Hedhi baada ya kufunga kizazi

Swali la msingi
Je, mwanamke alie funga kizazi kwa njia ya ku katwa mirija anaweza kuona siku zake ?
Majibu
Ndiyo, mwanamke aliyefunga kizazi kwa njia ya kukatwa mirija ya uzazi (tubal ligation) anaweza kuendelea kuona siku zake (hedhi) kama kawaida. Nitakujibu swali lako kwa kina hapa chini
Kufunga kizazi ni nini?
Ni njia ya kudumu ya uzazi wa mpango ambayo hufanyika kwa hiari ya mwanamke anayetaka kutozaa tena.. Hufanyika kwa upasuaji unaojumuisha mchakato wa kukata, kufunga au kuziba mirija ya fallopian ili kuzuia yai kukutana na mbegu ya kiume.
Kwa nini anaendelea kuona siku zake?
Hii ni kwasababu zifuatazo:
Kukata mirija hakuathiri ovari, ambazo ndizo zinatoa mayai na homoni estrojeni na progesteroni zinazodhibiti mzunguko wa hedhi.
Mzunguko wa hedhi huendelea kama kawaida kwa sababu mwili unaendelea kuzalisha homoni
Yai hutolewa kila mwezi kama kawaida, lakini haliwezi tena kupita kwenda kwenye mfuko wa uzazi. Ingawa yai haliwezi tena kufika kwenyekizazi,ukuta wa kizazi bado hujengeka na kuanguka kama kawaida, jambo linalosababisha hedhi.
Sababu zinazoweza kuathiri hedhi baada ya kufunga kizazi
Kukoma hedhi kwa sababu ya umri
Mabadiliko ya homoni au afya ya mwili kwa ujumla
Mimba nje ya kizazi – Japo ni nadra sana , mimba inaweza kutokea nje ya mfuko wa uzazi, hata baada ya kufunga kizazi.
Nifanye nini kama sioni eedhi baada ya kufunga kizazi?
Ukiona umeacha kuona siku zako baada ya kufunga kizazi:
Usihofie haraka, inaweza kuwa ni mabadiliko ya kawaida ya homoni.
Fanya kipimo cha ujauzito, hata kama ni nadra ni bora kuhakikisha.
Muone daktari kwa uchunguzi zaidi kama hali itaendelea.
Hitimisho
Kufunga kizazi hakumaanishi kuacha kuona hedhi. Mwanamke ataendelea kuwa na mzunguko wa kawaida kwa sababu homoni zake bado zinafanya kazi. Kama kuna mabadiliko yoyote yasiyo ya kawaida, ni vyema kushauriana na daktari kwa usalama zaidi.
Rejea za mada hii:
American College of Obstetricians and Gynecologists. (2021). Sterilization for women and men. https://www.acog.org/womens-health/faqs/sterilization-for-women-and-men. Imechukuliwa 16.04.2025
Mayo Clinic. (2022). Tubal ligation: Permanent birth control. https://www.mayoclinic.org/tests-procedures/tubal-ligation/about/pac-20388360. Imechukuliwa 16.04.2025
World Health Organization. (2018). Family planning: A global handbook for providers (2018 update). https://www.who.int/publications/i/item/9780999203705. Imechukuliwa 16.04.2025
Hatcher, R. A., Nelson, A. L., Trussell, J., Cwiak, C., Cason, P., & Policar, M. S. (2018). Contraceptive technology (21st ed.). Ayer Company Publishers.