Swali la msingi
Habari doctor, nimesoma kuhusu propranol kwenye tovuti yako ya ULY CLINIC, Sasa shida yangu ni kuwa nakuwa natetemeka kutokana na hofu hali inayopeleke kushindwa kuongea mbele za watu au naongea kwa kutetemeka sana nilikuwa nahitaji dawa ya kuondokana na shida hii inanifanya nakuwa sijiamini kabisaa mbele za watu.
Majibu

Habari yako na asante sana kwa ujumbe wako wa kutumia tovuti yetu kusoma makala. Pole sana pia kwa hali unayopitia, ni jambo la kawaida kabisa kwa watu wengi kukumbwa na hofu au wasiwasi wanapojaribu kuongea mbele za watu, lakini ni vizuri pia kuwa umeamua kutafuta msaada kwa kuwa kuna suluhisho.
Kuhusu tatizo lako
Kutetemeka, moyo kwenda mbio, kukosa ujasiri au hata kuduwaa unapotakiwa kuongea mbele za watu kunaweza kuwa dalili za hofu ya kijamii au aina ya hofu ya kutenda. Hali hii inaweza kudhibitiwa kwa njia mbalimbali, kutegemeana na tatizo na uzito wake.
Kuhusu propranolol
Propranolol ni dawa ya kundi la vifunga risepta beta, hutumika mara kwa mara kusaidia kudhibiti dalili za kimwili za hofu kama vile:
Kutetemeka
Moyo kwenda mbio
Kutokwa jasho
Kuhisi presha kabla ya kuongea au ku-tenda jambo
Kwa watu wengi, propranolol hufanya kazi vizuri sana kwa hofu inayojitokeza katika hali fulani tu, kama vile kuongea mbele za watu au kufanya mawasilisho. Inapotumika kwa kazi hii, huwa inatumiwa dakika 30–60 kabla ya tukio linalosababisha hofu.
Jambo la muhimu kufahamu
Ingawa propranolol husaidia kupunguza dalili za hofu, haiondoi chanzo cha hofu yenyewe, kwa hiyo inaweza kuwa vizuri kuchanganya na:
Tiba saikilojia//Tabia/Ufahamu
Mazoezi ya kujiamini
Kujiandaa vyema kabla ya kuzungumza
Dozi ya propranolo ikoje?
Mfano wa dozi ya kawaida kwa hofu ya kuongea mbele za watu ni
Propranolol ya kunywa miligramu 10 hadi miligramu 40, ikitumika dakika 30–60 kabla ya tukio (kutegemeana na mwitikio wa mtu). Usitumie dawa bila ushauri wa daktari, hasa kwa mara ya kwanza ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kutokea.
Ushauri
Onana na daktari ili akupime afya yako kwa ujumla na kuhakikisha hakuna magonjwa mengine yanayoweza kuzuiwa kutumia propranolol (mfano: pumu, presha ya chini, matatizo ya moyo n.k).
Ikiwa upo sawa kiafya, unaweza kuandikiwa propranolol kwa matumizi ya wakati maalumu na daktari wako.
Fuatilia pia tiba saikilojia/tabia/ufahamu ili kupata suluhisho la kudumu.
Wapi utapata maelezo zaidi?
Pata maelezo zaidi katika makala zifuatazo au kwa kuwasiliana na daktari wako;
Rejea za mada hii:
Steenen SA, van Wijk AJ, van der Heijden GJMG, van Westrhenen R, de Lange J. Propranolol for the treatment of anxiety disorders: Systematic review and meta-analysis. J Psychopharmacol. 2016;30(2):128–39.
Tyrer P. Propranolol in the treatment of anxiety. Br J Psychiatry. 1988;152:200–2.
Hofmann SG, Asnaani A, Vonk IJJ, Sawyer AT, Fang A. The Efficacy of Cognitive Behavioral Therapy: A Review of Meta-analyses. Cogn Ther Res. 2012;36(5):427–40.
Schneier FR, Blanco C, Antia SX, Liebowitz MR. The social anxiety spectrum. Psychiatr Clin North Am. 2002;25(4):757–74.
Clark DM, Wells A. A cognitive model of social phobia. In: Heimberg RG, Liebowitz MR, Hope DA, Schneier FR, editors. Social phobia: Diagnosis, assessment, and treatment. New York: Guilford Press; 1995. p. 69–93.