Swali la msingi
Habari daktari, sasa nilikua nauliza mimi ni mwanamke, sehemu yangu ya siri kwa wiki mbili sasa inatoa harufu mbaya na kutokwa na uchafu mweupe, nasikia kujikuna. Inaeza kua ni nini shida?
Majibu

Habari dada, asante kwa kuwasiliana na ULY Clinic. Kutokana na maelezo yako kuwa sehemu ya siri inatoa harufu mbaya sambamba na ute mweupe, na unahisi kujikuna kwa wiki mbili sasa inaonyesha inawezekana unakabiliwa na maambukizi ya ukeni. Hapa chini nitakueleza sababu zinazoweza kuchangia;
Visabaishi vya harufu mbaya ukeni
Visababisho vikuu ni pamoja na;
Maambukizi ya fangasi wa uke
Dalili: Kujikuna sana, ute mweupe kama mtindi, uke kuwa na muwasho na wekundu.
Harufu siyo kali sana, lakini muwasho ni mkubwa.
Vajinosisi ya bakteria
Dalili: Harufu mbaya kama ya samaki, ute wa kijivu au mweupe, huambatana na muwasho au kutokwa na ute mwingi.
Husababishwa na mabadiliko ya bakteria wa kawaida ukeni.
Maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama trikomoniasis
Dalili: Harufu mbaya, ute wa kijani au njano, muwasho, maumivu wakati wa kukojoa au kufanya tendo la ndoa.
Inahitaji matibabu ya haraka.
Visabaishi vingine
Visababishi vingine vinavyoweza kuchangia harufu mbaya ukeni ni pamoja na;
Saratani ya Shingo ya Kizazi
Dalili zinazoweza kujitokeza ni pamoja na;
Kutokwa na harufu kali isiyo ya kawaida ukeni
Kutokwa na damu baada ya tendo la ndoa
Maumivu ya nyonga
Damu isiyo ya kawaida kati ya hedhi au baada ya kukoma hedhi
Hii ni hatari na inahitaji uchunguzi wa PAP smia au kipimo cha kirusi.
Fistula ya uke au puru
Hali hii hupelekea uchafu au kinyesi kutoka ukeni. Harufu huwa kali sana.
Huletwa na madhara ya kujifungua au upasuaji.
Uchafu uliokwama ukeni
Mfano: pedi au tampon iliyosahaulika ukeni
Husababisha harufu mbaya kali sana na maambukizi
Maambukizi ya njia ya mkojo yanayoambatana na uke
Maumivu wakati wa kukojoa, harufu mbaya ya mkojo, na muwasho.
Kutumia sabuni au kemikali zenye manukato ukeni
Huleta muwasho na kuharibu uwiano wa bakteria wa kawaida ukeni.
Unachoweza kufanya kwa sasa ni nini?
Fanya mambo yafuatayo;
Epuka kusafisha uke kwa sabuni kali au manukato. Hii inaweza kuongeza tatizo.
Vaa chupi safi na kavu (isiyo na nailoni , tumia chupi ya pamba).
Usifanye ngono bila kinga hadi utakapopata uchunguzi kamili.
Nenda hospitali au kliniki upate uchunguzi wa kitaalamu. Daktari atachukua sampuli (uchunguzi wa ute) kuthibitisha aina ya maambukizi na kukupa dawa sahihi.
Matibabu ya harufu mbaya ukeni
Matibabu ya harufu mbaya ukeni hutegemea chanzo cha tatizo. Baadhi yake kulingana na vyanzo ni pamoja na;
Maambukizi ya Fangasi: Dawa kama fluconazole au krimu ya clotrimazole.
Vajinosisi ya bakteria: Antibiotiki kama metronidazole (vidonge au krimu).
Magonjwa ya zinaa: Dawa maalum kutegemea na ugonjwa uliogundulika.
Maelezo mengine ya ziada kuhusu harufu mbaya ukeni
Ikiwa dalili ya harufu mbaya ukeni inaambatana na dalili nyingine kama maumivu ya tumbo, kutokwa damu isiyo ya kawaida, au kama umefanya tendo la ndoa bila kinga hivi karibuni, zinaweza kusaidia kufahamu kisababishi. Hivyo wakati wa matibabu usisahau kumwambia daktari dalili zote unazopata.
Ushauri wa kuzingatia
Tafadhali muone daktari mapema ili kuzuia madhara zaidi kama maambukizi kupanda kwenye mfuko wa uzazi au changamoto za uzazi baadaye.
Rejea za mada hii:
Workowski KA, Bachmann LH, Chan PA, et al. Sexually transmitted infections treatment guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021;70(4):1–187.
Sobel JD. Bacterial vaginosis. Annu Rev Med. 2000;51:349–356.
Amsel R, Totten PA, Spiegel CA, Chen KC, Eschenbach D, Holmes KK. Nonspecific vaginitis. Diagnostic criteria and microbial and epidemiologic associations. Am J Med. 1983;74(1):14–22.
Workowski KA, Bolan GA. Sexually transmitted diseases treatment guidelines, 2015. MMWR Recomm Rep. 2015;64(RR-03):1–137.
Van Der Pol B. Trichomonas vaginalis infection: the most prevalent nonviral sexually transmitted infection receives the least public health attention. Clin Infect Dis. 2007;44(1):23–25.
Arbyn M, Weiderpass E, Bruni L, et al. Estimates of incidence and mortality of cervical cancer in 2018: a worldwide analysis. Lancet Glob Health. 2020;8(2):e191–e203.
Schiffman M, Castle PE, Jeronimo J, Rodriguez AC, Wacholder S. Human papillomavirus and cervical cancer. Lancet. 2007;370(9590):890–907.
De Ridder D, Badlani G, Browning A, et al. Fistulas in the developing world. In: Abrams P, Cardozo L, Khoury S, Wein A, editors. Incontinence. 5th ed. Paris: ICUD-EAU; 2013. p. 1525–1566.
Handa VL, Van Le L. Vaginal foreign bodies: diagnosis and management. UpToDate. Waltham, MA: UpToDate Inc. [Accessed 2025 Apr 18].
Stamm WE, Norrby SR. Urinary tract infections: disease panorama and challenges. J Infect Dis. 2001;183(Suppl 1):S1–S4.
Foxman B. Epidemiology of urinary tract infections: incidence, morbidity, and economic costs. Am J Med. 2002;113(Suppl 1A):5S–13S.
Nunn KL, Forney LJ. Unraveling the dynamics of the human vaginal microbiome. Yale J Biol Med. 2016;89(3):331–337.