
Wataalamu wa afya wanashauri mama anyonyeshe wakati wote , hata hivyo kuna nyakati ambapo mama anaweza kulazimika kukamua na kuhifadhi maziwa kwa ajili ya matumizi ya baadaye.
Ili kuhakikisha kuwa maziwa yanabaki salama na yenye ubora, ni muhimu kufuata kanuni sahihi za kuhifadhi. Makala hii imeelezea jinsi ya kuhifadhi maziwa, kutumia maziwa yaliyohifadhiwa na viashiria vya maziwa yaliyoharibika.
Jinsi ya Kuhifadhi Maziwa ya Mama
Wakati wa kuhifadhi unapaswa kufahamu namna sahihi ya kuweka mziwa katika vymbo vya kuhifadhia, hali joto na muda wa kuhifadhi maziwa ili yaendelee kuwa na ubora wake.
Namna sahihi ya kuweka maziwa kwenye vymbo ya kuhifadhia
Wakati wa kuweka maziwa yaliyokamuliwa kwenye vyombo vya kuhifadhia mambo yafuatayo yanatakiwa kufanyika;
Vyombo vinavyotakiwa kutumika katika kuhifadhi maziwa ni chupa za plastiki, glasi au mifuko maalumu ya kuhifadhia maziwa ya mama. Hakikisha vyombo ni visafi na havina kemikali ya BPA
Ikiwa unahifadhi maziwa katika vyombo vingi, andika tarehe ya kukamuliwa kwenye chombo cha kuhifadhi ili kuhakikisha unatumia maziwa yaliyokamuliwa kwanza.
Usijaze chombo kupita kiasi; hakikisha maziwa yaliyo ndani hayawezi kujaa na kufurika.
Ikiwa unakamua maziwa mara kwa mara na kwa kiasi kidogo, unaweza kuongeza maziwa mapya kwenye chombo hicho siku hiyo, lakini si baada ya siku hiyo.
Hali joto na muda wa kuhifadhi maziwa
Maziwa ya mama yanapaswa kuhifadhiwa kulingana na hali ya joto ya mahali yanapowekwa kama ifuatavyo;
Joto la chumba ( Nyuzi joto 16-29°C): Ni bora zaidi kuhifadhi kwa masaa 4, japo inakubalika kuhifadhi kwa masaa 6 hadi 8 katika hali ya usafi sana
Jokofu (Nyuzi joto 4°C): Yanabaki salama kwa siku 4 hadi 8, lakini ni bora kutumiwa ndani ya muda mfupi.
Jokofu la kugandisha (Nyuzi joto -20°C): Maziwa yanaweza kuhifadhiwa hadi miezi 6 kwa ubora, pia inakubalika kuhifadhi hadi miezi 12 ikiwa ni lazima.
Jinsi ya kuandaa maziwa kwa mtoto
Uandaaji unategemea hali joto iliyotumika kuhifadhi maziwa kama ifuatavyo
Maziwa yaliyohifadhiwa katika joto la chumba
Fuata hatua zifuatazo kuandaa maziwa yaliyohifadhiwa kwenye joto la chumba;
Kabla ya kuandaa hakikisha maziwa hayajapita muda wa masaa yanayotakiwa tangu yalipokamuliwa.
Inamisha chupa au chombo chenye maziwa juu kwenda chini taratibu ili kuyachanganya, usitikise kwa nguvu.
Weka tone la maziwa nyuma ya mkono wako ili kuhisi kama ni la joto linalofaa. Ikiwa yamepoa unaweza kuyapasha kwa kuweka kwenye bakuli lenye maji ya uvuguvugu.
Mara unapomimina maziwa kwenye chupa, hakikisha unamlisha mtoto na usihifadhi tena mabaki ya maziwa baada ya kula.
Maziwa yaliyohifadhiwa kweye jokofu
Fuata hatua zifuatazo kuandaa maziwa yaliyohifadhiwa kwenye jokofu;
Hakikisha hayajazidi siku zinazopendekezwa tangu yalipokamuliwa
Weka chupa au mfuko wa maziwa ndani ya bakuli lenye maji ya joto la wastani kwa dakika chache.
Inamisha chupa au chombo chenye maziwa juu kwenda chini taratibu ili kuyachanganya, usitikise kwa nguvu. Usitikise kwa nguvu.
Weka tone la maziwa kwenye nyuma ya mkono wako kuhakikisha hayana joto kali sana.
Mara baada ya kuyapasha, tumia maziwa ndani ya saa 2 na usihifadhi tena mabaki.
Maziwa yaliyohifadhiwa kweye jokofu la kugandisha
Fuata hatua zifuatazo kuandaa maziwa yaliyohifadhiwa kwenye jokofu;
Hakikisha hayajazidi siku zinazopendekezwa tangu yalipokamuliwa
Ondoa maziwa kutoka kwenye jokofu la kugandisha na weka kwenye jokofu ili yajeyuke polepole (huchukua takriban saa 12-24).
Weka chupa au mfuko wa maziwa ndani ya bakuli lenye maji ya joto la wastani kwa dakika chache.
Inamisha chupa au chombo chenye maziwa juu kwenda chini taratibu ili kuyachanganya, usitikise kwa nguvu.
Weka tone la maziwa kwenye nyuma ya mkono wako kuhakikisha hayana joto kali sana.
Mara baada ya kuyapasha, tumia maziwa ndani ya saa 24 na usihifadhi tena mabaki.
Mambo ya kuzingatia wakati wa kuandaa maziwa
Yafuatayo ni mambo ya kuzingatia wakati wa kuandaa maziwa kwa ajili ya kumlisha mtoto;
Usipashe maziwa kwa kuchemsha moja kwa moja kwani inaweza kuharibu virutubisho na hata kuyafanya kuwa na joto lisilo sawa, linaloweza kumuunguza mtoto .
Daima pima joto la maziwa kwenye kifundo cha mkono wako kabla ya kumpa mtoto
Usitikise maziwa ili kuchanganya mafuta na sehemu yenye maji zaidi. Badala yake, zungusha maziwa polepole ili kuyachanganya.
Usichanganye maziwa ya joto na yaliyohifadhiwa tayari kwenye jokofu au jokofu la kugandisha
Usihifadhi mabaki ya maziwa
Dalili za Maziwa Yaliyoharibika
Usitumie maziwa yaliyohifadhiwa endapo utaona viashiria vifuatavyo;
Harufu mbaya
Yakitikiswa hayachanganyiki tena
Rangi isiyo ya kawaida
Kubadilika kwa ladha
Maziwa yanaonekana kama yameganda au yana mabonge hata baada ya kupashwa joto
Yamehifadhiwa kwa muda mrefu
Hitimisho
Kuhifadhi maziwa ya mama kwa usahihi kunasaidia mtoto kuendelea kupata virutubisho muhimu hata wakati mama hayupo karibu. Mtoto anapaswa kunywa maziwa haraka iwezekanavyo baada ya kukamuliwa ikiwa hakuna ulazima wa kuhifadhi kwa muda mrefu kwani yana virutubisho bora.
Rejea za mada hii
Breast Milk Storage and Preparation | Breastfeeding – CDC. https://www.cdc.gov/breastfeeding/breast-milk-preparation-and-storage/handling-breastmilk.html. Imechukuliwa 29.03.2025
Handout-hand-expression-and-safe-storage.pdf. WHO. https://cdn.who.int/media/docs/default-source/mca-documents/nbh/enc-course/revised-resources/supplemental-materials/breast-milk-feeding-alternative-methods/handout-hand-expression-and-safe-storage.pdf?sfvrsn=8b1761cd_1. Imechukuliwa 29.03.2025
Breast Milk Storage and Feeding: Guidelines, Safety, Options. Healthline. https://www.healthline.com/health/baby/breastmilk-storage. Imechukuliwa 29.03.2025