Nyama nyekundu ni nini?
Kiafya unaposema nyama nyekundu hunamaanisha nyama yenye mwonekano wa rangi nyekundu. Nyama nyekundu huwa na mwonekano wa rangi yake kutoka kwenye protini za mayoglobin. Mayoglobini ni protini maalumu inayobeba oksijeni ya misuli, ambayo hutumika kuiwezesha misuli kutengeneza nishati inayowezesha kiumbe kufanya kazi mbalimbali za kifiziolojia kama vile kutembea, kupumua, kusukuma damu n.k
Nyama nyekundu hupatikana kwenye viumbe wengi sana wanaoliwa na binadamu ikiwa pamoja na baadhi ya ndege na samaki ambao hudhaniwa siku zote kuwa wana nyama nyeupe. Licha ya kuwa na viumbe jamii ya ndege wanaofahamika kuwa na nyama nyeupe, viumbe hao huwa na nyama nyekundu kwenye sehemu za miili yao ambazo zinafanya kazi zaidi kama kwenye miguu( kwa kuku wanaotembea) na kwenye mabawa kwa ndege wanaopaa, hata hivyo wanyama wenye nyama nyeupe hata kama wana sehemu zenye nyama nyekundu, nyama hiyo endapo itatumiwa haiwezi kufananishwa na kula nyama nyekundu kutoka kwa wanyama wenye nyama nyekundu.
Viumbe gani waana nyama nyekundu
Wanyama wafuatao huwa na nyama nyekundu;
Kware
Kangaroo
Tausi
Nguruwe
Ngombe
Mbuzi
Kondoo
Ngamia
Nyama nyekundu inafaida gani mwilini?
Kwa ujumla nyama nyekundu huupa mwili nishati, mafuta yaliyoshamiri, nishati na madini chuma ya himu kwa wingi. Nyama nyekundu pia ni chanzo kizuri cha vitamin B12 ambacho hakipatikani kwenye nafaka, matunda au mboga za majani. Virutubisho na madini mengine unayoweza kupata kwenye nyama nyekundu ni;
Mafuta yaliyoshamiri
Protini
Madini ya fosforazi
Hasara za nyama nyekundu
Kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya nyama nyekundu katika nchi zinazoendelea kwa sasa kuliko nchi zilizoendelea, hii inaonekana kuwa ni maisha ya kifahari, hata hivyo kuna magonjwa mengi yasiyo ya kuambukizwa ambayo yanazidi kuongezeka kutokana na maisha haya mapya.
Kwa ujumla nyama nyekundu huwa na kiasi kikubwa cha mafuta yaliyoshamiri, nishati na madini chuma ya himu ambayo huhusika na kuongeza hatari ya kuziba mishipa ya damu hivyo kusababisha magonjwa ya moyo kama kiharusi, mshituko wa moyo n.k, huchosha kongozo inayozalisha homon insulin hivyo kuleta ugonjwa wa kisukari na kusababisha saratani ya utumbo mpana.
Licha ya kuwa na hatari hiyo, nyama nyekundu iliyohifadhiwa huwa na hatari zaidi kwa kuwa hutiwa chumvi ( sodiamu) na kemikali mbalimbali ambazo husababisha shinikizo la juu la damu na magonjwa mengine ya moyo na mishipa ya damu.
Mfano wa nyama nyekundu zilizohifadhiwa ili kuongeza radha na muda wa kuishi ni, soseji na zinazofanana nazo. Ni heri kutumia nyama nyekundu ambayobado ni mbichi kuliko iliyohifadhiwa.
Utofauti wa nyama nyekundu na nyama nyeupe
Ili kufahamu utofauti wa nyama nyekundu na nyama nyeupe, tuangalie vilivyomo kwenye gramu 100 za nyama hizo;
Gramu 100 za nyama ya kuku ambaye ametolewa ngozi huwa na;
Kilokalori 175 za Nishati
Gramu 8.43 za Mafuta
Gramu 2.60 za Mafuta yaliyoshamiri
Gramu 25.95 za Protini
Miligramu 0.14 za vitamin B1
Miligramu 0.25 za vitamin B2
Miligramu 8.2 za vitamin B3
Mikrogramu 0.84 za vitamin B12
Miligramu 0.95 za Madini chuma
Miligramu 2.23 za Madini zinki
Miligramu 207 za Madini fosforazi
Miligramu 307 za Madini potasiamu
Vilivyomo kwenye gramu 100 ya nyama nyekundi iliyoyolewa mafuta ni;
Kilokalori 123 za Nishati
Gramu 4.3 za Mafuta
Gramu 1.9 za Mafuta yaliyoshamiri
Gramu 21 za Protini
Miligramu 0.06 za vitamin B1
Miligramu 0.21 za vitamin B2
Miligramu 5.1 za vitamin B3
Miligramu 5.2 za vitamin B5
Miligramu 0.2 za vitamin B6
Mikrogramu 1.9 za vitamin B12
Miligramu 1.3 za Madini chuma
Miligramu 1.7 za Madini zinki
Miligramu 230 za Madini fosforazi
Miligramu 167 za Madini potasiamu
Miligramu 59 za Madini sodiamu
Ni nyama gani nzuri ya kutumia?
Kutokana na umuhimu wa vitamin B na Madini chuma ambayo hupatikana pekee kwenye nyama, nchi nyingi zilizoendelea kwa kuona madhara ya nyama nyekundu kama yalivyoonekana kwenye tafiti, wametilia mkazo matumizi ya nyama nyeupe. Nyama nyeupe huwa na kiasi kidogo cha madini chuma ya himu, mafuta yaliyoshamiri na kolestro ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu kama ilivyokwisha elezewa hapo juu.
Kutokana na ushahidi wa tafiti mbalimbali za binadamu zilizokwisha fanyika, unashauriwa kiafya kutumia nyama nyeupe na kwa kiasi. Vyakula vya nafaka zisizokobolewa, matunda mboga za majani, maziwa, mayai na vyanzo vingine vya protini ni vizuri kutumiwa zaidi ya nyama kwani hupunguza hatari ya magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kama yalivyotajwa hapo juu yanayongezeka kwa kasi na kuleta mzigo katika sekta ya afya.
ULY CLINIC inakushauri siku zote ulinde afya yako kwa kupata taarifa sahihi na zilizofanyiwa tafiti ili kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa na ya kuambukizwa.
Sehemu gani unaweza pata taarifa zaidi kuhusu nyama?
Pata taarifa zaidi kuhusu nyama nyama nyekundu na nyama nyeupe kutoka kwa daktari wako au daktari wa ULY CLINIC au kupitia makala zingine kwa kubofya hapa
Baadhi ya maswali mengine yaliyojibiwa na makala hii ni;
Umuhimu wa nyama nyekundu mwilini
Vyakula vyenye nyama nyekundu
Hasara za nyama nyekundu mwilini
Utofauti wa nyama nyekundu na nyama nyeupe
Baadhi ya maswali na majibu yanayohusu nyma nyekundu
Je nguruwe ni nyama nyeupe?
Ndio!
Nyama ya nguruwe ipo kwenye kundi la nyama nyekundu, japo ikilinganishwa kimwonekano na nyama zilizo kwenye kundi moja, huonekana kuwa nyeupe kutokana na kuwa na kiasi cha chini kidogo cha mayoglobin.
Rejea za mada hii
Monounsaturated Fat. https://www.heart.org/en/healthy-living/healthy-eating/eat-smart/fats/monounsaturated-fats. Imechukuliwa 05.07.2021
A Wolk. Potential health hazards of eating red meat. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/27597529/. Imechukuliwa 05.07.2021
Sabine Rohrmann, et al. Processed meat: the real villain?. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/26621069/. Imechukuliwa 05.07.2021
NHS. Red meat and the bowe cancer. https://www.nhs.uk/live-well/eat-well/red-meat-and-the-risk-of-bowel-cancer/. Imechukuliwa 05.07.2021
NIH. New study shows that eating red meat, processed meat increases heart disease risk. https://www.nhlbi.nih.gov/news/2020/new-study-shows-eating-red-meat-processed-meat-increases-heart-disease-risk. Imechukuliwa 05.07.2021
Laila Al-Shaar, et al. Red meat intake and risk of coronary heart disease among US men: prospective cohort study. https://www.bmj.com/content/371/bmj.m4141. Imechukuliwa 05.07.2021
NCBI. CANCER IN HUMANS. General issues regarding the epidemiology of cancer and consumption of red meat and processed meat. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK507972/#:~:text=(a)%20Red%20meat,and%20is%20usually%20consumed%20cooked.imechukuliwa 17.07.2021