Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Mangwella S, MD
Jumanne, 6 Aprili 2021
Mafua ya aleji
Mafua ya aleji kwa jina jingine homa ya hay au rhinaitizi ni ugonjwa unaotokea sana kwa binadamu.
Mafua haya hutokea kutokana na michomo kwenye kuta za mfumo wa hewa haswa njia za pua. Ugonjwa huu huweza kuambatana na magonjwa mengine kama sinusaitizi sugu, pumu ya ngozi na kifua
Watu wanaopata tatizo hili sana ni wale wenye shida ya asthma/pumu, ezima na watu walio na historia ya asthma au rhinaitis kwenye familia zao
Umri wa tatizo la mafua ya aleji kuanza
Tatizo la mafua ya aleji linaweza kuanza muda wowote ule, hata hivyo watu huanza kupata dalili wakati wa utotoni na wanapoanza kukua watu wazima. Dalili mara nyingi huwa kali kwa watu wazima wenye umri kati ya miaka 30 hadi 50.
Nini husabaisha mafua ya aleji?
Kisababishi cha mafua ya aleji ni kuamshwa kwa seli za aleji kwenye njia ya hewa(puani), seli hizo zinazoitwa seli za mast na basophilis zikiamshwa huanza kutoa kemikali ya histamine ambayo husababisha michomo, kuvimba na kujaa kwa majimaji kwenye kuta za ndani ya pua hivyo kusababisha dalili za kushindwa kupumua, kuwashwa ndani ya pua, kupiga chafya na mafua kuchuruzika
Mafua ya aleji hutokea wakati gani?
Mafua ya aleji huweza kutokea kwenye msimu Fulani katika mwaka au kutokea muda wote katika mwaka.
Mafua ya msimu husababishwa na uchokozi wa poleni kutoka kwenye majani, miti au magugu wakati huo mafua ya aleji yanayotokea muda wowote huamshwa na viamsha aleji kama vumbi, vumbi la kinyesi cha wanyama, vumbi la miili ya mende na chawa, vumbi la wanyama na fangasi
Dalili za mafua ya aleji
Kupiga chafya
Kuchuruzika kwa mafua(rhinolea)
Kuchuruzika kwa mafua nyuma ya koo
Kuziba kwa pua
Kuwashwa kwa pua
Dalili zingine za mafua ya aleji
Kikohozi
Uchovu wa mwili
Kuwashwa kwenye koo/paa la mdomo na masikio
Kuwshwa kwa macho, kutokwa na machozi na kuhisi macho kuungua
Kutoa sauti kama ya farasi
Kupumulia mdomo
Macho kuwa mekundu
Vihatarishi vya kupata mafua ya aleji
Kuwa na historia kwenye familia ya tatizo la atopi (rhinaitis, pumu ya ngozi au kifua) ni;
Kuwa mwanaume
Kuzaliwa kipindi cha kutoka kwa maua
Kuishi na watu wanaovuta sigara kipindi cha mwaka wa kwanza baada ya kuzaliwa
Kukaa kwenye maeneo yenye viasha aleji
Kuwa na antijeni ya aleji ya IgE
Matibabu ya mafua ya aleji
Matibabu huhusisha kupunguza kukutana na viamsha aleji ambavo vimetajwa hapo juu pamoja na matumizi ya dawa za kupunguza aleji
Namna ya kudhibiti dalili za mafua ya aleji
Mafua ya aleji yanaweza kudhibitiwa kwa;
Kuzuia kukutana na viamsha mafua ya aleji
Kutumia maji kusafisha pua
Kutumia dawa jamii ya antihistamine
Kutumia dawa jamii ya glukokotikoidi
Kutumia dawa za kuzibua pua kabla ya kuanza kutumia dawa za glukokotikoidi
Kutumia dawa za kunjwa kwa ajili ya kuzibua pua kama pseudoephedrine au dawa zinazouzwa maduka ya dawa baridi jamii ya antihistamine
Kujifukiza kwa mvuke wa maji ya moto yenye mchanganyiko wa majani au dawa asilia zinazosemekana kuzibua pua kama vile tangawizi n.k chukua tahadhar kuepuka kuungua mfumo wa hewa, wasiliana na daktari wako kabla ya kufanya hivi.