Kipimo cha UKIMWI (VVU) kuwa negative maana yake ni kwamba hakuna virusi vya UKIMWI vilivyogunduliwa kwenye damu yako wakati wa kipimo. Hii ni habari njema, lakini kuna mambo machache muhimu ya kuzingatia kuwa unaweza kuwa kweli huna VVU au bado kwenye dirisha la matazamio ambalo ni muda baada ya maambukizi ambapo virusi vinaweza kuwa mwilini lakini havionekani bado kwenye kipimo. Kwa kawaida ni kati ya wiki 2 hadi 12, lakini kwa baadhi ya vipimo vinaweza kuchukua hadi siku 90 (takribani miezi 3).
Nini cha kufanya baada ya matokeo ya kipimo cha UKIMWI kuwa negative?

Kupokea majibu ya kuwa negative kwa kipimo cha UKIMWI ni hatua muhimu kuelekea kujua hali yako ya kiafya. Hata hivyo, kuna hatua kadhaa unazopaswa kuchukua ili kujilinda na kuhakikisha unaendelea kuwa salama.
1. Hakikisha Kipindi cha dirisha Kimepita
Kama ulifanya ngono isiyo salama au tukio lingine la hatari ndani ya wiki 2–12 zilizopita, kuna uwezekano kwamba kipimo hakijaweza kugundua virusi bado. Rudia kipimo baada ya siku 90 kutoka tukio hilo ili kupata matokeo ya uhakika.
2. Endelea Kujilinda
Tumia kondomu kila mara unapofanya ngono na mpenzi usiyejua hali yake ya kiafya.
Epuka kushiriki vifaa vinavyoweza kuchafuka na damu kama vile sindano.
Kama mwenzi wako ana VVU na anatumia dawa kwa ufanisi, bado ni vyema kuzingatia ushauri wa daktari.
3. Fikiria Upimaji wa Mara kwa Mara
Ikiwa uko kwenye mahusiano ya wapenzi wengi au mazingira ya hatari, pima afya yako mara kwa mara (angalau kila baada ya miezi 3–6). Pamoja na UKIMWI, chunguza pia magonjwa mengine ya zinaa kama kaswende, kisonono, na klamidia.
4. Ongea na Daktari
Kama una hofu, wasiwasi, au maswali kuhusu kinga, uhusiano, au afya ya uzazi, muone mtaalamu wa afya kwani anaweza pia kukupa ushauri kuhusu matumizi ya PrEP (dawa za kuzuia maambukizi kwa watu ambao hawajaambukizwa lakini wako kwenye hatari).
Kumbuka
Matokeo negative hayamaanishi huna hatari tena. Ni nafasi ya kufanya maamuzi bora ya kiafya kwa maisha yako ya sasa na ya baadaye.
Rejea za mada hii:
World Health Organization. HIV testing services: policy, principles and practices. Geneva: WHO; 2021. Available from: https://www.who.int/publications/i/item/9789240023581. Imechukuliwa 12.04.2025
Centers for Disease Control and Prevention. HIV Testing Overview. CDC; 2022. Available from: https://www.cdc.gov/hiv/basics/testing.html. Imechukuliwa 12.04.2025
UNAIDS. Global HIV & AIDS statistics – Fact sheet. UNAIDS; 2023. Available from: https://www.unaids.org/en/resources/fact-sheet. Imechukuliwa 12.04.2025