Swali: Kama ulikuwa na mwenza mwenye group B+(mwanaume) mkazaa na mwanamke mwenye group B-. Baadae mwanamke akakutana na mwanaume mwingine mwenye group O+ inakuwaje kupata mtoto?
Ufafanuzi wa swali
Lengo la swali hili ni kutaka kufahamu kuwa kama mimba itaharibika, endapo mwanamke mwenye kundi B la damu yenye hali hasi ya rhesus yaani (B-) aliyezaa na mwanaume mwenye damu kundi B yenye hali chanya ya rhesus yaani (B+).
Jibu
Ugonjwa wa rhesus unaosababisha kuharibika kwa mimba zinazofuata hutokea kwa wanawake wenye makundi hasi ya damu mfano (A-, AB-, B-, O-) kama watabeba mimba kutoka kwa wanaume wenye kundi chanya la damu yaani A+, AB+, B+, O+.
Kumbuka: Rhesus ni aina ya protini zinazopatikana kwenye kuta za chembe nyekundu za damu. Kama damu ina protini hizi, mtu huyu huitwa rhesus chanya au alama + hutumika, na endapo chembe nyekundu za damu hazina protini hii hufahamika kama rhesus hasi au alama - hutumika.
Nini hutokea mwanamke mwenye kundi hasi la damu akibeba mimba ya mwanaume mwenye kundi chanya?
Kibiolojia mtoto atarithi hali chanya ya rhesus kutoka kwa baba, endapo mama ana hali hasi ya rhesus.
Kwa mimba ya kwanza mama mwenye hali hasi ya rhesus anaweza kubeba ujauzito wake mpaka kujifungua bila shida yoyote, hata hivyo mara nyingi wakati wa kujifungua mfumo wa kinga ya mwili hutambua kuwa mama alikuwa amebeba mtoto mwenye damu yenye hali ya rhesus tofauti na yake. Na hii ni kutokana na kuchangamana kwa damu mbili, yaani damu ya mtoto kutoka kwenye kondo la nyuma au kitovu na damu ya mama kutoka kwenye majeraha yaliyofanyika wakati wa uzazi.
Kuchangamana kwa damu kunaweza tokea pia kama;
Kujipenyeza kwa chembe za damu ya mtoto kwenye mfumo wa damu wa mama kutatokea mtoto akiwa tumboni
Mama atatokwa damu wakati wa ujauzito
Mama atafanyiwa kipimo cha kuchukua maji kutoka kwenye chupa ya uzazi (amniosentesis au CVS)
Majeraha yataokea kwenye tumbo la uzazi
Mfumo wa kinga ya mwili wa mama kwa vile hutambua protini za rhesus (Kutoka kwa mtoto alizorithi kutoka kwa baba) kuwa ni kitu kigeni, huanza kutengeneza kemikali zenye jina la antibodi kwa ajili ya kufanya mashambulizi ya kuziondoa kabisa. Mashambulizi huwa madogo kwa ujauzito wa kwanza na hivyo mama anaweza kujifungua salama. Hata hivyo endapo mama atabeba ujauzito unaofuata kutoka kwa baba mwenye kundi chanya la damu yaani A+, AB+, B+ na O+, mashambulizi hayo huharibu mimba.
Matokeo ya mimba zinazofuata baada ya mimba ya kwanza
Kama mama alichoma sindano ya anti-D, wakati wa ujauzito wa kwanza kabla ya kujifungua, alizuia mfumo wa kinga ya mwili kutambua damu ya rhesus chanya kutoka kwa mtoto na hivyo kutotengenezwa kwa antibodi zinazoweza kushambuliwa ujauzito huu na kuharibu mimba. Anti-Di huchomwa kwa kila ujauzito zinazofuata.
Na endapo anti-D haikutumiwa na mama mwenye kundi hasi la damu kabla ya kujifugua au kabla ya mimba ya kwanza kuharibika (kutoka yenyewe au kutolewa), mimba hii endapo imepatikana kutoka kwa mwanaume mwenye hali chanya ya rhesus kutoka kundi lolote la damu (yaani A+, AB+, B+ na O+) itaharibika.
Pata maelezo zaidi ya Rhesus na mimba kuharibika kwenye makala ya Rhesus na ujauzito
ULY CLinic inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri unaoendana na hali yako kabla ya kuchukua hatua yoyote baada ya kusoma makala hii.
Pia unaweza wasiliana na daktari wa ULY Clinic kwa ushauri na tiba kupitia linki ya 'Pata tiba' au 'Wasiliana nasi' iliyo chini ya tovuti hii.
Rejea za mada hii;
NHS. Rhesus disease. https://www.nhs.uk/conditions/rhesus-disease/causes/#. Imechukuliwa 12/5/2022
John Costumbrado, et al. Rh Incompatibility. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK459353/. Imechukuliwa 12/5/2022
Frequently asked questions. Pregnancy FAQ027. The Rh factor: How it can affect your pregnancy. American College of Obstetricians and Gynecologists. https://www.acog.org/Patients/FAQs/The-Rh-Factor-How-It-Can-Affect-Your-Pregnancy. Imechukuliwa 12/5/2022
Moise KJ. Overview of Rhesus (Rh) alloimmunization in pregnancy. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 12/5/2022
Moise KJ. Prevention of Rh (D) alloimmunization. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 12/5/2022
American College of Obstetricians and Gynecologists (ACOG) Committee on Practice Bulletins. Obstetrics. ACOG Practice Bulletin No. 192: Management of alloimmunization during pregnancy. Obstetrics & Gynecology. 2018;131:611.
American College of Obstetricians and Gynecologists (ACOG) Committee on Practice Bulletins. Obstetrics. ACOG Practice Bulletin No. 181: Prevention of Rh D alloimmunization. Obstetrics & Gynecology. 2017;130:e57.