Kukamua maziwa ni mbinu inayomsaidia mama kuhakikisha mtoto anapata maziwa yake muda wowote hat kama anakosekana kwa muda. Hii ni muhimu sana hasa kwa akina mama wanaokwenda kazini au wenye changamoto za kunyonyesha moja kwa moja.
Njia za kukamua maziwa
Mama anaweza kukamua maziwa kwa kutumia mikono yake au vifaa maalumu vya kukamulia maziwa.
Kukamua kwa mikono

Kukamua maziwa kwa mikono ni njia rahisi na inaweza kufanyika wakati wowote, zifuatazo ni hatua za kufuata wakati wa kukamua maziwa kwa mkono
Kujiandaa
Kaa sehemu yenye utulivu na ruhusu akili yako kuwa katika hali ya faraja.
Osha mikono kwa sabuni na maji safi.
Andaa chombo safi cha kuhifadhi maziwa, kama vile chupa ya glasi au plastiki isiyo na kemikali hatarishi kama vile BPA.
Kusisimua mtiririko wa maziwa
Loweka kitambaa kwenye maji ya moto kiasi/uvuguvugu kikamue kisha funika matiti au kanda matiti kwa kutumia ncha za vidole taratibu kwa dakika kadhaa
Vuta hisia za kumnyonyesha mtoto wako au angalia picha yake, hii ihusaidia homoni ya oxytocin ambayo huchochea utolewaji wa maziwa.
Kukamua Maziwa
Weka kidole gumba juu ya eneo jeusi la mviringo wa chuchu na vidole vingine chini yake, ukifanya umbo la "C".
Bonyeza taratibu kuelekea ndani, kisha vuta vidole kuelekea mbele ya chuchu kwa mwendo wa taratibu.
Rudia hatua hii kwa mwendo wa kawaida, ukiepuka kubana au kukwaruza ngozi.
Endelea kwa dakika kadhaa hadi mtiririko wa maziwa upungue, kisha rudia hatua hizo kwa titi lingine.
Kuhifadhi maziwa
hifadhi maziwa katika chombo safi na salama katika joto la kawaida, kwenye jokofu au jokofu la kugandisha kulingana na muda wa matumizi
Kukamua maziwa kwa kifaa maalumu cha kukamulia maziwa (pampu ya maziwa)

Kutumia pampu ya kukamua maziwa ni njia inayotumia muda mfupi na yenye ufanisi mkubwa katika kutoa maziwa mengi ukilinganisha na kukamua kwa mkono.
Kuna aina mbili kuu za pampu, pampu za umeme na pampu za mkono.
zifuatazo ni hatua za kufuata wakati wa kukamua maziwa kwa kutumia pampu.
Kujiandaa
Kaa sehemu yenye utulivu na ruhusu akili yako kuwa katika hali ya faraja.
Osha mikono kwa sabuni na maji safi.
Andaa chombo safi cha kuhifadhi maziwa, kama vile chupa ya glasi au plastiki isiyo na kemikali hatarishi kama vile BPA.
Kusisimua mtiririko wa maziwa
Loweka kitambaa kwenye maji ya moto kiasi/uvuguvugu kikamue kisha funika matiti au kanda matiti kwa kutumia ncha za vidole taratibu kwa dakika kadhaa
Vuta hisia za kumnyonyesha mtoto wako au angalia picha yake, hii ihusaidia homoni ya oxytocin ambayo huchochea utolewaji wa maziwa.
Kukamua maziwa
Namna ya kukamua maziwa kulingana na aina ya kifaa unachotumia
Kukamua maziwa kwa pampu ya mkono
Weka kifuniko cha pampu juu ya chuchu yako kwa usahihi ili kuhakikisha kuwa imeshikika vizuri bila kuvuja hewa.
Bonyeza pampu kwa mwendo wa taratibu na wa kawaida ili kuvuta maziwa kutoka kwenye matiti.
Endelea kukamua kwa mwendo wa taratibu kwa dakika kadhaa hadi mtiririko wa maziwa upungue.
Badili upande mwingine na rudia mchakato huo.
Kukamua maziwa kwa pampu ya umeme
Weka kifuniko cha pampu juu ya chuchu kwa usahihi.
Washa pampu kwa kiwango cha chini kisha ongeza kasi polepole kadri utakavyoona inafaa.
Ruhusu pampu ifanye kazi kwa muda wa dakika 10-15 kwa kila ziwa au hadi maziwa yatakapopungua.
Badili upande na rudia mchakato huo.
Kuhifadhi maziwa
hifadhi maziwa katika chombo safi na salama katika joto la kawaida, kwenye jokofu au jokofu la kugandisha kulingana na muda wa matumizi
Mambo ya kuzingatia wakati wa kukamua maziwa
Zingatia usafi wa mwili wako , vyombo vinavyotumika kukamua na kuhifadhi maziwa
Kula chakula chenye mlo kamili zaidi ya milo mitatu kwa siku
Pata muda wa kutosha kupumzika na epuka msongo wa mawazo
Nyonyesha mtoto mara kwa mara unapokuwepo, na ukamue mara kwa mara kuongeza uzalishaji wa maziwa
Usibonyeze matiti kwa nguvu kuepuka maumivu au majeraha.Kama maziwa hayatoki vizuri, jaribu kupumzika na kusisimua chuchu kabla ya kujaribu tena.
Anza kukamua wiki kadhaa kabla ya kurejea kazini ili kumzoesha mtoto na kuufanya mwili kuzalisha maziwa ya kutosha.
Rejea za mada hii
Hand Expression|Infant and Child Feeding in Emergencies. CDC. https://www.cdc.gov/infant-feeding-emergencies-toolkit/php/hand-expression.html. Imechukuliwa 28.03.2025
Pumping Breast Milk | Infant and Toddler Nutrition. CDC. https://www.cdc.gov/infant-toddler-nutrition/breastfeeding/pumping-breast-milk.html. Imechukuliwa 28.03.2025
Patient education: Pumping breast milk (Beyond the Basics). UpToDate.https://www.uptodate.com/contents/pumping-breast-milk-beyond-the-basics/print. Imechukuliwa 28.03.2025