Makala hii imeandikwa kwa nia ya kufundisha namna ya kuzuia mkojo kuponyoka na kuongeza uwezo wa kibofu kutunza mkojo.
Je ni sahihi kwangu kufanya mazoezi ya kuongeza uwezo wa kibofu?
Maamuzi ya kufanya mazoezi ya kuimalisha kibofu hutegemea mara nyingi na kisababishi. Mazoezi ya kuimalisha uwezo wa kibofu hufanyika mara nyingi kutibu tatizo la kushindwa zuia mkojo au kuponyokwa na mkojo. Kuponyoka kwa mkojo hutokea sana kwa wanawake haswa baada ya kujifungua na wanapoingia komahedhi.
Aina za kuponyoka kwa mkojo
Kuna aina mbalimbali za kuponyoka kwa mkojo ambazo ni;
Kuponyoka mkojo kutokana na msongo: Msongo kwenye njia za mkojo hutokana na hali yoyote inayoongeza shinikizo ndani ya via vilivyo kwenye tumbo ikiwa pamoja na kibofu mfano kukohoa, kupiga chafya au kucheka huweza pelekea mkojo kuponyoka
Kuponyoka mkojo kutokana na hamu ya kukojoa: aina hii hutokea pale unapopata haja kali ya kukojoa na kutokana na kibofu kufanya kazi pasipo kudhibitiwa, unajikuta umekojoa kabla hata ya kufika chooni.
Kuponyoka mkojo kutokana na mchanganyiko wa visababishi: aina hii hutokana na ainambili zilizotajwa hapo awali, yaanikutokana na msongo pamoja na hamu kali ya kukojoa.
Kuponyoka kwa mkojo kutokana na kibofu kujaa: Hutokea pale endapo kibofu kimejaa mkojo kisha kutoka wenyewe licha ya kutouruhusi kutoka.
Njia za kuongeza uwezo wa kibofu kutunza mkojo
Kabla ya kuanza mazoezi haya, utashauriwa kuandika kumbukumbu kuhusu hali yako ya kukojoa ambapo utarekodi muda wa kila siku na kila mara unapopata hamu ya kukojoa au mkojo unapoponyoka.
Kwa kutumia kumbukumbu hizi, unaweza kuangalia na kuona kama mazoezi yanamatokeo mazuri au la;
Kujiwekea muda wa kwenda haja ndogo
Kwa kutumia kumbukumbu za muda wako wa kwenda haja ndogo, chelewesha kukojoa kwa muda wa dakika 15 kwenye kila unapopata haja. Utaendelea kuongeza muda kwa jinsi wiki zinavyoenda mpaka uhisi kuwa muda unatosha.
Kuchelewesha kukojoa
Unapopata hamu ya kwenda haja ndogo, zuia kukojoa kwa muda wa dakika 5 kwanza na kisha kwenda kukojoa. Baada ya hapo unaweza kuendelea ongeza muda huo kwa dakika 10 mpaka pale utakapoweza kuchelewesha kukojoa kwa muda wa masaa 3 hadi 5.
Kama hamu inakuwa kali zaidi, jaribu kusahaulisha akili yako kwa kuhesabu namba kwa kurudi nyuma kutoka 100 hadi 1 au kufanya tafakuri wakati unavuta pumzi kwa kina.
Ikiwa unashindwa kuzuia kwa muda mrefu zaidi baada ya hizi mbinu, unapaswa kuruhusu mkojo utoke na kisha kufanya hivyo utakapopata haja ndogo nyingine.
Mazoezi ya kegeli
Mazoezi ya kegel ni mazoezi ya kuimalisha sakafu ya nyonga ambayo huimarisha misuli inayosukuma au kuzuia mkojo kutoka. Tafiti zimeonyesha kuwa, kuchanganya mazoezi haya na mazoezi mengine ya kudhibiti mkojo kutoka huleta matokeo mazuri zaidi ya kutibu tatizo la kuponyoka kwa mkojo kwa wanawake. Kwa kawaida mazoezi haya hufanyika kwa kubana misuli inayoruhusu mkojo kutoka kwa sekunde 5 kisha kuachia. Muda wa mazoezi huongezeka taratibu kutoka dakika 5 hadi 10 na kuachia mkojo kisha kuongeza muda. Soma zaidi kwenye Makala ya mazoezi ya kuimalisha sakafu ya nyonga.
Njia zingine za kuongeza uwezo wa kibofu kutunza mkojo
Ili kuongeza uwezo wa kibofu kutunza mkojo unaweza fanya mambo yafuatayo;
Dhibiti kiwango cha vinywaji unachokunywa haswa vile vinavyoongeza haja ya kukojoa mfano soda, kahawa na chai
Punguza kiasi cha maji unachokunywa kabla ya kulala kama unakojoa mara kwa mara wakati wa usiku
Kojoa kabla ya kwenda kulala na mara unapoamka asubuhi
Endelea kutunza kumbukumbu za unapopata haja ya kwenda kukojoa na unapokojoa
Mazoezi haya husaidia nini?
Mazoezi ya kibofu husaidia
Kupunguza muda wa kukojoa kwa siku
Kuongeza uwezo wa kibofu kutunza mkojo mwingi zaidi
Kudhibiti haja ya kwenda kukojoa
Matokeo huonekana ndani ya muda gani?
Inaweza kuchukua muda wa hadi wiki 12 kupata matokeo mazuri ya mazoezi haya. Unapaswa kuwa mvumilivu na kuednelea kufanya mpaka utakapopata matokeo unayoyategemea.
Kama utafanya mazoezi haya kwa wiki kadhaa bila kupata matokeo yoyote, unapaswa kuonana na daktari ili kuweza kupatiwa matibabu mengine ikiwa pamoja na dawa au upasuaji.
Mazoezi haya yanaweza kutumika kwa watoto?
Ndio
Mazoezi ya kuongeza uwezo wa kibofu kutunza mkojo yanaweza kutumika kwa watoto wanaokojoa kitandani.
Majina mengine ya makala hii
Makala hii imejibu pia kuhusu;
Mazoezi ya kuzuia mkojo kutoka wenyewe
Mazoezi ya kubana mkojo
Mazoezi ya kuzuia mkojo kutoka wakati wa kupiga chafya na kukohoa
Mazoezi ya Kegel
Mazoezi ya kuimarisha dakafu ya nyonga
Wapi unaweza kupata msaada zaidi?
Ili kupata msaada zaidi, unapaswa kuwasiliana na daktari wako kwa ushauri na tiba inayoendana na tatizo lako.
Wasilina na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba kupitia kiungo cha mawasiliano yetu chini ya tovuti hii.
Rejea za mada hii.
Overflow Incontinence. https://www.uofmhealth.org/health-library/uh1227#:~:text=Overflow%20incontinence%20is%20the%20involuntary,feels%20no%20urge%20to%20urinate. Imechukuliwa 29.11.2021
Inh N. Tran, et al. Urinary Incontinence. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK559095/. Imechukuliwa 29.11.2021
Demaagd, et al. “Management of urinary incontinence.” P & T : a peer-reviewed journal for formulary management vol. 37,6 (2012): 345-361H.