top of page

Magonjwa

Public·783 members

Tetekuwanga

Tetekuwanga ni ugonjwa unaosababshwa na kirusi Varicella zoster AU kirusi tetekuwanga. Ugonjwa huu husababisha harara ndogo na malenge kwenye ngozi yanayoambatana na muwasho.


Dalili za tetekuwanga

Tetekuwanga huonekana siku 10 hadi 21 baada ya kupata maambukizi. Dalili kuu ya ugonjwa huu huwa ni malengelenge madogo yanayowasha na hudumu kwa muda wa siku 5 hadi 10. Dalili zingine zinazoonekana siku 1 hadi 2 kabla ya kuona vipele ni;

  • Homa

  • Kukosa hamu ya kula

  • Maumivu ya kichwa

  • Kuchoka

  • Hali ya kuhisi haupo sawa


Hatua za dalili za harara

Mara baada ya vipele kutokea kwenye ngozi hupitia hatua tatu;

  • Vipele vidogo ambavyo hupasuka siku chache baadae

  • Malenge madogo yanayotokea siku moja kisha kupasuka

  • Magamba yanayofunika malenge yaliyopasuka na huchukua siku chache kupona


Vipele vipya huendelea kuonekana kila baada ya siku kadhaa, hivyo mgonjwa anaweza kuwa na vipele, malenge na magamba kwa wakati mmoja.


Maambukizi na kusambaza kwa tetekuwanga

Masaa 48 kabla ya kuonyesha dalili, unaweza kuambukiza watu wengine ugonjwa huu na utaendelea kuambukiza mpaka pale vipele vinapotengeneza magamba.

Ugonjwa huu husambaa kirahisi sana kwa watu ambao hawajapata chanjo ya virusi hivi na ugonjwa unaweza kuathiri watu wengi kwa wakati mmoja. Kwa sasa chanjo inawalinda watoto dhidi ya maambukizi haya.


Njia za kusambaa kwa ugonjwa ni pamoja na;

  • Kugusana na majimaji ya kikohozi au chafya

  • Kushika kitu chenye virusi( Vitu ambavyo vimetumiwa na mgonjwa) kama nguo, vyombo n.k

  • Kushika malengelege ya mgonjwa au mkanda wa jeshi


Ukali wa ugonjwa

Ugonjwa mara nyingi huwa wa kiasi kwa watoto wenye afya njema. Hata hivyo unaweza kutokea kwenye mwili mzima. Malenge huweza kutokea pia kohoni na kwenye tishu za ndani ya yurethra, njia ya haja kubwa na tundu la uke.


Wakati gani wa kumwona daktari

Kama unafikiria kuwa mwanao ana tetekuwanga, wasiliana na daktari wako mara moja. Mara nyingi ugonjwa huu hutambulika kwa dalili na viashiria tu zinazoonekana kwenye mwili wa mtu. Unaweza kuhitaji dawa za kusaidia kupunguza uzalianaji wa virusi au kitibiwa shida zingine ambazo zinasababishwa na tetekuwanga. Ili kuepuka kuambukiza watu wengine, unaweza kupatiwa matibabu nyumbani.


Nini ufanye unapowasiliana na daktari

Kabla ya kuwasiliana na daktari hakikisha unamweleza

  • Kama upele unasambaa kwenye macho

  • Kama upele unakuwa wa moto au kuuma

  • Kama unaishi na watu ambao hawakupata chanjo ya ugonjwa

  • Kama kuna mjamzito ndani ya nyumba

  • Kama unaishi na mtu anayetumia dawa zinazoshusha kinga ya mwili


Vihatarishi vya kupata ugonjwa wa tetekuwanga

Vifuatavyo ni vihararishi vya kupata ugonjwa wa tetekuwanga

  • Kutopata chanjo ya ugonjwa

  • Kutougua tetekuwanga kabla


Kama umepata chanjo au ulishawahi ugua ugonjwa huu, kama ukipata tena ugonjwa utakuwa na dalili za wastani za kuwa na malenge machache, hata hivyo ni mara chache kupata ugonjwa kwa mara nyingine.


Madhara tetekuwanga

Tetekuwanga mara nyingi ni ugonjwa unaosababisha dalili za wastani. Hata hivyo unaweza kuwa mkali na kupelekea matatizo mengine ya kiafya kama;

  • Maambukizi kwenye ngozi, mifupa na damu yanayosababishwa na bakteria

  • Kuishiwa maji mwilini

  • Nimonia na magonjwa mengine ya mapafu

  • Kuvimba kwa ubongo

  • Sindromu ya sumu kutokana na bakteria

  • Ugonjwa wa Reyes kama mtoto akipewa aspirini

  • Kifo kwa nadra sana


Nani yupo kwenye hatari ya kupata tetekuwanga?

Watu waliohatarini kupata madhara ya tetekuwanga ni kama wafuatao;

  • Vichanga na watoto chini ya umri wa mwaka mmoja ambao hawajapata chanjo

  • Vijana wa umri wa miaka 11 hadi 19 na watu wazima

  • Wajawazito ambao hawakuwahi kuugua tetekuwanga

  • Wavuta sigara

  • Wagonjwa wa saratani au UKIMWI au wanaotumia dawa za kushusha kinga ya mwili

  • Wagonjwa wenye magonjwa sugu kama pumu, wanaotumia dawa za kushusha kinga ya mwili, au waliofanyiwa upandikizaji wa ogani mwilini na kutumia dawa za kushusha kinga ya mwili.

Kinga ya tetekuwanga

Kupata chanjo ya kirusi cha tetekuwanga ni njia nzuri ya kujikinga na ugonjwa na hata kama ukipata kwa mara nyingine ugonjwa hautakuwa mkali.


Utambuzi wa tetekuwanga

Mara nyingi htuambuliwa kwa dalili na viashiria vinavyoonekana kwenye mwili wa mtoto kwa kuangalia.


Matibabu ya tetekuwanga

Ugonjwa huu mara nyingi hauhitaji tiba kwa watoto wenye afya njema. Baadhi ya watoto wanaweza kupewa dawa za kupunguza mzio ili kupunguza dalili ya muwasho. Hata hivyo mara nyingi matibabu hayahitajiki na ugonjwa unabidi uendelee na kuisha wenyewe.


Matibabu kwa watu wenye hatari ya madhara

Kwa waliohatarini kupata madhara ya ugonjwa kama vile watu wenye upungufu wa kinga kutokana na sababu yoyote wanaweza kuhitaji matibabu ya dawa za kupunguza makali ya kirusi cha tetekuwanga. Dawa zinazotumika mara nyingi huwa ni acyclovir (Zovirax, Sitavig). Hufanya kazi vema kama zikitumika madaa 24 baada ya kuona harara kwa mara ya kwanza.


Dawa valacyclovir (Valtrex) na famciclovir, huweza kupunguza ukali wa ugonjwa pia, hata hivyo zinaweza zisiwe sahihi kwa kila mtu. Unaweza kushauriwa kupata chanjo pia kama itaonekana inafaa kuzuia hatari ya maambukizi mengine.


Matibabu ya nyumbani ya tetekuwanga

Unaweza kufanya mambo yafuatayo kudhibiti dalili za tetekuwanga nyumbani.

Acha kujikuna- kujikuna hupunguza kasi ya kupona na kuongeza hatari ya vidonda sambamba na maambukizi ya bakteria kwenye damu.

Punguza muwasho na homa kwa kufanya mambo yafuatayo:

  • Kuoga maji ya baridi yaliyotiwa magadisoda, aluminum acetate au shayiri

  • Kupaka losheni kalamine kwenye eneo linalowasha

  • Kutumia dawa za kupunguza mzio kama diphenhydramine (Benadryl)- wasiliana na daktari kwanza.

  • Kutumia parasetamol kwa ajili ya homa

  • Ongea na daktari wako kama unaweza kutumia dawa zingine kama ibuprofen (Advil, Motrin IB) n.k


Rejea za mada hii

  1. Centers for Disease Control and Prevention. Chickenpox (varicella). https://www.cdc.gov/chickenpox/about/index.html. Imechukuliwa 23.10.2024

  2. Centers for Disease Control and Prevention. Chickenpox (varicella): Vaccination. https://www.cdc.gov/chickenpox/vaccination.html. Imechukuliwa 23.10.2024

  3. Chickenpox. Newyork state. https://www.health.ny.gov/diseases/communicable/chickenpox/fact_sheet.htm#:. Imechukuliwa 23.10.2024

  4. Centers for Disease Control and Prevention. Chickenpox (varicella): Prevention and treatment. https://www.cdc.gov/chickenpox/about/prevention-treatment.html. Imechukuliwa 23.10.2024

  5. Centers for Disease Control and Prevention. Guidelines for vaccinating pregnant women. https://www.cdc.gov/vaccines/pregnancy/hcp-toolkit/guidelines.html. Imechukuliwa 23.10.2024

  6. Centers for Disease Control and Prevention. Shingles vaccination. https://www.cdc.gov/vaccines/vpd/shingles/public/shingrix/index.html. Imechukuliwa 23.10.2024

  7. Centers for Disease Control and Prevention. Types of chickenpox vaccine. https://www.cdc.gov/vaccines/vpd/varicella/public/index.html. Imechukuliwa 23.10.2024

  8. Centers for Disease Control and Prevention. Varicella (chickenpox). In: CDC Yellowbook 2018: Health Information for International Travel. New York, N.Y.: Oxford University Press; 2018. http://global.oup.com/. Imechukuliwa 23.10.2024

  9. Chickenpox vaccination: What everyone should know. https://www.cdc.gov/vaccines/vpd/varicella/public/index.html. Imechukuliwa 23.10.2024

  10. Longo DL, et al., eds. Varicella-zoster virus infections. In: Harrison's Principles of Internal Medicine. 20th ed. New York, N.Y.: The McGraw-Hill Companies; 2018. https://accessmedicine.mhmedical.com. Imechukuliwa 23.10.2024

  11. Merck Manual Professional Version. Chickenpox (varicella). https://www.merckmanuals.com/professional/infectious-diseases/herpesviruses/chickenpox. Imechukuliwa 23.10.2024

  12. Papadakis MA, et al., eds. Viral and rickettsial infections. In: Current Medical Diagnosis & Treatment 2019. 58th ed. New York, N.Y.: McGraw-Hill Education; 2019. https://accessmedicine.mhmedical.com. Imechukuliwa 23.10.2024

  13. ULY CLINIC. Kirusi variella zoster. https://www.ulyclinic.com/virusi/kirusi-varicella-zosta. Imechukuliwa 23.10.2024

15 Views

About

Sehemu ambayo imeandikwa magonjwa mbalimbali yanayowapata bi...

bottom of page