna P2 inavyofanya kazi ili kujua kama itazuai au la;
P2 (Postinor-2) ni dawa ya dharura ya kuzuia mimba ambayo imetengenezwa awali kutumiwa baada ya kufanya ngono bila kinga, na ufanisi wake ni asilimia 87, yaani kati ya wanawake 100 wanaotumia P2, ni wanawake 87 tu hawatapata mimba, wengine waliosalia watashika mimba. Dawa hii hufanya kazi kwa:
Kuchelewesha au kuzuia uovuleshaji
Kufanya ute wa mlango wa kizazi kuwa mzito – Hii inazuia mbegu za kiume kufikia yai.
Kubadilisha ukuta wa mji wa mimba – Hii inaweza kufanya uwezekano wa yai lililochavushwa kushindwa kujipandikiza na hivyo uwezekano wa kupata mimba hupungua, lakini si njia yake kuu ya kufanya kazi.
Njia sahihi ya kutumia P2:
P2 inapaswa kutumiwa ndani ya saa 72 (siku 3) ndani ya siku 3 baada ya kushiriki ngono bila kinga, kadri unavyoitumia mapema, ndivyo inavyofanya kazi kwa ufanisi. Hata hivyo tafiti zinaonyesha kuwa ufanisi ni mkubwa zaidi ikiwa inatumika ndani ya saa 24 baada ya ngono.
Njia zingine bora za kuzuia mimba kwa uhakika:
Njia zingine nzuri kama kondomu, vidonge vya majira, sindano za uzazi wa mpango, kitanzi (IUD), au vipandikizi badala ya kutegemea P2 mara kwa mara. P2 inapaswa kutumiwa tu kama mbinu ya dharura.
Majibu ya maswali
Hali ya Kwanza:
Mtu ambaye amefanya ngono kwenye siku ya uovuleshaji, kisha akatumia P2 siku inayofuata.
Tatizo: Ikiwa tayari uovuleshaji umetokea, P2 haina uwezo wa kuzuia mbegu kurutubisha yai.
Kwa nini? P2 hufanya kazi kwa kuchelewesha au kuzuia uovuleshaji. Ikiwa yai tayari limeachiwa kutoka kwenye ovari, mbegu zinaweza kulifikia na kurutubisha kabla ya dawa kufanya kazi.
Hatari ya mimba: Kubwa zaidi, kwa sababu dawa haitaweza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa baada ya ovulation.
Hali ya Pili
Mtu ambaye alimeza P2 kabla ya kufanya ngono ili kuzuia uovuleshaji, kisha akafanya ngono siku inayofuata.
Faida: Ikiwa P2 imefanikiwa kuchelewesha uovuleshaji, basi hakuna yai lililo tayari kurutubishwa na mbegu.
Kwa nini? P2 huzuia uovuleshaji kwa muda mfupi, na hivyo inafanya kazi kama kinga ya muda mfupi ikiwa imetumika kabla ya ovulation kutokea.
Hatari ya mimba: Chini zaidi, kwani hakuna yai lililotolewa kwa ajili ya kurutubishwa.
Nani Analindwa zaidi dhidi ya mimba?
Mtu aliyemeza P2 kabla ya ngono ana kinga zaidi kuliko aliyemeza baada ya ngono kwenye siku ya uovuleshaji. Hii ni kwa sababu dawa hiyo inafanya kazi kwa kuchelewesha au kuzuia uovuleshaji, lakini haiwezi kuzuia yai lililo tayari kurutubishwa.
Hitimisho Muhimu
P2 hufanya kazi vizuri zaidi ikiwa itatumika kabla ya uovuleshaji kutokea.
Ikiwa uovuleshajii tayari umetokea, ufanisi wake hupungua sana, na mimba inaweza kutokea.
Kwa uhakika wa kuzuia mimba, ni bora kutumia njia za muda mrefu kama vidonge vya uzazi wa mpango vya kila siku, sindano, au vijiti.
Rejea za mada hii
Levonorgestrel – StatPearls – NCBI Bookshelf.https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK539737/. Imechukuliwa 11.07.2023
Oral Contraceptive Pills – StatPearls – NCBI Bookshelf.https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK430882/. Imechukuliwa 11.07.2023
Overview of Contraception - Women's Health Issues - MSD Manuals.https://www.msdmanuals.com/home/women-s-health-issues/family-planning/hormonal-methods-of-contraception. Imechukuliwa 11.07.2023
STANDARD TREATMENT GUIDELINES AND NATIONAL ESSENTIAL MEDICINES LIST FOR TANZANIA MAINLAND. Sixth edition 2021. Pg 241-242.