Swali la mzingi
Daktari habari za jioni, nilivyomaliza hedhi nimetokwa vipele mithili ya kuungua vinamuwasho sana shida ni nini?
Majibu
Vipele vinavyofanana na malengelenge vinavyoambatana na muwasho baada ya hedhi vinaweza kusababishwa na sababu mbalimbali za kiafya, ikiwa ni pamoja na;

Maambukizi ya kirusi Herpes Simplex sehemu za siri
Maambukizi haya huambatana na dalili ya malengelenge (kama ya kuungua) kuwashwa, kuhisi maumivu au mwasho mkali, na wakati mwingine homa.
Maambukizi ya fangasi
Maambukizi ya fangasi ukeni yanaweza kusababisha muwasho, wekundu, na vipele vidogo. Hutokea mara nyingi baada ya hedhi kutokana na mabadiliko ya homoni na unyevunyevu ukeni.
Mzio wa ngozi wa mguzo
Sababu inaweza kuwa matumizi ya pedi, sabuni, au viosheo vyenye kemikali kali. Dalili zinaweza kuwa kutokewa na vipele vidogo vinavyowasha sana.
Maambukizi ya bakteria ukeni
Kama ni vipele vyekundu vyenye usaha, huenda ni dalili za maambukizi ya ngozi kama folikulaitiz (maambukizi ya vinyweleo vya nywele). Husababishwa na bakteria kama Staphylococcus aureus.
Magonjwa ya ngozi
Magonjwa kama Izima(pumu ya ngozi) au soriasis yanaweza kusababisha vipele vyenye muwasho hasa baada ya hedhi.
Mambo ya kuzingatia?
Endapo unatokwa na vipele baada ya hedhi, ni muhimu kuzingatia mambo yafuatayo ili kutozidisha na kutatua tatizo;
Usijikune ili kuepuka kueneza au kuchochea zaidi hali hiyo.
Epuka sabuni au kemikali kali zinazoweza kuongeza muwasho.
Vaa nguo safi, zisizobana, na za pamba.
Kama kuna maumivu makali, homa, au usaha, ni vyema kumuona daktari kwa uchunguzi na matibabu sahihi.
Maelezo ya ziada yanayohitajika
Wakati una swali hili, kumbuka kutoa maelezo kuhusu maswali yafuatayo katika sehemu ya maoni ya mada hii ili kujibiwa;
Je, unakumbuka kama umewahi kuwa na hali hii hapo awali?
Je, kuna mabadiliko ya bidhaa unazotumia (kama pedi au sabuni)?
Rejea za mada hii
Gupta, R., Warren, T., & Wald, A. (2007). Genital herpes. The Lancet, 370(9605), 2127-2137.
Sobel, J. D. (2007). Vulvovaginal candidosis. The Lancet, 369(9577), 1961-1971.
Warshaw, E. M., Buchholz, H. J., Belsito, D. V., et al. (2008). Allergic contact dermatitis in health care workers. Journal of the American Academy of Dermatology, 58(1), 1-12.
Levy, S. B., & Marshall, B. (2004). Antibacterial resistance worldwide: causes, challenges and responses. Nature Medicine, 10(12), S122-S129.