
Baada ya kutumia Misoprostol kwa ajili ya kutoa mimba, siku za kutoka damu zinaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu. Hapa kuna muhtasari wa kinachoweza kutokea:
Siku za Kutoka damu baada ya kutumia Misoprostol
Masaa 1-4 baada ya kutumia Misoprostol:
Damu huanza kutoka, mara nyingi ikiwa nzito kuliko hedhi ya kawaida.
Unaweza kupata maumivu makali ya tumbo kama ya hedhi.
Siku 1-3 baada ya kutumia Misoprostol:
Kutokwa na damu huendelea, ikiwa nzito kwa siku ya kwanza au ya pili.
Vipande vya tishu za kijusi vinaweza kutoka, hasa ndani ya saa 24 za kwanza.
Siku 4-7:
Damu huanza kupungua taratibu, lakini bado inaweza kuwa na mabonge madogo.
Wiki 1-2:
Kwa wanawake wengi, damu hupungua na kuwa kama mabaki ya hedhi ya kawaida.
Wiki 3-4:
Kwa baadhi ya wanawake, matone madogo ya damu yanaweza kuendelea.
Hedhi ya kawaida inatarajiwa kurejea ndani ya wiki 4-6 baada ya utoaji mimba.
Nani hatakiwi kutoa mimba wa kutumia misoprostol?
Utoaji mimba wa kitaalamu kwa kutumia dawa Misoprostol si salama kwa kila mtu. Haupaswi kufanya utoaji mimba wa dawa ikiwa:
Uko kwenye kipindi cha kwanza mwishoni au cha pili cha ujauzito na kuendelea (kwa kawaida zaidi ya wiki 10-12, kulingana na miongozo ya kitabibu.
Una mzio wa dawa za Misoprostol, au dawa zingine zinazofanana.
Umebeba mimba ya nje ya mfuko wa uzazi- mimba iliyo nje ya mji wa mimba haiwezi kutoka kwa kutumia Misoprostol na endapo utatumia unaweza kuhatarisha maisha yako.
Unatumia dawa jamii ya kortikosteroidi kwa muda mrefu- Dawa hizi zinaweza kuathiri ufanisi wa utoaji mimba kwa dawa.
Una kifaa cha uzazi wa mpango(kitanzi) ndani ya mfuko wa mimba – Kitanzi hiki kinapaswa kuondolewa kabla ya kutumia dawa za kutoa mimba ili kuepuka kuharibu kizazi.
Una matatizo ya damu kuganda, upungufu mkubwa wa damu, au kushindwa kwa tezi za adreno, kwani hali hizi zinaweza kuongeza hatari ya madhara makubwa.
Hakuna upatikanaji wa huduma za afya za dharura, endapo kutatokea matatizo kama kutokwa na damu nyingi kupita kiasi, maambukizi, au utoaji mimba usiokamilika unaweza kupoteza maisha kama hutipata huduma ya dharura.
Ikiwa unakabiliwa na mojawapo ya hali hizi, unapaswa kushauriana na mtoa huduma wa afya kuhusu mbinu nyingine salama za utoaji wa mimba.
Tahadhari Muhimu kwa mtumiaji wa misoprostol
Kama unatumia misoprostol kutoa mimba, unapaswa kuzingatia mambo yafuatayo kwa usalama wako;
Ikiwa damu inaendelea kutoka kwa zaidi ya wiki 2 kwa kiasi kikubwa sana, au unapata homa, maumivu makali yasiyopungua, au harufu mbaya kutoka ukeni, unapaswa kumuona daktari mara moja.
Ikiwa huna damu yoyote ndani ya masaa 24 baada ya kutumia Misoprostol, inaweza kuwa ishara ya utoaji mimba usiofanikiwa.
Rejea za mada hii
ULY CLINIC. Kutokwa damu baada ya kutoa mimba kwa dawa https://www.ulyclinic.com/foramu/majadiliano-na-wataalamu/kutokwa-damu-baada-ya-kutoa-mimba-kwa-dawa. Imechukuliwa 15.03.2025
Uptodate. Patient education: Abortion (pregnancy termination) (Beyond the Basics)https://www.uptodate.com/contents/abortion-pregnancy-termination-beyond-the-basics/print#:. Imechukuliwa 15.03.2025
How long do you bleed after an abortion?. https://www.msichoices.org.uk/news/how-long-do-you-bleed-after-an-abortion/. Imechukuliwa 15.03.2025
NCBI. POST-ABORTION. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK190099/. Imechukuliwa 15.03.2025
ULY CLINIC. Misoprostol. https://www.ulyclinic.com/dawa/misoprostol-. Imechukuliwa 15.03.2025