Mwandishi;
Mhariri:
Jaza jina na cheo cha mwandishi
Alhamisi, 22 Aprili 2021
Kumwagikiwa na kemikali machoni- Huduma ya kwanza
Kumwagikiwa na kemikali kwenye macho inapaswa kuchukuliwa kama tukio la kupata matibabu ya dharura na endapo hatua zisipochukuliwa mapema, inaweza pelekea kuharibika kwa umbo la jicho/macho, matatizo ya uono, ukavu, presha na hata upofu wa macho. Ukubwa wa jeraha na athari zinazoweza kujitokeza hutegemea aina ya kemikali, kiwango kilichomwagikia na muda wa kemikali kuwa katika jicho/macho.
Majeraha ya macho yatokanayo na kemikali yanakadiriwa kufikia asilimia 11.5 hadi -22.1,wanaume na watoto chini ya miaka 10 wapo katika hatari zaidi ya kupata majeraha ya macho yatokanayo na kemikali ukilinganisha na wanawake.
Asilimia kubwa ya ajali ya kumwagikiwa na kemikali machoni hutokea katika maeneo ya kazi hasa viwandani ukilinganisha na nyumbani. Kumwagikiwa na kemikali za alikali hutokea zaidi kuliko tindikali kwa sababu bidhaa nyingi zitumikazo majumbani , shughuli za kilimo na viwandani huwa na alikali na husababisha majeraha mabaya na athari kubwa.
Kemikali zinazoweza kuleta majeraha na athari nyingine kwenye macho
Kemikali zinazoweza kuleta majeraha na athari nyingine kwenye macho zipo katika makundi mawili ambayo ni;
Kemikali zenye alikali
Kemikali zenye tindikali
Kemikali zenye alikali
Hizi ni hatari sana kwasababu zinapoingia kwenye jicho hupenya hadi sehemu za ndani ya jicho.
Kemikali hizi ni zinahusisha ammonia hydroxide, potassium hydroxide, magnesium hydroxide, lye na lime. Kemikali zenye alikali hupatikana kwa kiwango kidogo kwenye bidhaa nyingi za usafi, mbolea, dawa za kuulia wadudu, plasta, simenti nk.
Kemikali zenye tindikali
Hizi hazina uwezo wa kupenya hadi sehemu za ndani za jicho, majeraha huishia sehemu ya nje ya jicho kwahiyo huwa na athari ndogo isipokua kemikali ya hydrofluoric acid yenye uwezo wa kupenya kama kemikali za alikali.
Kemikali hizi ni sulfuric acid, hydrochloric acid, chromic acid, na hydrofluoric acid. Hupatikana kwa kiwango kidogo kwenye rangi za glasi, bidhaa za kufutia rangi ya kucha, siki, maji ya betri nk.
Dalili na viashiria vya kuumia kwa jicho baada ya kumwagikiwa na kemikali
Kuumia kwa jicho hutokea ndani ya dakika tano baada ya kumwagikiwa na kemikali hizi. Dalili na viashiria hutegemea aina na kiwango cha kemikali pia muda ambao kemikali imeingia machoni. Dalili hizo zinajumuisha;
Hisia za macho kuungua
Hisia za mchanga machoni
Kushindwa kufumbua jicho
Kutokwa na machozi
Maumivu ya jicho
Jicho kuwa jekundu
Kupungua kwa uono(kutokuona vizuri)
Kuvimba kwa jicho
Namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa mtu aliyemwagikiwa na kemikali machoni
Lengo la kutoa huduma ya kwanza ni kupunguza muda na kiwango cha kemikali katika macho. Baada ya kumwagikiwa na kemikali fanya yafuatayo;
Safisha jicho kwa maji safi
Ili kemikali itoke katika jicho kwa haraka tumia maji mengi yanayotiririka, ni vema zaidi kutumia maji yanayotiririka katika bomba kwa muda wa dakika 10-20 .
Maeneo ya kazi hasa viwandani huwa kuna sehemu maalumu ya maji kwa ajili ya ajali za kumwagikiwa na kemikali, upatapo ajali fika eneo hilo kwa huduma ya kwanza.
Endapo ajali imetokea nyumbani fumbua jicho lililo athirika na ulishike kwa vidole sehemu ya juu na chini kwenye kope kisha inama kwenye bomba kuruhusu maji yatiririke vema kwenye jicho lako. Hakikisha maji hayavuki upande wa jicho ambalo halijaathirika. Ikiwa macho yote yameathirika unaweza kuruhusu maji kutiririka pande zote kwa wakati mmoja. Unaweza kutumia maziwa au soda kama mbadala wa maji
Nawa mikono
Nawa mikono yako kwa maji na sabuni, hii itakusaidia kuzuia kusambaa kwa kemikali sehemu nyingine za mwili.
Acha kufikicha jicho
Haishauriwi kufikicha macho hata baada ya kusafisha na maji
Usitoe lenzi ya kupachika jichoni kabla ya kusafisha kwa maji
Toa pale ambapo umejiridhisha kuwa umesafisha macho kwa maji mengi na muda wa kutosha
Nenda kituo cha afya kilicho karibu nawe
Japokua baada ya kusafisha vizuri jicho kwa maji kemikali huisha, ni vema kwenda kituo cha afya kwa msaada zaidi hasa ikiwa kemikali hiyo ilikua ni alikali au hydrofluoric acid na imemwagika kwenye jicho kwa kiwango kikubwa.Unaweza kuandika jina au kubeba kemikali hiyo kwa ajili ya kumuonesha muhudumu wa afya.
Kumbuka
Kutumia vifaa vya kujikinga na ajali za kumwagikiwa na kemikali uwapo kazini
Kuweka kemikali zote na bidhaa za nyumbani zenye kemikali mbali na watoto
ULY CLINIC inakukumbusha siku zote uwasiliane na daktari wako kwa elimu na ushauri zaidi kabla ya kuchukua thatua yoyote baada ya kusoma makala hii
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa suhauri zaidi kupitia namba za simu au kwa kubonyeza 'Pata tiba' chini ya tovuti hii
Imeboreshwa,
1 Oktoba 2021, 08:12:08
Rejea za mada:
Tahra AlMahmoud, MD, et al. Epidemiology of eye injuries in a high-income developing country An observational study. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC6617434/. Imechukuliwa 20.04.2021
Clare, G., et al, Amniotic membrane transplantation for acute ocular burns. Cochrane database of systematic reviews, 2012. 9: p. CD009379. Imechukuliwa 20.04.2021
Dubey A, et al. Clinical profile & visual outcome in ocular chemical injury. https://opthalmology.medresearch.in/index.php/jooo/article/view/57/106. Imechukuliwa 20.04.2021
Web Md. Chemical Eye Burns. https://www.webmd.com/eye-health/chemical-eye-burns. Imechukuliwa 20.04.2021
Myhealth1st. Common Household Eye Injuries and How to Avoid Them. https://www.myhealth1st.com.au/health-hub/articles/common-household-eye-injuries/. Imechukuliwa 20.04.2021
Chemical Injury to the Eye .https://www.health.harvard.edu/a_to_z/chemical-injury-to-the-eye-a-to-z. Imechukuliwa 20.04.2021
Eye wiki. https://eyewiki.aao.org/Chemical_(Alkali_and_Acid)_Injury_of_the_Conjunctiva_and_Cornea. Imechukuliwa 20.04.2021
Mayo clinic. First aid eye emergency. https://www.mayoclinic.org/first-aid/first-aid-eye-emergency/basics/art-20056647. Imechukuliwa 20.04.2021
Emedicine. Ophthalmologic Approach to Chemical Burns. https://emedicine.medscape.com/article/1215950-overview#a2https://emedicine.medscape.com/article/1215950-overview#a2. Imechukuliwa 20.04.2021