
Meloxicam ni dawa ya maumivu jamii ya NSAIDs inayotumika kwa matibabu ya hali na magonjwa mbalimbali yanayosababisha uvimbe kutokana na mwitikio wa kinga ya mwili na maumivu.
Makala hii imezungumzia kwa undani kuhusu magonjwa, maudhi, madhara na vizuizi vya matumizi ya meloxicam.
Meloxicam inatibu nini?
Hali na magonjwa yafuatayo hutibiwa kwa kutumia meloxicam;
Kupunguza maumivu na uvimbe kwenye mifupa na misuli.
Kutibu magonjwa ya maumivu ya viungo, ikiwemo:
Maumivu ya kusagana kwa mifupa – Ugonjwa wa kuharibika kwa viungo katika maeneo ya makutano ya mifupa.
Baridi yabisi – Ugonjwa wa kingamwili unaoshambulia viungo.
baridi yabisi ya watoto (kwa watoto kuanzia miaka 2).
Kutuliza maumivu ya mgongo, misuli, na majeraha ya mwili.
Kupunguza uvimbe na maumivu ya gauti.
Maudhi ya meloxicam
Baadhi ya watu wanaweza kupata maudhi madogo yafuatayo mara wanapotumia meloxicum;
Maudhi kwenye mfumo wa mmeng'enyo wa chakula: Kichefuchefu, kiungulia, gesi, au kuhara.
Kizunguzungu au maumivu ya kichwa.
Uvimbaji wa mwili (maji mwilini).
Mpele au kuwashwa kwenye ngozi.
Madhara ya meloxicam
Dalili hizi zinaashiria uhitaji wa msaada wa kitabibu wa haraka ili kuokoa maisha ya mtu;
Kuvia damu tumboni: Huonekana na dalili ya kinyesi cheusi, kutapika damu au dalili za vidonda vya tumbo.
Shida za moyo: Hatari ya mshtuko wa moyo, kiharusi, au shinikizo la damu.
Kufeli kwa figo: Huonekana na dalili ya kupungua kwa mkojo, kuvimba mwili, uchovu mwingi.
Mzio mkali( mzio wa anafailaksia): Huonekana na dalili za kuvimba uso, koo, au kushindwa kupumua.
Usumu kwenye ini: Huonekana na dalili ya ngozi na macho kuwa ya njano na mkojo mweusi.
Watu gani wanapaswa kuepuka meloxicam?
Inashauriwa usitumie meloxicam ikiwa una hali au magonjwa yafuatayo;
Mjamzito (hasa katika kipindi cha mwisho) – Inaweza kudhuru mtoto tumboni.
Una vidonda vya tumbo au umewahi kupata tatizo la kuvia damu tumboni.
Una ugonjwa sugu wa figo au ini.
Una matatizo ya moyo au umewahi kupata kiharusi.
Una mzio wa dawa jamii ya NSAIDs kama aspirin, ibuprofen, naproxen n.k.
Una shinikizo kubwa la damu lisilodhibitiwa.
Tahadhari Muhimu wakati wa kutumia meloxicam
Unapaswa kuzingatia tahadhari hizi wakati wa kutumia meloxicam ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza;
Kabla ya kunywa hakikisha unatumia dawa ukiwa umekula chakula ili kupunguza hatari ya vidonda vya tumbo.
Usitumie pamoja na kilevi (pombe)Â kwani huongeza hatari ya kuvia kwa damu tumboni.
Usitumie pamoja na dawa za kueyusha damu (mfano warfarin)Â bila ushauri wa daktari.
Rejea za mada hii:
ULY CLINIC. Meloxicam.https://www.ulyclinic.com/dawa/meloxicam .Imechukuliwa 15.03.2025
Khalil NY, Aldosari KF. Meloxicam. Profiles Drug Subst Excip Relat Methodol. 2020;45:159-197. doi: 10.1016/bs.podrm.2019.10.006. Epub 2019 Dec 12. PMID: 32164967.
Dalal D, et al. Meloxicam and risk of myocardial infarction: a population-based nested case-control study. Rheumatol Int. 2017 Dec;37(12):2071-2078. doi: 10.1007/s00296-017-3835-x. Epub 2017 Oct 13. PMID: 29030657; PMCID: PMC8143590.
Drug bank. Meloxicam. https://go.drugbank.com/drugs/DB00814. Imechukuliwa 15.03.2025
Fleischmann R, et al. Expert Opin Pharmacother. 2002 Oct;3(10):1501-12. doi: 10.1517/14656566.3.10.1501. PMID: 12387696.