Kutokwa matone ya damu kunakoambatana na maumivu ya kujirudia ya tumbo la uzazi: Visababishi
Swali la msingi
Daktari habari, mimi ni binti wa umri wa miaka 21, sipo kwenye hedhi, swali langu ni tumbo la uzazi kuuma na kuacha na damu kutoka kitone na kuacha ni dalili za nini?
Majibu

Habari yako dada, na asante kwa kuuliza swali la kiafya. Maelezo yako yanaonyesha kuwa:
Una miaka 21
Haupo kwenye hedhi kwa sasa
Lakini unapata maumivu ya tumbo la uzazi yanayoanza na kuacha
Na pia kuna kutoka kwa damu kidogo (kitone), halafu inaacha
Hali hii inaweza kusababishwa na mambo kadhaa yanayoweza kuwa hali ya kawaida au inayohitaji uchunguzi wa haraka. Hebu tuangalie baadhi ya sababu zinazowezekana;
Baadhi ya visababishi vya dalili ulizonazo
1. Kuwa kwenye kipindi cha uovuleshaji
Hili ni tukio la kawaida katikati ya mzunguko wa hedhi, ambapo yai hutolewa kutoka kwenye ovari. Huweza kuambatana na maumivu madogo upande mmoja wa tumbo na damu kidogo sana (matone). Kuonekana kwa dalili hii wakati huu ni kawaida kabisa, hasa kwa wasichana wadogo au walioko katika umri wa uzazi.
2. Mabadiliko ya homoni
Mabadiliko kidogo ya homoni yanaweza kuleta maumivu ya tumbo na kutokwa na matone ya dmau, hasa kama:
Umepitiliza muda wa hedhi
Unatumia au umeacha kutumia vidonge vya uzazi wa mpango
Umehangaika na msongo wa mawazo au uzito kubadilika ghafla
3. Maambukizi ya njia ya uzazi au magonjwa ya zinaa
Kama una maumivu ya tumbo ya mara kwa mara na damu isiyo ya kawaida, inaweza kuwa ni ishara ya maambukizi kwenye mfumo wa uzazi aua magonjwa ya zinaa. Dalili zingine zinazoweza kuambatana ni pamoja na;
Harufu mbaya ukeni
Uchafu usio wa kawaida
Homa au maumivu wakati wa tendo la ndoa
4. Kuwa na mimba changa au mimba nje ya mfuko wa uzazi
Kama kuna uwezekano wa mimba, damu kidogo na maumivu ya tumbo vinaweza kuwa ishara ya;
Ishara ya kujipandikiza kwa kiinitete kwenye mji wa mimba
Ujauzito kutungwa nje ya mfuko wa uzazi. Hali hii ni ya dharura ya kitabibu ikiwa maumivu ni makali upande mmoja na unatokwa na damu
5. Ugonjwa wa vifuko maji kwenye mayai
Wakati mwingine kuna vivimbe maji vidogo kwenye ovari vinavyopasuka na kutoa damu kidogo. Hii husababisha maumivu makali ya muda mfupi yanayoweza kuambatana na kutokwa na matone ya damu ukeni.
Nini unapaswa kufanya sasa?
Fanya kipimo cha ujauzito ikiwa umewahi kushiriki ngono bila kinga
Tembelea kituo cha afya kwa uchunguzi wa kitaalamu kama kipimo cha uchunguzi wa uke, ultrasound na vipimo vya maambukizi
Rekodi mzunguko wako wa hedhi na mabadiliko yanayotokea katika tarehe hizo ili kuona kama ni wa kujirudia rudia ili kumshirikisha daktari wako.
Wakati gani wa kuwasiliana na daktari haraka?
Mara nyingi dalili unayopata huwa haisababishwi na hali za dharura, hata hivyo kama zinaambatana na maumivu makali, homa, kichefuchefu, au kutokwa na damu nyingi usichelewe kwenda hospitali haraka kwa matibabu.
Rejea za mada hii:
Speroff L, Fritz MA. Clinical Gynecologic Endocrinology and Infertility. 8th ed. Philadelphia: Lippincott Williams & Wilkins; 2011.
Hatcher RA, Trussell J, Nelson AL, Cates W, Kowal D, Policar MS. Contraceptive Technology. 20th rev. ed. New York: Ardent Media; 2011.
American College of Obstetricians and Gynecologists. Management of acute abnormal uterine bleeding in nonpregnant reproductive-aged women. Obstet Gynecol. 2013;121(4):891–6.
Cunningham FG, Leveno KJ, Bloom SL, Dashe JS, Hoffman BL, Casey BM, et al. Williams Obstetrics. 25th ed. New York: McGraw-Hill Education; 2018.
Ankum WM, Mol BW, Van der Veen F, Bossuyt PM. Risk factors for ectopic pregnancy: a meta-analysis. Fertil Steril. 1996;65(6):1093–9.
Workowski KA, Bolan GA. Sexually transmitted diseases treatment guidelines, 2015. MMWR Recomm Rep. 2015;64(RR-03):1–137.