Mwandishi: ULY CLINIC
​
Mhariri: Dkt Sospeter M, MD
​
Imeandikwa 16.10.2018
Kutojimudu kwa shingo ya kizazi
​
Shingo ya uzazi kufunguka kabla ya wakati humaanisha nini?
Ni kufunguka kwa shingo ya kizazi kabla ya kuanza kwa uchungu.
​
Kutojimudu kwa shingo ya kizazi hutokea kama shingo ya kizazi imefunguka mapema katika kipindi cha pili cha ujauzito (kuanzia miezi mitatu hadi 6) kunakopelekea kutoka kwa mimba.
Ili kuitwa kwamba shingo ya kizazi haijimudu, unapaswa kuwa na vipindi viwili vya kutoka kwa mimba vilivyofuatana. Kwa hivyo shingo ya kizazi isiyojimudu humaanisha kujirudia kufunguka kwa shingo ya uzazi kabla ya uchungu.
Epidemiolojia ya tatizo
Taarifa halisi bado hazijulikani hata hivyo imeripotiwa kwenye tafiti kuwa, tatizo hili hutokea kwenye asilimia 1 ya ujauzito zote na hujirudia kwenye ujauzito unaofuata kwa asilimia 20 hadi 30 ya ujauzito zinazofuata. Inafahamika pia, asilimia 70 hadi 75 wenye shingo ya kizazi isiyojimudu bila kuwa na maumivu, ujauzito wao huendelea mpaka kipindi cha tatu cha ujauzito.
Dalili
Dalili huwa pamoja na;
​
-
Hisia za mgandamizo ndani ya nyonga
-
Maumivu mapya ya nyuma ya mgongo
-
Maumivu ya tumbo ya kubana
-
Kubadilika kwa ute unaotoka ukeni
-
Kutokwa na damu kiasi ukeni
​Visababishi
Mfuko wa uzazi umetengenezwa kwa misuli laini tishu unganishi na mishipa ya damu. Mgawanyiko wa tishu hizi kwenye shingo ya uzazi huwa sio sawia kulinganisha na sehemu nyingine ya kizazi. Kuna misuli mingi kwenye mlango wa ndani na tishu unganishi nyingi sehemu ya nje. Utofauti wa muundo wa tishu kwenye mfuko wa shingo ya kizazi unaelezewa kuwa ni sababu inayopelekea kutojimudu kwa shingo ya kizazi na kupelekea kufunguka kabla ya kufika mwisho wa ujauzito.
​
Vipimo na utambuzi
Kipimo gani cha kutegemewa kujua tatizo la shingo ya kizazi isiyojimudu?
Hufanyika awali kwa kuuliza historia ya mjamzito, lakini kuna vipimo kadhaa vinavyoweza kufanyika. Uwezo wa kupitisha mpira wa foley namba 16 au kitanua shingo ya kizazi namba 8 huweza maanisha kuna tatizo la kutojimudu kwa shingo ya kizazi. Kuna kipimo cha ultrasound inayopimwa kupitia ukeni kuingia kwenye kizazi pia kwa ajiri ya kuangalia tabia na umbo la uzazi.
Kwa miaka mingi, njia ya kutumia vidole kupima urefu wa shingo ya kizazi ilikuwa ikitumika. Lakini kwa sasa matumizi ya ultrasound yamekuwa yakiongezeka na kuwa njia muhimu katika utambuzi wa tatizo hili.
​
Kuna utofauti mdogo unatokea kati ya mpimaji mmoja na mwingine kuhusu urefu wa shingo ya kizazi ukilinganisha na njia ya kidole.
Ultrasound inauwezo wa kupima urefu wote wa shingo ya uzazi ukilinganisha na njia ya vidole ambayo hupima urefu wa shingo ya kizazi sehemu ya nje kwenye uke tu. Kuwa na shingo ya kizazi chini ya urefu wa sentimita 2.5, hutambuliwa kama shingo fupi ya uzazi, na pia kama kipimo cha ultrasound hutabili kutokea kwa tatizo la kutojimudu kwa shingo ya kizazi kama sehemu ya ndani ya shingo ya kizazi imefunguka kwenye wiki ya 24 ya ujauzito.
Vihatarishi
Kihatarishi kikuu ni kuwa na historia ya kupoteza ujauzito uliopita kutokana na kutojimudu kwa shingo ya kizazi. Matatizo ya kuzaliwa nayo ya kutofanyika vema kwa shingo ya kizazi na matumizi ya dawa ya DES yameripotiwa kuhusiana na tatizo hili. Vihatarishi vya kimazingira ni kama;
​
-
Majeraha kwenye shingo ya kizazi
-
Upasuaji wa shingo ya kizazi
-
Kukatwa kwa sehemu ya shingo ya kizazi
-
Kuchanika kwa shingo ya kizazi wakati w akujifungua
-
Kutanuliwa kwa lazima kwa shingo ya kizazi
-
Majeraha kutokana na sababu zingine​
Madhara
Madhara ya kuwa na shingo ya uzazi isiyojimudu huambatana na kujifungua kabla ya wakati au mimba kutoka. Kwa nadra sana madhara yafuatayo huweza kutokea pia;
​
-
Kupasuka kwa kizazi
-
Kuvia kwa damu ndani ya kizazi
-
Majeraha kwenye shingo ya kizazi
-
Maambukizi ya shingo ya kizazi au ndani ya uzazi
Matibabu
Hakuna orodha ya matibabu mengi yanayoweza kutibu tatizo hili ipasavyo. Matibabu huanza kwa kupumzika kwa muda fulani kitandani au bila kufanya kazi na kufanyiwa upasujai wa kuimairhsa shingo ya kizazi kwa muda.
Nani ni mteja wa kufungiwa shingo ya kizazi kwa mda?
​
Wanawake waliothibitishwa kwamba wana shingo ya kizazi isiyojimudu hufanyiwa upasuaji huu mdogo. Upasuaji huu hufanyika kwa mama ambaye hana dalili za uchungu tu.
Kuwa na uchungu kunamaanisha uchungu kabla ya wakati na hivyo matibabu ya upasuaji hayatafanyika kwa sababu mimba inaweza kutoka wakati wowote.
Baadhi ya wataalamu wanatoa hoja kwamba kufunguka kwa shingo ya kizazi kabla ya wakati kunaweza kuanzisha uchungu na hivyo kuleta utata nani afanyiwe upasuaji wa kuimarisha shingo ya kizazi hata kama hakuna uchungu. Hata hivyo hairuhusiwi kufanyiwa upasuaji huu mwanamke ambaye anauchungu.
Kipindi gani ni muafaka kwa ajiri ya kufanyiwa upasuaji huu?
Inashauriwa kwamba kufungwa kwa shingo ya kizazi kwa muda kufanyike kwenye wiki ya 13-16 za ujauzito. Kuna baadhi ya hali zinazoweza kupelekea kusogezwa mbele kwa upasuaji, mfano kwa sababu mama amechelewa kuhudhuria kliniki au kutojimudu au kama kutojimudu kumetokea bila kutarajiwa.
​
Kwa watu kama hawa upasuaji unaweza kufanyika hadi wiki ya 23 ya ujauzito. Kama mtoto anaweza kuishi endapo mama atajifungua, upasuaji huu mara nyingi pia huwa haufanyiki.
Marufuku ya upasuaji huu ni nini?
Hali na mambo yafuatayo huzuia kufanyika kwa upasuaji w akuimarisha shingo ya kizazi;
-
Kuwa na uchungu
-
Kupasuka kwa chupa ya uzazi
-
Maambukizi ndani ya chupa ya uzazi
-
Kutokuwa kwa mtoto ndani ya mfuko wa uzazi
-
Matatizo mengine makubwa ya uumbaji wa mtoto
Madhara ya upasuaji huu ni yapi?
Madhara yanayohusiana na upasuaji wa kuimarisha shingo ya kizazi kwa muda yamegawanyika kwenye makundi mawili. Yale yanayotokana na upasujia na yale yanayotokea baadae.
-
Madhara kutokana na upasuaji ni;
-
Madhara ya dawa za usingizi
-
Majeraha kwenye tishu za mama
-
Kutokwa na damu
-
Maambukizi
-
Kupasuka kwa chupa ya uzazi
-
Mimba kutoka
Madhara ya baadae ni kama;
-
Kuchanika kwa shingo ya kizazi
-
Kufanyika kwa fistula
-
Ongezeko la kujifungua kwa upasuaji
​ Wakati gani shingo ya kizazi hufunguliwa?
Mshono wa kufunga shingo ya kizazi kwa muda hushauliwa kuondolewa kwenye wiki ya 37-38 za ujauzito kabla uchungu haujaanza ili kupunguza hatari ya uharibifu wa shingo ya kizazi na kuchanika kwa mfuko wa kizazi. Mara nyingi nyuzi huweza kutolewa kwenye ofisini na wakati mwingine inaweza hitajika kuingia chumba maalumu cha upasuaji ili kutolewa chini ya kaputi.
Kinga
Inaweza kuwa vigumu kuzuia visababishi vya kutojimudu kwa shingo ya kizazi, hata hivyo kuna mambo unaweza kufanya ili kuishi na ujauzito mpaka muda wa kujifungua ufike. Mambo hayo ni;
Hudhuria kliniki yako.
Kuhudhuria kliniki kutakusaidia wewe na daktari wako kufanya uchunguzi w amaendeleo yako na afya ya mtoto. Wakati umefika kliniki ongea na daktari kuhusu dalili unazopata hata kama unafikiria kuwa hazina maana.
Kula mlo wa kiafya
Mlo wa kiafya utakufanya uwe na afya njema wewe na mwanao tumboni. Chakula unachotakiwa kula ni kile chenye wingi wa;
-
Folic acid
-
Kalisiamu
-
Chuma
-
na madini mengine madogo
Kama hupati viinilishe kutoka kwenye chakula, unapaswa kuwasiliana na daktari uone uwezekano wa kupata kutoka kwenye vidonge vyenye virutubisho vya nyongeza.
Dhibiti ongezeko la uzito
Unapaswa kuwa na ongezeko la kawaida la uzito kutokana na mtoto anavyokuwa tumboni. Ongezeko la uzito wa kilo 11 hadi 16 ni kawaida wakati wa ujauzito, ongezeko zaidi a hili ni ongezeko lililokithiri.
Usitumie vitu vya hatari
Vitu vya hatari vinaweza kudhuru ujauzito wako, mfano wake ni
-
Matumizi ya tumbaku au kuvuta sigara
-
Kunywa tombe
-
Kutumia dawa za kulevya au zile zisizoruhusiwa wakati wa ujauzito
​
Unapaswa kuwasiliana na daktari wako pia kabla hujatumia dawa yoyote ile hata kama ni dawa zinazonunuliwa bila cheti cha daktari.
Wasiliana na daktari kama una historia ya tatizo hili
Kuna hatari ya kujirudia kwa tatizo la kutojimudu kwa shingo ya kizazi kwenye ujauzito zinazofuata. Kama umepanga kuwa mjamzito, unapaswa kuwasiliana na daktari wako kwa uchunguzi na ushauri kabla ya kubeba ujauzito mwingine.
Mambo ya kutofanya
Kama una tatizo la kutojimudu kwa shingo ya kizazi wakati wa ujauzito, daktari atakushauri kutojishungulisha na ngono au kutofanya baadhi ya shughuli kama vile kunyoanyua vitu vizito n.k. Soma zaidi kwenye makala za mazoezi wakati wa ujauzito.
​
Majina mengine
​
Majina mengine yanayotumika kumanisha shingo ya kizazi ni;
-
Kutojimudu kwa Seviksi
-
Kutojiweza kwa shingo ya kizazi
-
Cervical incompetence
-
Kutojiweza kwa hsingo ya uzazi
​
Imeboreshwa , 11.10.2021
​
ULY Clinic inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchuku hatua yoyote ile inayohusu afya yako.
​
​​
Rejea za mada hii;
​
-
Berghella V, et al. Cervical insufficiency. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 11.10.2021
-
Gabbe SG, et al. Cervical insufficiency. In: Obstetrics: Normal and Problem Pregnancies. 7th ed. Philadelphia, Pa.: Saunders Elsevier; 2017. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 11.10.2021
-
Papadakis MA, et al., eds. Obstetrics and obstetric disorders. In: Current Medical Diagnosis & Treatment 2018. 57th ed. New York, N.Y.: McGraw-Hill Education; 2018. http://accessmedicine.mhmedical.com. Imechukuliwa 11.10.2021
-
Tanner LD, et al. Maternal race/ethnicity as a risk factor for cervical insufficiency. European Journal of Obstetrics & Gynecology and Reproductive Biology. 2018;221:156.
-
Boelig RC, et al. Current options for mechanical prevention of preterm birth. Seminars in Perinatology. 2017;41:452.
-
American College of Obstetricians and Gynecologists (ACOG) Committee on Practice Bulletins — Obstetrics. ACOG Practice Bulletin No. 142: Cerclage for the management of cervical insufficiency. Obstetrics & Gynecology. 2014;123:372.
-
What can I do to promote a healthy pregnancy? National Institute of Child Health and Human Development. https://www.nichd.nih.gov/health/topics/preconceptioncare/conditioninfo/healthy-pregnancy. Imechukuliwa 11.10.2021
​
​
Bonyeza kusoma makala zingine zaidi kuhusu;
​