Swali: Mimi na mke wangu tunajitibu kisonono ila kinajirudia, tufanyaje?
Kumbuka: Neno Gono pia limetumika kama jina mbadala la Kisonono katika makala hii.
Jibu
Kisonono ni moja ya ugonjwa wa zinaa unaosabaishwa na bakteria anayefahamika kama Neisseria gonorrhoeae. Kimelea huyu hukwea kwenye via vya uzazi ikiwa pomoja na uke na mrija wa mkojo kabla ya kusababisha maambukizi. Baadhi ya watu huonyesha dalili za ugonjwa na wengine huwa hawaonyeshi kabisa. Dalili zinazoonekana mara nyingi hufanana na dalili za maambukizi kwenye mfumo wa mkojo, hata hivyo pia hupelekea kutokwa na usaha sehemu za siri haswa kwa wanaume.
Kwa ujumla sababu kuu inayopelekea gono ya kujirudia ni kutokana na usugu aliojitengenezea kimelea huyu kwenye dawa. Baadhi ya tafiti za maabara zinaonyesha kuwa bakteria N. gonorrhoeae amejenga usugu wa asilimia 100 to kenye dawa tetracycline na penicillin na wa asilimia 80% kwenye dawa zaidi ya moja. Usugu huu unaweza kusababishwa na matumizi holela ya dawa pasipo vipimo au uchunguzi wa daktari.
Kisonono cha kujirudia
Kisonono kinaweza kujirudia ndani ya siku 4 hadi 8 baada ya kupata matibabu endapo mtu atapata maambukizi mapya baada ya kutumia dawa.
Hata hivyo kuna sababu zingine zinazoweza kusababisha kujirudia kwa kisonono ikiwa pamoja na;
Vimelea kutengeneza usugu kwenye dawa
Kupata maambukizi ya kimelea wasiosikia dawa
Kutumia dozi isiyo sahihi au kutomaliza dozi
Kutumia dawa isiyo sahihi
Kuwa na magonjwa mengine ya zinaa yasiyohusiana na kisonono
Endapo una sababu kati ya zilizotajwa hapo unapaswa kuwasiliana na daktari wako mara moja kwa uchunguzi na tiba.
Mambo ya kufanya endapo gono inajirudia
Jambo muhimu la kufanya ili kutibu gono ya kujirudia rudia ni kuwasiliana na daktari wako kwa uchunguzi na tiba. Pia unapaswa kuzingatia njia ulizofundishwa ili kujikinga kupata maambukizi mapya kama vile kutumia kondomu na kuwa na mpenzi asiye na maambukiziya gono au magonjwa ya zinaa.
Ni nini daktari atafanya kutibu gono ya kujirudia?
Endapo umetibiwa kisonono na mara baada ya kupona dalili zikajirudia, daktari atakuuliza maswali mbalimbali kuhusu ushauri aliokupa awali wakati anakuandikia dozi ya dawa ili kuona kama ulitumia dawa ipasavyo wewe na mpenzi wako kisha kukufanyia uchunguzi wa mwili na vipimo.
Vipimo gani hufanyika kwa gono ya kujirudia rudia?
Mara nyingi endapo gono inajirudia, ni muhimu kufanya kipimo cha culture and sensitivity ya ute ute kutoka kwenye uume au ukeni. Kipimo cha culture and sensitivity hulenga kuotesha vimelea walio kwenye majimaji haya ya sehemu za siri na kuangalia ni dawa gani ina ufanisi dhidi ya vimelea hao.
Vipimo vingine vinaweza kufanyika pia kutegemea hali ya mgonjwa na ni nini daktari anafikiria kuwa kisababishi cha kujirudia kwa kisonono.
Matibabu ya gono ya kujirudia
Baada ya kipimo hiki na vingine, utapatiwa matibabu yanayoendana na hali yako pamoja na dawa ambazo zina ufanisi wa kutibu ugonjwa wako wewe na mpenzi wako( wote unaoshiriki nao ngono). Utapatiwa ushauri pia wa kuwa na mpenzi mmoja asiye na maambukizi au kutumia kondomu kwa kila tendo.
Rejea za Mada hii;
Glozman VN, Borisenko KK. Retsidivy gonorei u muzhchin (osobennosti techeniia i lecheniia) [Recurrences of gonorrhea in men (the characteristics of the course and treatment)]. Vestn Dermatol Venerol. 1990;(3):51-3. Russian. PMID: 2195797.
Bautista CT, Wurapa EK, Sateren WB, Morris SM, Hollingsworth BP, Sanchez JL. Repeat infection with Neisseria gonorrhoeae among active duty U.S. Army personnel: a population-based case-series study. Int J STD AIDS. 2017;28(10):962-968. doi:10.1177/0956462416681940
Fung M, Scott KC, Kent CK, et al. Chlamydial and gonococcal reinfection among men: a systematic review of data to evaluate the need for retesting. Sex Transm Infect 2007; 83: 304–309.
CDC. Updated to CDC’s sexually transmitted diseases treatment guidelines, 2010: oral cephalosporins no longer a recommended treatment for gonococcal infections. MMWR 2012; 61: 590–594.
Ng LK, Martin IE. The laboratory diagnosis of Neisseria gonorrhoeae. Can J Infect Dis Med Microbiol. 2005;16(1):15-25. doi:10.1155/2005/323082
Bignell C, Ison CA, Jungmann E. Gonorrhoea. Sex Transm Infect. 2006;82 Suppl 4(Suppl 4):iv6-iv9. doi:10.1136/sti.2006.023036
Yeshanew, A.G., Geremew, R.A. Neisseria Gonorrhoae and their antimicrobial susceptibility patterns among symptomatic patients from Gondar town, north West Ethiopia. Antimicrob Resist Infect Control7, 85 (2018). https://doi.org/10.1186/s13756-018-0376-3