Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Mangwella S, MD
Ijumaa, 2 Julai 2021
Magonjwa ya zinaa
Ugonjwa wa zinaa au magonjwa ya zinaa ni magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya kujamiana, inaweza kuhusisha kujamiana kwa kuingiza uume au uke mdomoni, ukeni na uume kwenye tundu la haja kubwa. Kwa imezoeleka wanawake na wanaume ndio wanajamiana, kwa sasa kuna njia nyingingine zaidi ya kujamiana na hivyo njia zote ambazo zinahusisha kubadilishana majimaji kwenye viungo vilivyotajwa hapo huu huitwa kujamiana na huchangia kwenye maambukizi ya magonjwa ya zinaa.
Takwimu za magonjwa ya zinaa duniani
Matokeo ya utafiti wa kimataifa wa shirika la afya duniani (WHO) kwa mwaka 2016 umeonyesha kwamba zaidi ya wanawake na wanaume milioni 376 wa umri wa miaka kati ya 15 hadi 49 wana maambukizi ya magonjwa ya zinaa. Orodha hiyo inaongozwa na muwasho ukiongoza kwa visa milioni 156, ukifuatiwa na klamidia visa milioni 127, huku kisosnono kikiwa na visa milioni 87 na kaswende visa milioni 6.3
Kwa ujumla magonjwa haya kwa mwaka 2016 yamesababisha watoto takribani 200,000 kufia tumboni na pia idadi kubwa ya vifo vya watoto wachanga na kufanya kuwa sababu iliyoongoza kwa vifo vya Watoto duniani kwa mwaka huo.
Takwimu magonjwa ya zinaa Tanzania kupitia mtandao wa ULY CLINIC
Tafiti zinazofanywa na kupitia mtandao wa ULY CLINIC mwaka 2020/2021 zimeonyesha kuwa, wastani wa wanaume 15 kila mwezi wanatafuta matibabu ya magonjwa ya zinaa, dalili kuu ni kutokwa na usaha kwenye uume na pia wanawake 5 wanatafuta tiba kila mwezi kwa kuwa na dalili ya kutokwa na uchafu usio wa kawaida ukeni hivyo kufanya jumla ya visa kuwa jumla ya 20 kila mwezi na 240 kwa mwaka.
Takwimu hizi ni kubwa na inakadiliwa kuwa mara mbili au tatu zaidi ya hii kwa kuwa mtandao wa ULY CLINIC bado haujaweza kuwafikia watu wengi zaidi kwa sasa.
Taarifa za data za tovuti ya ULY CLINIC kwa mwezi Juni 2020 hadi Juni 2021 zimeonyesha jumla ya watumiaji 2,821 walitafuta kuhusu dawa za gono, hii inaendelea kuonyesha kuwa tatizo hili ni kubwa.
Dalili
Dalili za magonjwa ya zinaa zimetajwa hapa bila kuzingatia jinsia, yaani dalili hizi zinaweza tokea kwa mwanaume na mwanamke. Hata hivyo asilimia 50 hadi 80 ya wanawake wanaougua magonjwa ya zinaa huwa hawaonyeshi dalili yoyote ile, inashauriwa kwamba endapo mwanaume ameonyesha dalili, wanawake wote anaoshiriki nao wanapaswa kupata matibabu ili kuzuia kupata maambukizi au kusambaza maambukizi kwa mpenzi ambaye amepata dawa na kupona. Endapo dalili zitatokea huhusisha dalili zilizoorodheshwa hapo chini.
Dalili zamagonjwa ya zinaa kwa wanawake
Kutokwa na harufu kali ukeni (kama ya kitu kimeoza au samaki)
Kutokwa na ute wenye rangi isiyo ya kawaida ( njano, bluu, kijivu)
Maumivu ya tumbo la chini ya kitovu
Kuota kwa malengelenge kwenye mashavu ya uke au uke
Kuvimba kwa mitoki ya maeneo ya kinena( karibu na mikunjio ya mapaja)
Kuota kwa vipele visivyouma au vinavyoume kwenye mashavu au maeneo yoyote ya uke
Maumivu wakati wa kujamiana
Dalili za magonjwa ya zinaa kwa wanaume
Kutokwa na usaha sehemu za siri
Maumivu wakati wa kukojoa au kumwaga shahawa
Kumwaga shahawa zenye damu
Kuota kwa vidonda vinavyouma kwenye kichwa au mpini wa uume
Kuota kwa malengelenge kwenye sehemu za siri
Kuvimba kwa mitoki ya maeneo ya kinena( karibu na mikunjio ya mapaja)
Maumivu ya korodani au tezi dume endapo zitashikwa au kugandamizwa wakati wa kujamiana
Kuota kwa vipele visivyouma kwenye uume
Maumivu ya tumbo la chini ya kitovu
Aina ya magonjwa ya zinaa
Makala hii imetaja aina mbili za magonjwa ya zinaa, ambazo ni;
Magonjwa ya zinaa yasiyo yasiyo tibika
Magonjwa ya zinaa yanayotibika
Magonjwa ya zinaa yanayotibika
Magonjwa ya zinaa yanayotibika ni yale ambayo mwathirika akiyapata, akipewa dawa atapona. Hata hivyo ili kuzuia madhara makubwa ya ugonjwa, mwathirika anatakiwa kufika hospitali mapema zaidi mara atakapotambua dalili zilizoorodheshwa hapo juu.
Orodha ya magonjwa ya zinaa yanayotibika;
Klamidia (Chlamydia)
Trikomoniasis (Trichomoniasis)
Sunzua (maoteo sehemu za siri)
Chawa wa mavuzi
Maikoplazma genitalium
Granuloma inguinale
Skebiz (Scabies)
Kaswende
Chankroidi (chankroid)
Limfagranuloma veneramu (LVG)
Katika magonjwa hayo yote, magonjwa mashuhuri ya zinaa ni klamidia, kaswende, kisonono(gono) na trikomoniasis
Magonjwa ya zinaa yasiyotibika
Mbali ya magonjwa hayo hapo juu, magonjwa ya zinaa yasiyotibika ni;
Homa ya ini aina B ( Hepataitiz B)
Virusi vya herpes aina ya 1 na 2 (viirusi vya malengelenge aina 1 na 2)
Virusi vya UKIMWI (VVU)
Kirusi cha human papilloma (HIV)
Vipimo na uchunguzi wa magonjwa ya zinaa
Magonjwa mengi ya zinaa huwa hayahitaji vipimo ili kutambua, utambuzi huhusisha kuulizwa maswali maalumu na daktari, kisha kufnayiwa uchunguzi wa awali wa mwili bila kipimo. Daktari atachunguza sehemu za siri ili kuangalia ute unaotoka ukeni au kwenye uume, rangi yake na kama una damu au la pamoja na dalili zingine za magonjwa ya zinaa kisha anaweza kukupa dawa moja kwa moja au kushauri kufanyika kwa vipimo. Endapo vipimo vitashauriwa kufanyika huhusisha kuchukua sampuli ya damu au ute kutoka kwenye ute wa ukeni au unaotoka kwenye shingo ya kizazi au njia ya haja kubwa au kwenye tundu la uume. Kijiti kidogo kitatumika kuchukua sampuliza ute na sindano itatumika kuchukua sampuli za damu.
Baadhi ya vipimo vinavyoweza kshauriwa fanyika ni;
Kipimo cha FBP
Kipimo cha kaswende na Virusi vya UKIMWI kwenye damu
Kipimo cha culture ya ute
Kipimo cha picha ya Ultrosound au hysterosalpingography
Matibabu ya magonjwa ya zinaa
Magonjwa ya zinaa manne ambayo ni Kisonono (gono), klamidia, trikomoniais, LVG, Maikoplazma genitalium, Granuloma inguinale hutibiwa kwa pamoja kwa kutumia mchanganyiko zaidi ya dawa moja za antibiotic. Baadhi ya dawa zinazotumika ni;
Doxycycline
Erythromycin
Azithromycin
Metronidazole au tinidazole
Ceftriaxon
Muda wa matibabu hutegemea jinsia na hali ya mtu na aina ya ugonjwa ulionao, hata hivyo matibabu huweza kuchukua kati ay siku 7 hadi 21.
Matibabu ya Kaswende
Matibabu ya kaswende huhusisha kutumia dawa ya kuchoma kwenye misuli ya Penicillin G Benzathine
Matibabu ya magonjwa ya zinaa kutokana na virusi
Magonjwa ya zinaa yanayosababishwa na virusi huwa hayana tiba kuponya, endapo maambukizi yametokea, yatadumu na huweza kuambukizwa kwa mtu mwingine. Matibabu yake ambayo yanalenga kudhibiti au kuzuia kusambaa kwa ugonjwa yameorodheshwa hapa chini.
Matibabu ya Herpez
Matibabu ya kuzuiamakali ya maambukizi ya herpes huhusisha matumizi ya dawa za Acyclovir, valacyclovir, au famciclovir
Matibabu ya VVU
Matibabu ya VVU huhusisha matumizi endelevu ya dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI zenye jina ya ARV.
Chanjo ya magonjwa ya zinaa
Zipo chanjo mbalimbali ambazo zimeonekana kufanya kazi, mfano wa chanjo ni chanjo ya maambukizi ya HBV na HPV.
Athari za magonjwa ya zinaa
Athari mbaya za magonjwa manne mashuhuri ya zinaa yanayotibika ambayo ni klamidia, kisosonono, kaswende na muwasho sehemu za siri ambazo hutokea endapo matibabu yatachelewa ni pamoja na;
Makovu kwenye mirija ya uzazi
Makovu njia ya mkojo
Ugumba kwa mwanaume na mwanamke
Kupoteza ujauzito
Mtoto kufia tumboni
Matatizo wa wakati wa ujauzito
Saratani ya mlango wa kizazi
Saratain ya koo
Ongezeko la hatari ya kuambukizwa Virusi vya UKIMWI
Ongezeko la hatari ya kupata bakteria vajinosis
Kinga
Ili kujikinga na magonjwa ya zinaa inapaswa kufanya mambo yafuatayo;
Kuacha ngono
Njia pekee na madhubuti ya kukinga maambukizi ya magonjwa ya zinaa ni kuacha kushiriki ngono aina yoyote ile
Tumia kondomu
Endapo unashindwa kuacha kushiriki ngono, unaweza tumia kondomu kwa namna sahihi ili kuepuka magojwa ya zinaa. Kumbuka unaweza kupata magonjwa endapo kondom itapasuka au endapo utashiriki ngono ya kuhusisha midomo kwa mdomo, au uke kwa uke, njia ambazo ni vigumu kutumia kondomu.
Punguza idadi ya wapenzi unaofanya nao ngono
Kupunguza idadi ya wapenzi unaoshiriki nao ngono itapunguza hatari ya kupata magonjwa ya zinaa. Ni vema wewe na mpenzi wako mkapima na kushirikishana majibu endapo mmekaa muda mrefu bila kukutana kwa usalama wenu.
Pata chanjo
Kupata chanjo ya zinazopatikana kama ya HPV, HBV na zingine zinapunguza hatari ya kupata magonjwa ya zinaa ambayo hayana tiba. Licha ya kupata chanjo bado utahitajika kujikinga na hatari za kupata maambukizi kwa njia zingine zilizotajwa hapo juu.
Je matumizi ya njia za uzazi wa mpango hukinga kupata magonjwa ya zinaa?
Matumizi ya njia za uzazi wa mpango isipokuwa kondomu, hayawezi kukuzuia kupata magonjwa ya zinaa. Watu wengi wamekuwa wakifikiria kwamaba endapo watatumia njiti, vizuizi au vidonge vinavyozuia kupata ujauzito watajikinga na magonjwa ya zinaa, hii si kweli. Magonjwa ya zinaa yanaambukizwa endapo utagusana na majimaji yaliyo kwenye milango iliyotajwa hapo juu yaani midomoni, ukeni, na njia ya haja kubwa.
Endapo unatumia njia za uzazi wa mpango isipokuwa kondomu, kuna uhaja wa kufuata hatua za kujikinga na magonjwa ya zinaa kama zilivyoorodheshwa hapo juu.
Sehemu gani unaweza kupata taarifa zaidi kuhusu magonjwa ya zinaa?
Unaweza kupata taarifa zaidi kwenyemakala za ULY CLINIC zinazohusu kila ugonjwa wa zinaa kwa kuandika ugonjwa huo unaotaka kuoma
Majina mengine ya magonjwa ya zinaa
Magonjwa ya zinaa yamekuwa yakiitwa kwa majina tofauti, jina kuu ambalo watu wamezoea kulitumia ni ugonjwa wa gono au kisonono. Ifahamike kuwa, kutokwa usaha sehemu za siri haswa kwa wanaume hakusabaishwi na gono tu bali na baadhi ya magonjwa mengine ya zinaa yaliyoorodheshwa hapo juu. Kwa wanawake, kuwa na maumivu chini ya tumbo na kutokwa na uchafu ukeni si moja kwa moja dalili ya PID bali inaweza kuwa dalili ya magonjwa ya zinaa. Unahitaji kuongea na daktari wako kwa uchunguzi ili kufahamu ni shida gani inayokusumbua kabla ya kujihukumu unaumwa nini kwa ufanisi wa matibabu yako.
Makala hii imejibu pia sehemu ya maswali ya 'dalili za magonjwa ya zinaa kwa wanaume' na 'dalili za magonjwa ya zinaa kwa wanawake' na 'dawa za magonjwa ya zinaa kwa wanaume na wanawake'