Swali la msingi
Mimi nimetumia misotroposal vidonge 4 leo siku ya 3 damu zinatoka kidogo kidogo sana. Mimba ilikuwa ya wiki 4. Je ni kawaida? Nifanyeje ili itoke angalau kama inavyotokaga nikiwa kwenye siku zangu?
Majibu

Pole sana kwa changamoto unayopitia. Maelezo yako yanaonyesha umetumia misoprostol (vidonge 4) kwa ajili ya kutoa mimba ya wiki 4, na sasa ni siku ya 3, lakini damu inatoka kidogo sana. Hali hii inaweza kuwa ya kawaida kwa baadhi ya wanawake, lakini pia inaweza kuashiria kuwa;
Mimba bado haijatoka kikamilifu
Kwa ujauzito wa wiki 4, mara nyingine mwili huondoa mimba kimya kimya na damu haitoki nyingi kama hedhi ya kawaida. Lakini pia kuna uwezekano kuwa kuna masalia ya mimba au mimba imeshindwa kutoka kabisa.
Ushauri wa nini unavyoweza kufanya sasa
1. Fanya kipimo cha picha ya mionzi sauti ya kizazi
Kipimo hiki cha picha ya mionzi sauti ya kizazi (ultrosound) kinaweza kuthibitisha kama mfuko wa mimba bado una mabaki ya mimba au la. Hii ndiyo njia salama ya kujua kama dawa zilifanya kazi.
2. Wahi hospitali
Tafadhali nenda hospitali ya karibu au kituo cha afya kwa vipimo na ushauri wa kitaalamu kama una dalili zifuatazo;
Maumivu makali yasiyoisha
Homa au baridi kali
Kutokwa na uchafu ukeni wenye harufu mbaya
Kutokwa damu nyingi sana ghafla
3. Kusubiri siku chache zaidi
Kwa baadhi ya wanawake, damu huanza kutoka polepole kisha huongezeka baada ya siku 3–5. Kama hakuna mabadiliko baada ya siku 7, ni muhimu sana kwenda hospitali.
4. Usijaribu kuongeza dozi bila ushauri wa daktari
Kuongeza dozi ya misoprostol bila uangalizi kunaweza kusababisha hatari ya kutoka damu nyingi au maambukizi kwenye kizazi.
5. Kawaida damu hutoka kwa siku 1 hadi 2 baada ya misoprostol
Kama damu haitoki kabisa au ni ndogo sana kwa muda mrefu, inaweza kuwa mimba imeshindwa kutoka. Wengine hupata damu ndogo lakini tayari mimba imetoka hivyo kipimo cha picha ya mionzi sauti ya kizazi ndicho kitathibitisha.
Kupima homoni za ujauzito
Unaweza kufanya kipimo cha mkojo cha ujauzito baada ya siku 14 tangu kutumia dawa hizi. Utapaswa kutumia kinga wakati unashiriki ngono ili kuepuka kupata mimba nyingine.
Rejea za mada hii:
World Health Organization (WHO). Medical management of abortion. Geneva: WHO; 2018. p. 10–25.
Raymond EG, Harrison MS, Weaver MA. Efficacy of misoprostol alone for first-trimester medical abortion: a systematic review. Obstet Gynecol. 2019;133(1):137–47. doi:10.1097/AOG.0000000000003017.
Tang OS, Gemzell-Danielsson K, Ho PC. Misoprostol: pharmacokinetic profiles, effects on the uterus and side-effects. Int J Gynaecol Obstet. 2007;99 Suppl 2:S160–7. doi:10.1016/j.ijgo.2007.09.009.
Grossman D, Grindlay K. Alternatives to surgical evacuation for early pregnancy failure. Curr Opin Obstet Gynecol. 2011;23(6):448–53. doi:10.1097/GCO.0b013e32834cb7f1.
American College of Obstetricians and Gynecologists (ACOG). Medical management of first-trimester abortion. Practice Bulletin No. 225. Obstet Gynecol. 2020;136(4):e31–47.