Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Mangwella S, MD
Jumanne, 6 Aprili 2021
Mafua ya kirusi Influenza
Mafua ni tatizo linalofahamika sana duniani kote na hutokea mara kwa mara kwa binadamu. Makala hii imeangalia mafua yanayosababishwa na kirusi maarufu cha jina la kirusi cha influenza.
Je mafua ya kirusi cha influenza hufahamika kwa jina gani jingine?
Mafua ya kirusi cha influenza kwa jina jingine hufahamika kama homa ya mafua, hii ni kwa sababu kirusi huyu huleta mafua ambayo yanaambatana na homa.
Aina za virusi vya influenza
Virusi vya influenza vinavyosababisha sana mafua kwa binadamu ni kirusi aina
Influenza A
Influenza B
Kirusi huyu hukaa kwenye majimaji ya mfumo wa hewa kwa mgonjwa aliyeambukizwa na mara baada ya mambukizi huchukua takribani siku 1 hadi 4 kuanza kupata dalili za mafua na chafya.
Hata hivyo kuna aina ya tatu ya kirusi cha influenza ambaye husababisha mafua yasiyo makali sana, kirusi huyo ni Influenza C
Usambazaji wa kirusi cha mafua ya influenza
Mafua yanayosababishwa na kirusi huyu huwa yanaambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya;
Matone ya maji wakati wa kupiga chafya, kukohoa
Kugusa maeneo ambayo yameguswa na mgonjwa wa mafua
Kutumia vifaa na vyombo pamoja na mtu mwenye mafua
Kukaa karibu na mtu mwenye mafua
Hata hivyo ni vema kufahamu kuwa mtu anaweza kusambaza kirusi huyu siku 5 hadi 10 kabla ya kuanza kuonyesha dalili, kwa watoto na watu wenye kinga za mwili za chini kirusi huweza kusambazwa kwa watu wengine takribani siku 10 hadi miezi kadhaa baada ya kupata dalili za mafua.
Mafua ya kirusi Influenza hutokea wakati gani katika mwaka?
Mafua ya virusi hutokea kipindi cha miezi yenye baridi, hii ni kwa sababu watu katika wakati huu huwa wanapenda kukaa karibu karibu kwa sababu ya baridi. Wakati huu kirusi cha influenza husambazwa kutoka kwa mtu mmoja na kwenda kwa mwingine
Dalili za mafua ya kirusi cha Influenza
Dalili huambatana na kuanza ghafla kwa
Homa
Maumivu ya kichwa
Maumivu ya misuli
Na uchovu wa mwili
Dalili zingine za mafua ya Kirusi cha Influenza
Dalili pia zinaweza kuambatana na dalili zingine za maambukizi mfumo wa hewa kama
Kikohozi kikavu
Koo kavu
Kutokwa na makamasi
Dalili za mafua ya kirusi cha Influenza hupotea baada ya muda gani?
Dalili za mafua ya virusi hupotea baada ya siku 2 hadi 5, hata hivyo ugonjwa unaweza kudumu kwa wiki moja au zaidi
Kinga na matibabu ya mafuaa ya kirusi cha Influenza
Ingawa ugonjwa huu huambukizwa, unaweza kujikinga kwa kupata chanjo ya kirusi cha influenza. Chanjo mara nyingi ni muhimu kwa watu ambao wapo kwenye hatari ya kupata madhara makubwa kutokana na maambukizi ya kirusi huyu.
Dawa za antivirus hutumika kupunguza makali ya dalili za kirusi huyu lakini huwa haziondoi ugonjwa kabisa. Matumizi ya dawa hushauriwa kutumika ndani ya masaa 48 toka dalili za maambukizi kuanza kuonekana
Matibabu ya mafua haya hufanya mtu ajihisi vema, hata hivyo tiba huwa haifupishi muda wa ugonjwa kukaa ndani ya mwili
Matibabu pia yasiyo dawa ya mafua ya kirusi cha Influenza
Kupumzika mpaka dalili kali zitakapoisha- kwa wale wenye dalili kali za mafua
Kunywa maji ya kutosha ili kujikinga na kuishiwa maji mwilini
Matumizi ya panado kupunguza homa na maumivu ya kichwa
Kujifukiza kwa mvuke wa maji ya moto yenye mchanganyiko wa majani au dawa asilia zinazosemekana kuzibua pua kama vile tangawizi n.k chukua tahadhar kuepuka kuungua mfumo wa hewa, wasiliana na daktari wako kabla ya kufanya hivi
Kumbuka
Dawa za kuzuia kukohoa huwa hazisaidii kwa sababu kikohozi huisha chenyewe pasipo matibabu
Madhara ya mafua ya kirusi cha Influenza.
Madhara mara nyingi huwa hayatokei, hata hivyo huweza kutokea kwa baadhi ya watu wenye kinga za mwili za chini kama vile
Nimoni ya virusi
Nimonia ya bakteria
Mayolisisi
Perikadaitis
Rabdomayolisisi
Sindromu ya toksik shoku
Wakati gani wa kwenda hospitali endapo una mafua ya kirusi cha Influenza?
Endapo mgonjwa anapata dalili zifuatazo hakikisha anafika hospitali kupata matibabu ya haraka
Kwa mtoto
Kuhema kwa haraka haraka au kupata shida ya kuhema
Kubadilika rangi na kuwa na rangi ya bluu
Kuishiwa maji
Homa pamoja na harara kwenye ngozi
Kushindwa kula vema
Kwa mtu mzima
Kupumua kwa shida, au kuishiwa pumzi
Maumivu au kuhisi mgandamizo wa kifua
Kizunguzungu cha ghafla
Kuchanganyikiwa
Kutapika sana au kutapika kunakoendelea