Swali muhimu
Habari daktari, nina maumivu ya goti ninapo chuchumaa, kupiga magoti na wakati nakimbia hata nikitulia maumivu yanababua kama moto. nataka nijue kwa uzoefu wako haya yanatokana na nini na tiba zake. Maana nimepima uric acid iko normal, RF iko normal, Athritis hakuna, sukari iko normal, presha pia iko normal Na x-ray pia haioni kitu. Kwa utalaam wako ni nini visababishi?
Majibu

Asante kwa maelezo ya kina, na pole sana kwa maumivu ya goti. Kwa mujibu wa maelezo yako—vipimo vya uric acid, RF (Rheumatoid Factor), X-ray, sukari, na shinikizo la damu vyote ni vya kawaida, hii inaondoa sababu nyingi kuu za kimfumo wa mifupa kama arthraitis, gauti, au osteoatharaitis.
Visababishi
Hali hii inaonyesha maumivu ya goti ambayo hayana uhusiano na magonjwa ya damu au uharibifu wa mifupa unaoonekana kwa X-ray, lakini bado yanaumiza hasa unapochuchumaa, kupiga magoti au kukimbia. Kwa uzoefu wa kitaalamu, hivi ni baadhi ya visababishi vinavyowezekana vimeorodheshwa hapa chini;
1. Kondromalesia ya patella (Sindromu ya fupa patela-paja)
Hii ni hali ambapo katileji chini ya patella (kifupa cha mbele ya goti) inakuwa dhaifu au kuharibiwa.
Huchochewa na kupiga magoti, kupanda ngazi, au kukimbia.
Huweza kusababisha maumivu ya kuchoma au kuungua kama moto hasa mbele ya goti.
Kwa sababu katileji haionekani kwa urahisi kwenye X-ray, inahitaji kipimo cha MRI kama kuna shaka kubwa.
2. Tendinaitis (Michomokinga ya nyuzi zinazoshikilia goti)
Mara nyingi huathiri nyuzi ya patela iliyopo chini ya goti au nyuzi za misuli ya mbele ya paja inayojishikiza juu ya goti. Hii hutokea kwa watu wanaofanya shughuli nyingi za kuruka, kukimbia au kubeba mizigo. Maumivu huongezeka unapopinda goti, kuchuchumaa, au kuinuka ghafla.
3. Mkereketo kwenye Basa
Mifuko midogo yenye majimaji kwa ndani (Basa) kwenye goti inayolinda goti inapopata mkereketo kwa sababu ya kuchokoza magoti mara kwa mara mfano kazini au kwenye sala, husababisha maumivu makali, haswa unapopiga magoti.
4. Uwiano usiosawa wa misuli ya paja (misuli dhaifu ya paja)
Misuli ya mapaja ikiwa dhaifu au kutofautiana nguvu, inaweza kuvuruga usawaziko wa goti, na hivyo kusababisha maumivu hasa kwenye harakati kama kuchuchumaa au kukimbia.
5. Maumivu ya rufaa kutoka mgongoni
Ingawa haitokei mara nyingi, matatizo ya neva kwenye mgongo wa chini (L4–L5) yanaweza kuleta maumivu kwenye goti bila kuonyesha tatizo moja kwa moja gotini.
Tiba na ushauri wa kitaalamu
Tiba isiyo ya dawa
Fanya mazoezi ya kuimarisha misuli ya paja na nyuma ya paja.
Epuka kukaa kupiga magoti kwa muda mrefu au kuchuchumaa mara kwa mara.
Tumia barafu kwa dakika 15–20 baada ya shughuli ya kutembea.
Paka dawa ya kutuliza maumivu kama diclofenac gel
Vaa viatu vyenye unyumbufu mzuri, epuka visigino virefu.
Tiba ya dawa (kwa muda mfupi)
NSAIDs (kama ibuprofen, diclofenac) kwa siku chache tu iwapo maumivu ni makali.
Dawa za kulainisha katileji kama glukosamine na kondroitin zinawasaidia baadhi ya watu.
Fiziotherapia
Inasaidia sana kwa kurekebisha hali ya mijongeo, kunyoosha na kuimarisha misuli.
Mtaalamu wa fiziotherapi anaweza kukusaidia kwa kutumia tiba ya mionzi sauti au mwale wa leza kama kuna michomokinga.
Hitimisho
Kwa kuwa vipimo vyote vya msingi ni vizuri, na X-ray haioneshi uharibifu wa mfupa, maumivu yako yanaweza kutokana na shida za tishu laini za goti (katileji, tendoni, basa). Hali kama Kondromalesia ya Patela au tendinaitis ndiyo zinazofanana zaidi na dalili zako. Napendekeza uanze kwa mazoezi maalum na uonane na fiziotherapia. Kama maumivu hayaishi, MRI inaweza kusaidia kufuatilia zaidi hali ya katileji na mishipa.
Rejea za mada hii:
Cross M, Smith E, Hoy D, Nolte S, Ackerman I, Fransen M, et al. The global burden of hip and knee osteoarthritis: estimates from the Global Burden of Disease 2010 study. Ann Rheum Dis. 2014;73(7):1323–30.
Bhosale AM, Richardson JB. Articular cartilage: structure, injuries and review of management. Br Med Bull. 2008;87(1):77–95.
Panni AS, Tartarone M, Patricola A, Paxton EW, Fithian DC. Patellofemoral pain syndrome. Knee Surg Sports Traumatol Arthrosc. 2005;13(7): 498–506.
Khan KM, Cook JL, Bonar F, Harcourt P, Astrom M. Histopathology of common tendinopathies. Sports Med. 1999;27(6):393–408.
Doral MN, Donmez G, Turhan E, Atay OA, Demirel M, Tandogan RN. Pathophysiology of patellofemoral pain: a review. Acta Orthop Traumatol Turc. 2012;46(6):404–9.
Warden SJ, Davis IS, Fredericson M. Management and prevention of bone stress injuries in long-distance runners. J Orthop Sports Phys Ther. 2014;44(10):749–65.
Wood L, Muller S, Peat G. Knee osteoarthritis in general practice: care and outcomes in the STOPP cohort. Br J Gen Pract. 2007;57(541):95–101.
Cook JL, Rio E, Purdam CR, Docking SI. Revisiting the continuum model of tendon pathology: what is its merit in clinical practice and research? Br J Sports Med. 2016;50(19):1187–91.