Swali la msingi
Doctor habari za leo, nina umri wa miaka 27 nina tatizo uwa napitia nikiwa nashiriki tendo la ndoa nikimaliza round ya 1 uume ausimami tena na wala sipati hisia ata kidogo tatizo ni nini?
Majibu

Asante kwa kuleta swali hili la kiafya, ambalo ni la muhimu na linaweza kumsaidia mtu yeyote anayepitia hali kama hiyo. Kwa maelezo yako.
Ni hali ya kawaida kabisa kwa wanaume kupitia tatizo la kutopata tena msisimko wa kimapenzi mara baada ya kumaliza tendo la ndoa (bao la kwanza). Hali hii kitaalamu inajulikana kama muda wa mapumziko baada ya kufika kileleni ambapo mwili wa mwanaume hupumzika kabla ya kurudia tendo lingine la ndoa. Muda huu hutofautiana kwa kila mtu kulingana na afya ya mwili, umri, msisimko wa kihisia, na hali ya maisha kwa ujumla. Kkwa kawaida kwa wanaume vijana huweza kuchukua muda wa dakika chache hadi 30 na wanaume watu wazima zaidi(wazee) muda wa wa saa moja hadi siku nzima.
Kwa mwanaume mwenye umri wa miaka 27, mara nyingi uwezo wa kufanya tendo la ndoa zaidi ya mara moja kwa usiku huwa bado upo, hasa kama mwili na akili viko katika hali nzuri. Hata hivyo, kuna sababu mbalimbali zinazoweza kuchangia tatizo hili kuonekana mapema au kuendelea kwa muda mrefu. Ili kuelewa vizuri, ni muhimu kuchunguza kwa makini visababishi kabla ya kufikiria matibabu au msaada wa kitaalamu.
Visababishi mapumziko marefu zaidi baada ya kufika kileleni
Msongo wa mawazo na wasiwasi: Hali ya akili inapokuwa na hofu au mawazo mengi, uzalishaji wa homoni za raha hupungua na hivyo kupunguza hamu ya tendo la ndoa na uwezo wa kusimamisha uume.
Kuchoka kimwili au kisaikolojia: Kama mwili umechoka kutokana na kazi nyingi au usingizi hafifu, uwezo wa mwili kuitikia msisimko wa kimapenzi hupungua.
Kiwango cha chini cha homoni ya testosteroni: Testosteroni ni homoni ya kiume inayochochea hamu ya tendo la ndoa. Kiwango cha chini kinaweza kusababisha kupungua kwa nguvu za kiume kunakoambatana na kukosa hamu pamoja na kutosimama kirahisi kwa uume.
Lishe duni na kutofanya mazoezi: Mwili usipopata virutubisho sahihi na kutopata mazoezi ya kutosha, mzunguko wa damu kwenda kwenye uume unaweza kuwa hafifu, hali inayoweza kusababisha tatizo la nguvu za kiume.
Matumizi ya pombe na sigara: Hivi huathiri mishipa ya damu na kupunguza uwezo wa kusimamisha uume vizuri, hasa kwa mara ya pili baada ya tendo la kwanza.
Magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu, au magonjwa ya moyo: Haya huathiri mishipa ya damu na mfumo wa neva unaohusika katika msisimko wa tendo la ndoa.
Kutokuwepo kwa mawasiliano mazuri na mwenza: Mahusiano yenye migogoro, hofu ya kushindwa kurudia tendo, au ukosefu wa ushirikiano kati ya wapenzi unaweza kuathiri utendaji wa kimapenzi.
Ufanye nini kupunguza muda wa mapumziko baada ya kufika kileleni?
Baadhi ya mambo unaweza kuyafanyali kupunguza muda wa mapumziko baad aya kufika kileleni ni kama yafuatayo;
Mazoezi ya moyo na nguvu (kama riadha, kusimama na kuchuchumaa) na mazoezi ya sakafu ya nyonga.
Lishe yenye protini, zinc, na vyakula vya kuongeza mzunguko wa damu (kama parachichi, karanga, mayai, tikiti maji, asali)
Kuwasiliana kwa karibu zaidi na mwenza, mapenzi hayaanzi tu kwenye kitanda, bali kwenye ukaribu wa kila siku.
Kuepuka kujichua kupita kiasi, kwani kunaweza kupunguza hisia halisi wakati wa tendo.
Kupata mapumziko ya kutosha, usingizi duni unaua kabisa nguvu za tendo la ndoa.
Kuondoa msongo wa mawazo kupitia tafakuri, mazoezi ya kupumua au kushiriki shughuli unazozifurahia.
Kuepuka pombe na sigara, au punguza kwa kiasi kikubwa.
Je, ni lazima kumwona daktari?
Ndiyo. Ikiwa hali hii inaendelea kwa zaidi ya miezi mitatu, au imeanza ghafla bila sababu inayoeleweka, ni vyema kumwona daktari wa afya ya uzazi au daktari wa magonjwa ya ndani. Daktari anaweza kupendekeza vipimo vya:
Kiwango cha testosteroni
Sukari ya damu
Shinikizo la damu
Vipimo vya figo, ini, au mfumo wa neva
Matibabu
Matibabu hutegemea chanzo kilichogundulika. Wakati mwingine, ushauri wa kisaikolojia pia unaweza kusaidia ikiwa chanzo ni matatizo ya kiakili au ya mahusiano.
Rejea za mada hii:
La Torre A, Giupponi G, Conca A, Gormez A, Fabbri A. Erectile dysfunction and refractory period: the role of prolactin. J Endocrinol Invest. 2021;44(5):967–974.
Carani C, Isidori AM, Granata AR, et al. Multicenter study on the prevalence of sexual symptoms in male hypo- and hypergonadism. J Clin Endocrinol Metab. 2005;90(2):647–655.
Corona G, Ricca V, Bandini E, et al. Selective serotonin reuptake inhibitor-induced sexual dysfunction. J Sex Med. 2009;6(5):1259–1269.
Feldman HA, Goldstein I, Hatzichristou DG, Krane RJ, McKinlay JB. Impotence and its medical and psychosocial correlates: results of the Massachusetts Male Aging Study. J Urol. 1994;151(1):54–61.
Rosen RC, Wing R, Schneider S, Gendrano N. Epidemiology of erectile dysfunction: the role of psychosocial factors. J Urol. 2000;163(5):1712–1719.
Shabsigh R. The effects of testosterone on the cavernous tissue and erectile function. World J Urol. 2003;21(5):346–351.
Ismail SB, Wan Mohammad WMZ, George A, Nik Hussain NH. The effect of exercise on erectile function: a review of literature. Asian J Androl. 2020;22(6):538–545.