Shinikizo la kifafa cha mimba
Imeandikwa na ULY CLINIC
​
7 julai 2018
​
Preeclampsia au kwa jina jingine 'Shinikizo la kifafa cha mimba' ni tatizo linalosababishwa na ujauzito na huambatana na shinikizo la juu la damu, dalili za kudhulika kwa viungo ndani ya mwili, mara nyingi huanza na figo.
Tatizo hili huonekana kuanzia wiki ya ishirini ya ujauzito kwa mwanamke ambaye shinikizo lake la damu lilikuwa kawaida.
Kuongezeka taratibu kwa shinikizo la damu huwa ni dalili mojawapo ya shinikizo preeclampsia, pasipo matibabu preeclampsia huweza kuleta madhara makubwa kwa mama hata kuondoa uhai wa mama au mtoto au mama na mtoto.
​
Dawa pekee ya kutibu preeclampsia ni kujifungua.
Kama utagundulika mapema zaidi kuwa una preeclampsia, wewe na dakitari mtakuwa na wakati mgumu wa kufanya maamuzi kwa sababu mtoto atakuwa bado hajakomaa kuweza kuishi kama akizaliwa lakini pia kuendeleza ujauzito kunakuweka wewe hatarini kupata madhara au kifo.
​
Dalili za preeclampsia
​
Mara nyingi ugonjwa huu unaweza usionekane kwa dalili . Shinikizo la damu la juu linaweza likaongezeka polepole, lakini mara nyingi huanza ghafla wakati wa ujauzito katika kipindi baada ya wiki 20 za ujauzito. Tabia ya kupima shinikizo la damu na kudhibiti ongezeko ni sehemu ya matibabu ya kuzuia madhara mabaya ya tatizo hili.
Shinikizo la damu la 140/90mmHg au zaidi, lililopimwa mara mbili kwa nyakati yenye utofauti wa masaa 4, huitwa kuwa shinikizo la juu.
​
Kuna dalili zingine za preeclampsia
​
Ndio!
​
Dalili zingine za shinikizo la kifafa cha mimba ni
​
-
Kukojoa mkojo wenye kikubwa cha protini
-
Kupungua kwa mkojo ama mkojo kuwa na rangi tofauti
-
Maumivu makali ya kichwa
-
Kubadilika kwa uono kama vile kutoona kabisa au kuona ukungu au kuumizwa na mwanga
-
Maumivu tumbo juu ya kitovu, mara nyingi upande wa kulia kwenye mbavu
-
Maumivu ya chembe ya moyo
-
Kichefuchefu na kutapika
-
Kupungua kwa chembe sahani za damu (chembe zinazofanya damu igande)
-
Kufeli kwa ini
-
Mapafu kujaa maji kunakopelekea kushindw akupumua
Kuongezeka uzito ghafla na kuvimba sana kwenye maeneo ya uso na mikono maranyingi huambatana na preeclampsia lakini dalili hii huonekana kwenye magonjwa mengi na wakati mwingi ni kawaida kipindi cha ujauzito na hivo sio dalili ya kuashiria preeclampsia pekea yake.
Nini husababisha preeclampsia
Sababu halisi inayopelekea kusababisha tatizo hili bado haijulikani. Wanasayansi wanaamini kwamba tatizo hili huanzia kwenye kondo la nyuma ambalo hutumika kumlisha mtoto kipindi chote cha ujauzito.
Mwanzoni kabisa mwa ujauzito, mishipa mipya ya damu hutengenezwa ili kuingiza damu kwenye kodo la nyuma, wanawake wenye tatizo la preeclamsia mishipa hii huwa haitengenezwi vema. Mishipa huwa myembamba kuliko kawaida na tabia tofauti inapokutana na vichochezi mwili ambapo husababisha mishipa hii kuruhusu kiwango kidogo cha damu kupita ndani yake ili kuingia kwenye mji wa mimba
Sababu zinazosabaisha kufanyika vibaya kwa mishipa hii huwa ni
​
-
Kiwango kidogo cha damu kinachofika katika tumbo la uzazi
-
Kuharibiwa kwa mishipa ya damu
-
Tatizo la mfumo wa kinga za mwili kupambana na mwili
-
kuwa na vinasaba vinavyoambatana na ugonjwa huu
Matatizo mengine ya shinikizo la damu
​
Preeclampsia huwa moja miongoni mwa magonjwa manne yanayoambatana na matatizo ya shinikizo la damu. Magonjwa mengine ni kama
Shinikizo la damu linaloanza kwenye ujauzito
​
Wanawake wenye shinikizo la damu la juu wakati wa ujauzito wanakuwa na shinikizo hilo pasipo kuwa na protini kwenye mkojo kama wakipimwa mkojo wao, pia huwa hawana dalili za kuharibika kwa organi mojawapo mwilini.
Baadhi ya wanawake wenye shinikizo la damu la juu wakati wa ujauzito huweza kupata preeclampsia.
Shinikizo la damu sugu
​
Shinikizo la damu sugu ni lile mwanamke anakua nalo kabla ya kupata ujauzito au linalogunduliwa kabla ya wiki ya 20 ya ujauzito na liaendelea baada ya mama kujifungua mtoto.
​
Kwa sababu shinikizo la damu huwa halina dalili wakati mwingine huwa vigumu kutambua kwamba limeanza lini kwa mama kama asipofanya vipimo
Shinikizo sugu la kifafa cha mimba
​
Shinikizo hili hutokea kwa wanawake wenye tatizo sugu la shinikizo la damu la juu ambao shinikizo hilo hubadilika kuwa baya zaidi na kuonekana kwa protini kwenye mkojo baada ya kipimo au matatizo mengine ya kiafya wakati wa ujauzito
​
​
Vihatarishi vya kupata preeclampsia
​
Preeclampsia hutokea kama matokeo/madhara ya ujauzito.
Vihatarishi vyake ni kama;
​
-
Kuwa na historia ya preeclampsia-kuwa na historia kwa mama au ndugu wa tumbo moja huongeza hatari ya kupata tatizo hili kwa kiasi kikubwa
-
Ujauzito wa kwanza- hatari ya kupata tatizo hili huongezeka kwenye ujauzito wa kwanza
-
Kupata ujauzito wa mpenzi mpya- kila ujauzito unapokuwa na baba mpya huongeza hatari ya kupata tatizo hili la preeclampsia ukilinganisha na mwanamke anayepata ujauzito kwa mwanaume yuleyule
-
Umri wa kupata ujauzito- hatari ya kupata tatizo hili huongezeka kwa wanawake wanaopata mimba kwenye umri wa zaidi ya miaka 40 au chini ya miaka 15
-
Obeziti- kuwa na uwiano mkubwa wa uzito kwa urefu huambatana sana na tatizo hili kama inavyoonekana kwenye tafiti mbalimbali
-
Ujauzito wa mapacha- kuwa na mapacha au watoto wengi zaidi kwenye ujauzito mmoja huongeza hatari ya kupata preeclampsia
-
Muda kati ya ujauzito mmoja na mwingine- kuwa na mtoto chini ya miaka miwili au zaidi ya miaka kumi baada ya ujauzito uliopita huongeza hatari ya kupata tatizo hili la preeclampsia
-
Magonjwa mengine-kuwa na tatizo sugu la shinikizo la juu la damu kabla ya kupata ujauzito, kipanda uso, kisukari aina ya 1 na 2, magonjwa ya figo, tatizo la damu kuganda, au ugonjwa wa lupus huongeza hatari ya kupata preeclampsia
​
Madhara ya preeclampsia
Tatizo la preeclampsia linapoonyesha dalili mbaya mapema hutishia maisha ya mtoto na mama. Mama mwenye Preeclampsia anaweza kuanzishiwa uchungu ili kujifungua au kujifungua kwa upasuaji endapo kuna matatizo yanayofanya isiwe salama kujifungua kwa njia ya uke mfano mtoto kutanguliza makalio, au matatizo mengine.
Kama una preeclampsia kali au ujauzito wako una wiki chini ya 30 unawe kufanyiwa upasuaji wa kuondoa ujauzito
Madhara ya preeclampsia ni;
Kukatishwa damu inayoenda kwenye kondo la nyuma-preeclampsia hudhuru mishipa inayopeleka damu kwenye kondo la nyuma(placenta) na kama lisipopata damu ya kutosha mtoto atapata damu kidogo na kiwango kidogo cha chakula na hivyo hukua taratibu, kuwa na uzito kidogo au kujifungua kabla ya wakati, mtoto kupata matatizo ya mfumo wa upumuaji.
Kunyofoka kwa kondo la nyuma- kondo la nyuma linaponyofoka kutoka kwenye ukuta wa uzazi husababisha kuvia kwa damu ndani ya kizazi na kufa wa mtoto tumboni. Kiwango cha damu kikipotea kwa wingi mama huwa hatarini kuishiwa na damu na kifo .
Kupata dalili za sindromu ya HELLP. Dalili hii huambatana na kuvunjwa vunjwa kwa chembe nyekundu za damu mwilini, kuongezeka kwa kemikali Ini zinazoashiria uharibifu kwenye Ini, kiwango kidogo cha chembe za kugandisha damu. Dalili hizi zinapotokea huweza kusababisha majanga kwa mama na mtoto puia- dalili zake huwa ni;
​
-
Kchefuchefu na kutapika,
-
Maumivu ya kichwa na
-
Maumivu upande wa juu wa kulia ya tumbo amabapo ini limekaa.
Sindromu ya HELLP huwa hatari kwa sababu huonyesha uharibifu mkubwa wa organi mbalimbali mwilini na huweza kutokea ghafla hata kabla ya kutokea kwa shinikizo la damu la juu.
Kifafa cha mimba- kama preeclampsia ikidhibitiwa vyema kifafa cha mimba au eclampsia huwa hakitokei, kifafa cha mimba huambatana na dalili za kutetemeka mwili.
-
Dalili za mama anayeelekea kupata kifafa cha mimba ni kama maumivu upande wa kulia juu ya tumbo,
-
maumivu makali ya kichwa,
-
tatizo la kuona,
-
na kubadilika kwa
Ugonjwa wa moyo- kuwa na preeclampsia kunaongeza hatari ya kupata ugonjwa wa moyo na mishipa ya damu, hatari ya kupata ugonjwa huu huongezeka zaidi kama umeshawahi kupata preeclampsia mara mbili au umewahi kujifungua mtoto kabla ya kutimiza umri. Kuzuia kupata ugonjwa huu, mara baada ya kujifungua jaribu kuwa na uzito kiasi, kula mbogamboga za majani na matunda fanya mazoezi kwa kufuata ratiba na pia usivute sigara.
​
Vipimo vya preeclampsia
Ili Kuweza kutambua kwamba una preeclampsia, unatakiwa uwe na shinikizo la damu la juu na moja au zaidi kati ya viashiria vifuatavyo;
-
Protini kwenye kipimo cha mkojo
-
Kiwango kidogo cha chembe vigandishi damu kwenye kipimo cha damu
-
Kushindwa kufanya kazi kwa ini
-
Dalili za tatizo kwenye figo mbali na kuwa na protini kwenye mkojo
-
Maji kwenye mapafu
-
Maumivu ya kichwa yanayoanza ghafla
-
Kupata matatizo ya kutoona
Kipindi cha nyuma mtu aliambiwa na dakitari kwamba ana preeclampsia kama mama alikuwa na shinikizo la damu la juu na protini kwenye mkojo tu. Ingawa wataalamu waliobobea kutafiti tatizo hili wanafahamu kwamba mama anaweza kuwa na preeclampsia bila kuwa na protini kwenye mkojo.
Shinikizo la damu linalozidi 140/90 huwa sio la kawaida katika ujauzito, ingawa kipimo kimoja cha shinikizo la damu kikiwa juu hakimaanishi kwamba una preeclampsia. Kama dakitari akikupima na kugundua kwamba kipimo chako hakipo kawaida na baadae akakupima baada ya masaa manne kupita na akakuta shinikizo lako la damu bado lipo juu, dakitari anaweza kukuambia una preeclampsia na baadae atafanya vipimo vingine kama cha damu na mkojo.
Vipimo vinavyohitajika
Kama dakitari amekuhisi una preeclampsia, utafanya vipimo vingine kama
Kipimo cha damu- kipimo hiki kitaonyesha jinsi gani chembe zako za damu za mgandisho zipo kawaida au zimepungua na pia kitaonyesha ufanyaji kazi wako wa ini na figo.
Kipimo cha mkojo- kipimo hiki kinapima kiwango cha uwiano kati ya protini na creatine kilichopo kwenye mkojo kila wakati . Mkojo hukusanywa kwa masaa 24 kutoka kwa mgonjwa kwa kuwekewa mpira wa mkojo, kipimo kikifanyika kitaonyesha ukubwa wa tatizo la preeclampsia
Picha ya mionzi sauti ya ujauzito-ultrasound. Dakitari atakuwa akifanya kipimo hiki mara kwa mara ili kuangalia ukuaji wa mtoto. Kipimo hiki kinaweza kupima uzito wa mtoto na kiwango cha maji kwenye mfuko wa uzazi
Kipimo cha kuangalia mapigo ya moyo ya mtoto yanavyobadilika kama mtoto akiwa anajicheza tumboni.
​
Matibabu ya preeclampsia
Tiba pekee ya preeclampsia ni mimba kutolewa kwa maana nyingine kujifungua. Unakuwa hatarini kupata kifafa cha mimba, kondo la nyuma kujiachisha kutoka kuta za mfuko wa uzazi, kiharusi na kutokwa na damu kunakoweza kusababisha kuwa na shinikizo la chini la damu endapo ujauzito utabaki. Kama mimba ni changa sana basi itakuwa mapema kujifungua kichanga ambacho hakijakamilika kutengenezwa na huwa si kitu kizuri.
Kama ukigundulika una preeclampsia, dakitari wako atakufahamisha na utatakiwa kuja mara kwa mara kitengo cha uzazi kwa ajili ya uchunguzi.
Utahitaji pia vipimo vya damu ,mkojo na shinikizo la damu mara kwa mara unapokuja clinic, utahitaji kipimo cha mionzi sauti na mapigo ya moyo ya mtoto kuliko mama mwingine ambaye hana preeclampsia.
Matibabu dawa
​
Matibabu yanayoweza kutumika ni:
​
-
Dawa za kupunguza shinikizo la damu la juu .Zipo dawa aina nyingi na zingine si salama kutumia wakati wa ujauzito
-
Corticosteroids- Kama mgonjwa ana HEELP syndrome dawa hii itatumika na huweza kusaidia kwa muda kazi za ini na chembe mgando za damu(chembe zinazogandisha damu). Dawa hii pia hufanya mapafu ya mtoto kufanya kazi kama ikipewa masaa ishirinina nne kabla ya kuanzisha uchungu wa uzazi kwa mama ambaye mtoto hajafikisha wiki 37 za ujauzito
-
Dawa za kifafa- Kama ukiwa na preeclampsia kali daktari atakupa dawa kama magnesium sulphate ili kuzuia kutokea kwa kifafa.
Matibabu mengine ya preeclapmsia
​
Pumzika
Kupumzika kitandani hushauriwa sana kwa wanawake wenye kifafa cha mimb, lakini utafiti haujaonyesha faida za tendo hili. Kupumzika kunaweza kuongeza kuganda kwa damu na kushuka kwa kipato na kwa wanawake wengi kupumzika kitandani hakushauriwi kwa sasa.
Kulazwa hospitali
Endapo una preeclampsia hatari basi utalazwa hospitali na kupimwa mapigo ya moyo na kiwango cha maji kwenye mfuko wa uzazi na kama maji ni kidogo maana yake kiwango cha damu inayoingia kwenye kondo la nyuma na mtoto ni kidogo
Chakula
Kama umekutwa na preeclampsia mwishoni mwa ujauzito dakitari anaweza kuamuru ujifungue mara moja
Kama unapreeclampsia mbaya basi dakitari hataangalia kwamba mtoto anawiki ngapi na ataamua kukuanzishia uchungu ili mtoto atoke tumboni kwa ajili ya kuokoa maisha yako, kama haishauriwi kuachwa kwa muda basi upasuaji utafanyika mara moja na wakti huu unaweza kupewa dawa za magnesium sulphate kuzuia kifafa cha mimba kutokea
Baada ya kujifungua, mategemeo ni shinikizo la damu litashuka na ndani ya wiki 12 lakini huwa haraka sana kushuka hata kabla ya wiki hizo. Kama unamaumivu na unahitaji dawa za maumivu baada ya kujifungua basi mulize dakitari wako dawa gani zinafaa, dawa aina ya NSAIDs kama ibuprofen,naproxen, huongeza shinikizo la damu. Dawa aina ya panadol huwa salama kutumiwa.
Imeboreshwa, 17.07.2021
​
ULY Clinic inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchuku hatua yoyote ile inayohusu afya yako.
​
​​
Bonyeza kusoma makala zingine zaidi kuhusu;
​
​
Rejea za mada hii;
​
-
Jennifer Uzan,et al. Pre-eclampsia: pathophysiology, diagnosis, and management. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3148420/. Imechukuliwa 17.07.2021
-
Sibai B, Dekker G, Kupferminc M. Pre-eclampsia. Lancet. 2005;365:785–799
-
Pottecher T, Luton D. Prise en Charge Multidisciplinaire de la Prééclampsie. French. Issy Les Moulineaux, France: Elsevier; Masson SAS; 2009.
-
Carty DM, et al. Preeclampsia and future maternal health. J Hypertens. 2010;28:1349–1355.
-
Duley L. The global impact of pre-eclampsia and eclampsia. Semin Perinatol. 2009;33:130–137.
-
Zhang J, et al. Epidemiology of pregnancy- induced hypertension. Epidemiol Rev. 1997;19:218–232.
-
Barton JR, et al. Prediction and prevention of preeclampsia. Obstet Gynecol. 2008;112(2 Pt 1):359–372.
-
7. Rijhsinghani A, et al. Risk of preeclampsia in second-trimester triploid pregnancies. Obstet Gynecol. 1997;90:884–888.
-
Julian CG. High altitude during pregnancy. Clin Chest Med. 2011;32:21–31.