Utangulizi

Vidonge vya kuzuia mimba vya mchanganyiko (Combined Oral Contraceptives - COCs) ni mojawapo ya njia za kuzuia mimba inayotumiwa na wanawake wengi duniani. Vidonge hivi vina homoni mbili yaani estrojeni na projesteroni, ambazo hufanya kazi kwa pamoja kuzuia ujauzito.
Vidonge hivi vinaweza kutumiwa kwa njia tofauti kulingana na aina yake na mahitaji ya mtumiaji. Ni muhimu kuelewa jinsi vinavyofanya kazi, jinsi ya kuvitumia, faida zake, madhara yanayoweza kutokea, na wakati wa kumuona daktari.
Jinsi vidonge vya kuzuia mimba vinavyofanya kazi
Vidonge vya kuzuia mimba vya mchanganyiko hufanya kazi kwa njia kuu tatu:
Kuzuia uzalishaji wa yai (uovuleshaji) – Homoni za vidonge hivi huzuia ovari kutoa yai, hivyo hakuna yai litakalokutana na mbegu ya kiume ili kutunga mimba.
Kufanya ute wa mlango wa kizazi kuwa mzito – Hii huzuia mbegu za kiume kuingia kwenye mfuko wa uzazi kwa urahisi.
Kufanya ukuta wa ndani ya mfuko wa uzazi kuwa mwembamba – Hata kama yai litatungwa, haliwezi kujishikiza kwenye ukuta wa mfuko wa uzazi kwa sababu ni mwembamba na hauwezi kuhimili mimba.
Aina za vidonge vya kuzuia mimba vya mchanganyiko
Aina ya vidonge hutegemea idadi ya siku vinavyotumika, aina hiyo ni kama ifuatavyo:
Vidonge vya siku 21 – Unakunywa kidonge kimoja kila siku kwa siku 21, kisha unafanya mapumziko ya siku 7 bila kutumia vidonge vyovyote. Katika kipindi hiki, utapata hedhi.
Vidonge vya siku 28 – Unakunywa kidonge kimoja kila siku kwa siku 28 bila mapumziko. Vidonge 21 vina vichocheo, huku vidonge 7 vya mwisho vikiwa vichocheo bandia. Hedhi hutokea wakati wa kutumia vidonge visivyo na vichocheo.
Vidonge vya mzunguko mrefu – Hivi hutumiwa kwa miezi mitatu mfululizo kabla ya kufanya mapumziko ya wiki moja, hivyo kupunguza idadi ya hedhi kwa mwaka.
Jinsi ya kutumia vidonge vya kuzuia mimba
Anza kutumia kidonge siku ya kwanza ya hedhi yako
Hii hutoa kinga mara moja. Unaweza pia kuanza siku yoyote ya mzunguko wako, lakini utahitaji kutumia njia nyingine ya dharura (kama kondomu) kwa siku 7 za mwanzo.
Kunywa kidonge kila siku kwa wakati uleule
Hii inahakikisha kiwango cha homoni mwilini hakipungui na kinabaki thabiti kwa ufanisi wa juu.
Mambo ya kuzungatia wakati unatumia vidonge vya majira
Ikiwa umesahau dozi moja ya majira ufanyaje?
Meza kidonge mara tu unapokumbuka, hata kama inamaanisha kunywa vidonge viwili kwa siku moja.
Ikiwa umesahau vidonge viwili au Zaidi vya majira ufanyaje?
Tumia njia nyingine ya kuzuia mimba kama kondomu kwa siku 7 mfululizo na endelea na dozi yako kama kawaida.
Usitumie dawa zinazoingiliana na vidonge vya kuzuia mimba
Baadhi ya dawa kama rifampicin, dawa za kifafa, na baadhi ya dawa za mitishamba kama St. John’s Wort zinaweza kupunguza ufanisi wa vidonge.
Faida za vidonge vya kuzuia mimba
Hutoa kinga madhubuti ya kupata mimba ikiwa vinatumika kwa usahihi huku ikiwa na ufanisi wa asilimia 99.
Husaidia kupunguza maumivu makali ya hedhi na kurekebisha mzunguko wa hedhi.
Hupunguza hatari ya saratani ya ovari na mfuko wa mimba.
Hupunguza chunusi na mafuta kwenye ngozi.
Husaidia kudhibiti dalili za tatizo la ovari kuwa na vifuko vingi vya maji
Maudhi yanayoweza Kutokea
Baadhi ya wanawake wanaweza kupata maudhi madogo wanapoanza kutumia vidonge, ikiwa ni pamoja na:
Kichefuchefu
Maumivu ya kichwa
Kuongezeka uzito kidogo
Kutokwa na damu kidogo katikati ya mzunguko wa hedhi
Mabadiliko ya hisia au msongo wa mawazo
Madhara haya mara nyingi hupungua baada ya miezi michache ya matumizi endelevu.
NB: Kuhusu madhara makubwa ya matumizi ya vidonge vya majira nenda katika makala ya madhara ya kutumia vidonge vya majira.
Wakati wa kumwona daktari
Ni muhimu kumuona daktari ikiwa unapata dalili zifuatazo:
Maumivu makali ya kichwa yanayoendelea
Maumivu ya kifua au upungufu wa pumzi
Kuvimba kwa miguu au maumivu makali ya mguu mmoja
Kupata hedhi nzito isiyo ya kawaida
Kushuka kwa hamu ya tendo la ndoa kwa muda mrefu
Je, vidonge vya kuzuia mimba vinazuia magonjwa ya zinaa?
Hapana. Vidonge vya kuzuia mimba havimlindi mwanamke dhidi ya magonjwa ya zinaa kama vile UKIMWI, kisonono, kaswende, na klamidia. Kwa hiyo, inashauriwa kutumia kondomu kwa ulinzi wa ziada dhidi ya magonjwa ya zinaa.
Hitimisho
Vidonge vya kuzuia mimba vya mchanganyiko ni njia mojawapo ya kuzuia mimba ikiwa itatumika kwa usahihi. Ni muhimu kufuata maelekezo ya daktari na kuhakikisha unakunywa vidonge vyako kila siku wakati mmoja ili kuepuka kupungua kwa kiwango cha ufanisi.
Wapi utapata maelezo zaidi?
Ikiwa una maswali yoyote kuhusu vidonge hivi, ni vyema kushauriana na daktari wako.
Rejea za mada hii:
NCBI. Contraceptive Benefits and Risks.https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK235069/#. Imechukuliwa 08.03.20025
NCBI. Oral Contraceptive Pills.https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK430882/. Imechukuliwa 08.03.20025
Estrogen and progestin oral contraceptives (oral route). https://www.mayoclinic.org/drugs-supplements/estrogen-and-progestin-oral-contraceptives-oral-route/description/drg-20069422. Imechukuliwa 08.03.20025
MSD manual. Oral Contraceptives.https://www.msdmanuals.com/professional/gynecology-and-obstetrics/family-planning/oral-contraceptives. Imechukuliwa 08.03.20025