Swali muhimu
Habari daktari, nina shida, tar 21 mwezi huu niliharibikiwa mimba ya miezi mi nne (4) nikaenda kituo cha afya nikasafishwa lakin tumbo lilikuwa bado linauma nikarudi tena kiumbe kikatoka lakini sikusafishwa tena nikapewa antibiotics nikameza na nika maliza dozi sasa damu bado zinatoka. Nikakaa wik 2 tena nikaenda hospitali nikapiga ultrasound wakasema hamna uchafu lakini nikapewa dawa za kukata damu lakini damu zinaendelea kutoka mpaka sasa. Jana nimetoka hospitali nikaonana na dokta wa wanawake ameniandikia ultrasound tena wakasema uchafu umebaki na kuniandikia miso na oxytocin kukata damu hii imekaaje na pia nina damu ndogo ambayo ni 7 naomba msaada tafadhali.
Majibu
Ufafanuzi wa hali yako na maelezo muhimu ya kitaalamu
Hapa chini nimefafanua kuhusu dalili zako ili kuwa na uelewa wa undani sambamba na kutoa ushauri wa awali. Utapaswa kuwasiliana na daktari wako ili kupata ufafanuzi zaidi na hatua zinazofuata.

1. Kuharibika kwa mimba na kusafishwa (Evacuation)
Baada ya mimba kuharibika ukiwa na miezi minne, hatua ya kusafishwa mji wa mimba ni ya muhimu sana ili kuhakikisha mabaki yote yanatolewa. Hii husaidia kuzuia maambukizi, kutokwa damu, na matatizo ya baadaye.
Kusafishwa hufanywa kwa njia ya dawa au upasuaji mdogo.
Ikiwa mabaki bado yanabaki, damu huendelea kutoka na maumivu yanaweza kuendelea.
Kusafishwa kwa kiwango kidogo au kutokamilika husababisha kubakia kwa mabaki ya ujauzito kwenye kizazi
2. Kupima kwa Ultrasound na kuendelea kutokwa damu
Ultrasound husaidia kutathmini kama bado kuna mabaki kwenye mji wa mimba baada ya kusafishwa. Kukutwa na mabaki baada ya vipimo viwili ni jambo la kuangaliwa kwa makini.
Vipimo vya awali huenda vilikosa kuona mabaki au hayakuwa yameonekana wazi.
Damu kuendelea kutoka kwa wiki kadhaa ni dalili kwamba mji wa mimba haujasafishika au kuna tatizo jingine kama vile kutoganda kwa damu
Dawa za kukata damu peke yake hazitoshi kama kuna mabaki ya ujauzito.
3. Dawa Ulizopewa: Misoprostol na Oxytocin
Baada ya kugundulika kuwa bado kuna mabaki, daktari ameamua kutumia dawa za kusaidia kusafisha kwa njia ya asili kupitia misuli ya mji wa mimba.
Misoprostol:
Hufanya mji wa mimba kusinyaa na kutoa mabaki.
Inaweza kuambatana na maumivu na kuvuja damu kwa muda.
Oxytocin:
Huchochea mikazo ya mji wa mimba na kusaidia kukata damu.
Hupunguza hatari ya kuvuja damu nyingi na maambukizi.
4. Kiwango kidogo cha damu – Haemoglobin 7 g/dL
Kiwango cha damu 7 g/dL ni chini kuliko kawaida na kinahitaji uangalizi wa karibu ili kuzuia madhara zaidi ya kiafya.
Inaweza kusababisha dalili kama uchovu, kizunguzungu, moyo kwenda mbio, na kupumua kwa shida.
Sababu kubwa ni kupoteza damu nyingi baada ya mimba kuharibika.
Kutibiwa kwa dawa za kuongeza damu au kuongezewa damu hospitalini inaweza kuwa muhimu kulingana na hali yako.
Ushauri muhimu kwa sasa
Kwa kuzingatia hali yako, kuna hatua unapaswa kuchukua mara moja ili kulinda afya yako.
Tumia dawa zote ulizoandikiwa kwa kufuata maagizo ya daktari.
Kama damu zinaendelea kutoka kwa wingi au unapata maumivu makali, rudi hospitali haraka.
Pumzika vya kutosha; epuka shughuli nzito au kunyanyua vitu vizito.
Kula chakula chenye madini ya chuma (kama maini, mboga za majani, kunde, dagaa) ili kusaidia kuongeza damu.
Fuatilia hali yako ya damu kwa vipimo vya mara kwa mara hadi iwe juu ya 10 g/dL.
Mambo ya kuelewa
Misoprostol na Oxytocin hutumika kusaidia mji wa mimba kujisafisha kwa kusinyaza. Lakini kama uchafu bado hautoki, inaweza kuhitajika usafishwe tena kwa upasuaji.
Haemoglobin 7 ni ya chini sana. Ikiendelea kushuka au kama uko na dalili kama kizunguzungu, uchovu mwingi, mapigo ya moyo kwenda kasi unaweza kuhitaji kuongezewa damu.
Ni vizuri ufuatiliwe kwa karibu na daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, na pia vipimo vya damu kama picha kamili ya damu vinaweza kuhitajika mara kwa mara ili kuona hali yako inavyoendelea.
Ushauri wa haraka
Fuata dozi ya Misoprostol na Oxytocin kama ulivyoelekezwa.
Rudi hospitali haraka kama:
Una damu nyingi mno au nzito.
Maumivu ya tumbo yanakuwa makali zaidi.
Unapoteza fahamu, unazimia au una dalili za upungufu mkubwa wa damu.
Fanya ultrasound ya kufuatilia kama hali haijaimarika baada ya dawa.
Ulizia kuhusu uwezekano wa kuongezewa damu kama dalili za anemia ni kali.
Shirikishana na daktari kufanya vipimo vingine kuangalia kama una madhaifu ya kuganda kwa damu ili kujiridhisha kuwa huna.
Ratiba ya mlo wa muongeza damu kwa siku nzima
Kwa sababu unaendelea kutokwa na damu na inaonekana unaupungufu pia, unaweza kufuata ratiba hii kwa angalau wiki 2 hadi 4, sambamba na kutumia dawa za madini chuma kama utakavyoandikiwa na daktari. Omba ushauri wa daktari wako kama mpango huu unafaa kwako.
Asubuhi (Saa 12 - 2 asubuhi)
Uji wa dona au ulezi uliopikwa na maziwa au na kutiwa ndimu
Tunda: Embe, parachichi au chungwa
Kidonge cha madini chuma kama ulivyoandikiwa (kinywaji chenye vitamini C kisaidie kufyonzwa vizuri)
Mchana (Saa 7 - 9 mchana)
Wali wa mchele au ugali wa dona
Maharage au dengu
Mboga za majani: Mchicha, matembele au kisamvu
Tunda: Papai au tikiti
Jioni (Saa 12 - 2 usiku)
Supu ya maini, samaki, au kuku aliyechemshwa (kidogo tu kama uwezo unaruhusu)
Mkate wa kahawia au viazi vilivyochemshwa
Bilauri ya juisi ya limao au machungwa
Vitu vya Kuepuka kwa sasa
Chai ya rangi (huchelewesha kufyonzwa kwa madini ya chuma)
Kahawa
Kunywa dawa za iron sambamba na maziwa (zinapunguza ufyonzwaji)
Rejea za mada hii:
World Health Organization. Clinical Practice Handbook for Safe Abortion. Geneva: WHO; 2014.
Royal College of Obstetricians and Gynaecologists. The Management of Early Pregnancy Loss. Green-top Guideline No. 25. London: RCOG; 2016.
American College of Obstetricians and Gynecologists. Early Pregnancy Loss: Practice Bulletin No. 200. Obstet Gynecol. 2018;132(5):e197–e207. doi:10.1097/AOG.0000000000002958
Tang OS, Gemzell-Danielsson K, Ho PC. Misoprostol: Pharmacokinetic profiles, effects on the uterus and side-effects. Int J Gynaecol Obstet. 2007;99 Suppl 2:S160–7. doi:10.1016/j.ijgo.2007.09.004
Hofmeyr GJ, Gülmezoglu AM, Pileggi C. Oxytocin for the prevention of postpartum haemorrhage: A systematic review. BJOG. 2005;112(9):1121–8. doi:10.1111/j.1471-0528.2005.00737.x
Breymann C. Iron deficiency anemia in pregnancy. Semin Hematol. 2015;52(4):339–47. doi:10.1053/j.seminhematol.2015.07.003
World Health Organization. Iron Deficiency Anaemia: Assessment, Prevention and Control. A guide for programme managers. Geneva: WHO; 2001.
Pavord S, Daru J, Prasannan N, Robinson S, Stanworth S, Girling J. UK guidelines on the management of iron deficiency in pregnancy. Br J Haematol. 2020;188(6):819–30. doi:10.1111/bjh.16221
Hurrell R, Ranum P, de Pee S, Biebinger R, Hulthen L, Johnson Q, et al. Revised recommendations for iron fortification of wheat flour and an evaluation of the impact of recent national wheat flour fortification programs. Food Nutr Bull. 2010;31(1_suppl):S7–21. doi:10.1177/15648265100311S102
Abbaspour N, Hurrell R, Kelishadi R. Review on iron and its importance for human health. J Res Med Sci. 2014;19(2):164–74.