top of page

Majadiliano na Wataalamu

Public·804 members

Dalili za UKIMWI kwenye ngozi

Dalili za UKIMWI kwenye ngozi

Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) huathiri moja kwa moja mfumo wa kinga ya mwili, na kumweka mgonjwa katika hatari ya kupata magonjwa nyemelezi mbalimbali. Moja ya maeneo yanayoonyesha dalili mapema ni ngozi, ambayo hutoa viashiria muhimu vinavyoweza kusaidia kugundua ugonjwa mapema. Mabadiliko haya yanaweza kuanza kuonekana katika hatua za awali za maambukizi au baadaye pale kinga ya mwili inapopungua sana. Kupitia makala hii, tutajadili kwa undani dalili za ngozi kwa watu walioambukizwa VVU, umuhimu wake, na muda sahihi wa kutafuta huduma ya daktari.


Dalili za UKIMWI zinazoonekana kwenye ngozi

Ngozi ni kiungo kinachoathirika mapema pindi virusi vya VVU vinapoingia mwilini, hasa kwa sababu kinga ya mwili inapodhoofika, magonjwa mengi ya ngozi hupata nafasi ya kushambulia. Mabadiliko haya ya ngozi yanaweza kuwa matokeo ya virusi vyenyewe, maambukizi ya magonjwa nyemelezi, au hali sugu zinazochochewa na kinga duni ya mwili. Hapa chini tunaangazia aina mbalimbali za mabadiliko yanayoonekana kwenye ngozi kwa mtu mwenye VVU.


Visababishi vya vipele vya UKIMWI kwenye ngozi

Vipele vya ukimwi kwenye ngozi vinaweza kutokana na magonjwa yaguatayo;


1. Harara ya VVU

Hii ni moja ya dalili za awali kabisa zinazoweza kujitokeza baada ya mtu kuambukizwa VVU. Vipele hivi hutokana na mwitikio wa mwili dhidi ya virusi vipya, na huonekana siku 14 hadi 28 baada ya maambukizi mapya.

  • Huwa na vipele vidogo vyekundu au vya pinki

  • Huonekana kwenye kifua, mgongo, uso au mikono.

  • Huambatana na muwasho au kutokuwa na maumivu.

  • Mara nyingi hupotea bila matibabu ndani ya siku chache.


2. Mkanda wa jeshi

Ugonjwa wa Herpes zoster hujulikana pia kama "mkanda wa jeshi" kwa sababu ya mwelekeo wake wa kuenea upande mmoja wa mwili. Kwa mtu mwenye VVU, huashiria kuwa kinga ya mwili imedhoofika na virusi vya utotoni (varicella) vimeamshwa tena.

  • Malengelenge huambatana na maumivu na hisia ya kuchoma.

  • Huathiri upande mmoja wa mwili – hasa kifua, mgongo au uso.

  • Maumivu yanaweza kuendelea hata baada ya vipele kupona.


3. Vipele vya herpes

Vipele vya herpes ni maambukizi ya mara kwa mara kwa watu wenye kinga dhaifu. Kwa watu wenye VVU, hujitokeza mara kwa mara zaidi, ni makali, na huchukua muda mrefu kupona.

  • Hutokea kama malengelenge mdomoni au sehemu za siri

  • Hushambulia midomo, kinywa au sehemu za siri.

  • Huambatana na kuchoma, kuwashwa na kuvimba.

  • Hutokea kwa mzunguko na kuwa sugu kwa baadhi ya dawa.

4. Sunzua kwenye ngozi

Sunzua husababishwa na virusi vya HPV na mara nyingi huwa sugu kwa mtu aliye na VVU kwa sababu mwili hushindwa kupambana navyo. Sunzua hizi zinazoonekana kama mithiri ya maoteo ya vinyama vinaweza kuota sehemu yoyote ya mwili ikiwa pamoja na sehemu za siri.

  • Huonekana kama uvimbe mdogo ulioinuka.

  • Huenea kwa kasi na kuwa vigumu kutibu.

  • Maeneo yanayoathirika zaidi ni vidole, nyayo, shingo na sehemu za siri.

5. Saratani ya Kaposisi

Saratani ya Kaposi’s ni aina ya saratani inayojitokeza zaidi kwa watu wenye kinga dhaifu sana, hasa waliochelewa kuanza dawa za ARVs. Ni dalili ya maambukizi ya VVU iliyoendelea hadi hatua ya UKIMWI.

  • Mabaka ya zambarau, damu ya mzee au bluu kwenye ngozi au mdomoni.

  • Huonekana kwenye uso, miguu, mapajani au ndani ya kinywa.

  • Huweza kuenea hadi ndani ya mapafu au njia ya chakula.

6. Maambukizi ya fangasi

Maambukizi ya fangasi hujitokeza zaidi kwa watu walio na kinga dhaifu kwa sababu mwili hauna uwezo wa kudhibiti ukuaji wa fangasi wa kawaida.

  • Huambatana na muwasho, wekundu au harufu mbaya.

  • Candida ya midomo, koromeo na maeneo ya siri ni ya kawaida.

  • Fangasi wa ngozi huonekana kama duara la wekundu au ngozi kujaa ungaunga.


7. Michomokinga ya kiseboreiki kwenye ngozi

Hii ni hali ya ngozi inayosababisha ngozi kuwa na ungaunga au kuwa na mafuta kupita kiasi. Kwa watu wenye VVU, inaweza kuwa kali na sugu.

  • Huonekana usoni, kichwani au nyuma ya masikio.

  • Ngozi huwa na wekundu, muwasho au kuwa na magamba meupe.

  • Huambatana na ngozi yenye mafuta kupita kiasi.

8. Soriasis au izima au pumu ya ngozi

Hali hizi za ngozi ambazo husababishwa na mfumo wa kinga kushambulia ngozi, huwa kali zaidi kwa watu walioambukizwa VVU.

  • Mabaka mekundu, ngozi kupasuka au ngozi kuwa ngumu.

  • Huambatana na muwasho mkali na maumivu.

  • Huathiri sehemu mbalimbali ikiwemo mikono, magoti, na ngozi ya kichwa.


Wakati gani wa kumwona daktari?

Kama unakumbana na mabadiliko yasiyo ya kawaida kwenye ngozi yako, ni muhimu usiyapuuzie. Dalili nyingi zinaweza kutibiwa mapema na kuepusha madhara makubwa. Muda sahihi wa kumwona daktari ni:

  • Unapopata vipele au vidonda visivyopona kwa muda mrefu.

  • Dalili za ngozi kuambatana na homa, kuvimba au maumivu makali.

  • Kuona mabaka yasiyo ya kawaida rangi kama ya zambarau au damu ya mzee.

  • Kuona vipele vinavyorudia kila mara au kuwa sugu kwa matibabu ya kawaida.

  • Vidonda vya mdomoni au sehemu za siri visivyopona.


Hitimisho

Ngozi inaweza kutoa dalili muhimu kuhusu hali ya afya ya ndani ya mwili. Kwa mtu aliyeambukizwa VVU, mabadiliko ya ngozi yanaweza kuwa ishara ya kwanza ya maambukizi au kupungua kwa kinga. Elimu sahihi, utambuzi wa mapema, na matibabu ya haraka vinaweza kusaidia kudhibiti hali hizi na kuboresha maisha ya mgonjwa. Ni muhimu kufuatilia mabadiliko yoyote ya ngozi na kupata ushauri wa kitaalamu.


Rejea za mada hii;

  1. Havlir DV, Currier JS. HIV infection in adults. N Engl J Med. 2010;362(9):846–58.

  2. Bolognia JL, Schaffer JV, Cerroni L. Dermatology. 4th ed. Elsevier; 2018.

  3. Tchernev G, et al. Kaposi’s sarcoma: diagnostic and therapeutic challenges. Wien Med Wochenschr. 2013;163(21–22):493–8.

  4. Deeks SG, Lewin SR, Havlir DV. The end of AIDS: HIV infection as a chronic disease. Lancet. 2013;382(9903):1525–33.

  5. Koenig HC, et al. Skin conditions in HIV infection. HIV Curriculum for the Health Professional. UCSF; 2021.

  6. WHO. HIV and skin diseases. World Health Organization. 2023.

30 Views

Kuhusu kundi

Uliza swali pamoja na kusoma majibu ya maswali yaliyoulizwa,...

bottom of page