Kiunga mwana ni nini?
Katika Makala hii, neno kiunga mwana limetumika kumaanisha kiunganishi kati ya kondo la mama na mtoto. Kiunga mwana kimetumika pia kumanisha kipande cha kiunga mwana kilichobaki baada ya kutenga mtoto na kondo la nyuma. Baadhi ya watu huita kiunga mwana kama ‘kitovu cha mtoto’ lakini lugha sahihi ni kiunga mwana na kitovu kina maana ya shina linalobakia tumboni baada ya kunyauka kwa kipande cha kiungamwana.
Wakati gani kiunga mwana hudondola?
Kiunga mwana hudondoka wiki 1 hadi 2 baada ya mtoto kuzaliwa.
Nifanye nini ili kuharakisha kudondoka haraka kwa kiunga mwana?
Kiunga mwana kilichokauka hudondoka haraka zaidi ya kile kilicho kibichi, hivyo ili ni vema kuhakikisha hakipati maji wala uchafu ili kuzuia maambukizi yanayoweza kusababisha kisianguke haraka. Wakati wa kumsafisha mtoto, tumia kitambaa ili badala ya kummwagia maji mwili mzima. Mambo ya kuzingatia ili kutunza kiunga mwana Endapo mtoto anavaa pampasi, hakikisha unaifunga chini ya kitovu kiasi cha kutogusa kiunga mwana au unaweza kukata sehemu ya katikati ili kuacha huru kiungamwana dhidi ya mkojo au kinyesi cha mtoto kinachoweza kupelekea maambukizi na kuchelewa kuanguka. Endapo unataka kutumia maji badala ya kitambaa kumwogesha mtoto, hakikisha anakuwa kwenye pozi ambalo maji hayatagusa kiunga mwana mpaka pale kitakapoanguka.
Kama kuna maji yamegusa kiunga mwana na yakaushe kwa kitambaa kisafi kilichochovywa kwenye maji ya uvuguvugu na kukamuliwa, fanya hivi kwa taratibu ili kuepuka kung’oa au kukata kiunga mwana
Mabadiliko ya kiunga mwana kabla ya kuanguka
Baada tu ya kuzaliwa, kiunga mwana huwa na rangi nyeupe ya kung’aa na hukauka na kupata rangi ya kijivu, kahawia au nyeusi jinsi mtoto anavyoongeza siku. Mabadiliko haya ni ya kawaida na hivyo haupaswi kupata hofu kama kiunga mwana ni kisafi na kikavu. Baada ya kuanguka kwa kiunga mwana nini kinafuata?
Baada ya kiunga mwana kuanguka, tegemea kuona wekundu kwenye kitovu sehemu ambapo kiunga mwaa kilikuwa kimejishikiza pamoja na majimaji au damu kidogo sana inayotoka na kukatika katika muda usiozidi wiki mbili. Wakati gani utafute msaada wa daktari haraka?
Wasiliana na daktari endapo;
Kiunga mwana hakijaanguka wiki mbili baada ya kuzaliwa
Kiunga mwana kutoa majimaji yasiyo ya kawaida au yanayonuka
Ngozi ya shina la kitovu kuwa nyekundu na yenye maumivu ikiguswa.
Kulia kwa mtoto unapogusa kitovu au kiunga mwana
Mtoto anapata homa
Kidonda ni chekundu wiki mbili baada ya kudondoka kwa kiunga mwana
Via ndani ya tumbo vinachomoza kupitia kitovu
Majina mengine ya kiunga mwana ni yapi?
Baadhi ya watu hufahamu kiunga mwana kuwa ni;
Kitovu cha mtoto
Umbilical cord
Rejea za mada hii
Patricia S. Coffey, et al. Umbilical cord-care practices in low- and middle-income countries: a systematic review. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC5319165/. Imechukuliwa 16.07.2021
María Dolores López-Medina, et al. Umbilical cord separation time, predictors and healing complications in newborns with dry care. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC6953818/. Imechukuliwa 16.07.2021
Zupan J, et al. Topical umbilical cord care at birth. Cochrane Database of Systematic Reviews. 2004; 10.1002/14651858.CD001057.pub2. Imechukuliwa 16.07.2021
World Health Organization. Newborn deaths decrease but account for higher share of global child deaths. Inapatikana. http://www.who.int/mediacentre/news/releases/2011/newborn_deaths_20110830/en/. Imechukuliwa 16.07.2021
World Health Organization. Newborns: reducing mortality. Inapatikana: http://www.who.int/news-room/fact-sheets/detail/newborns-reducing-mortality. Imechukuliwa 16.07.2021
Pantoja-Ludueña M. Onfalitis In: Espinoza-Osorio F., editor. La neonatología en la atención primaria de salud. La Paz: Grupo Impresor; 2005. pp. 591–593.
Imdad A, et al. Umbilical cord antiseptics for preventing sepsis and death among newborns. The Cochrane database of systematic reviews. 2013; CD008635 10.1002/14651858.CD008635.pub2
Gallagher PG, et al. Omphalitis. Inapatikana: http://www.emedicine.com/ped/topic1641.htm. Imechukuliwa 16.07.2021