Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Mangwella S, MD
Jumapili, 4 Julai 2021
Polisaithemia
Kuwa na damu nyingi hufahamika kwa jina jingine la polisaithimia (polycythemia) ni tatizo linalotokea endapo kiwango cha himoglobin ni kingi kuliko kawaida ya umri au jinsia ya mtu. Kwa mwanaume mtu mzima kiwango kikizidi gramu 16.5 kwa desilita moja ya damu (16.5g/dL) au kuzidi 16g/dL kwa mwanamke mtu mzima hufaa kuitwa tatizo la polisaithemia au damu nyingi. Kiwango cha damu cha kwaida kwa watoto kimeandikwa sehemu nyingine katika tovuti hii.
Katika makala hii utasoma kuhusu kuhusu polisithemia ya awali kwa jina jingine la polisaithemia vera na polisaithemia ya sekondari.
Dalili
Dalili za kuwa na damu nyingi kupita kawaida mwilini ni;
Muwasho
Maumivu ya kichwa
Kizunguzungu
Kupata majeraha kirahisi au kutokwa na damu kirahisi
Kutokwa na jasho zaidi ya kawaida
Maumivu na kuvimba kwa maungio
Kupungua uzito bila sababu
Njano kwenye macho na ngozi
Kuchoka
Maumivu ya tumbo
Alama za zambarau au nyekundu kwenye ngozi
Wakati gani wa kutafuta msaada wa dataktari haraka mwenye damu nyingi?
Endapo unatatizo la damu nyingi na unapata dalili zifuatazo, unapaswa kuonana na daktari haraka kwa uchunguzi na tiba;
Kutokwa na damu muda mrefu
Kuvimba endelevu kwa maungio
Kupumua kwa shida
Kuishiwa pumzi
Dalili za kiharusi kama kushindwa kuongea au kuwa dhaifu sehemu moja ya mwili
Visababishi
Visababishi vya polisithemia vinaweza kuwa vya awali au sekondari. Visababishi vya awali vinahusisanishwa na mabadiliko kwenye jeni JAK2 ya mifupa inayopelekea uzalishaji endelevu wa damu na huweza kurithiwa. Bado haijulikani kwanini mabadiliko haya yanatokea na pia ugonjwa unaotokana na mabadiliko hayo huitwa polisaithimia vera.
Visababishi vya sekondari hutokana na sababu zinazopunguza kiwango cha oksijeni kwenye tishu, kwa jina la haipoksia ya tishu au matumizi ya homon erythropoietin. Sababu mbalimbali zinaweza pelekea polisaithimia ya sekondari ni;
Magonjwa ya mapafu na moyo
Saratani ya figo, ini, na mfuko wa kizazi na polisaithimia vera
Uvutaji sigara
Upungufu wa maji mwilini
Msongo
Matumizi ya homon erythropoietin bila sababu ya msingi
Tatizo la kurithi la polisaithimia vera
Tatizo hubebwa kwenye jeni na mtoto anaweza kuzaliwa nalo. Hata hivyo kuna visababishi vingine ambavyo mtu anaweza kupata ugonjwa wa polisaithimia vema isiyo ya kurithi.
Saratani ya polisaithimia vera
Husababisha uboho wa mifupa kuzalisha chembe nyekundu za damu kwa wingi.
Kuishi mbali na usawa wa bahari.
Maeneo ya nyanda za juu na milimani huwa na kiwango kidogo cha oksijeni, mwili hutambua hilo na hivyo kuanza kuzalisha himoglobin (damu) kwa wingi ili kuweza kubeba oksijeni ya kutosha kwa ajili ya mwili wako. Hii inadhihirisha kuwa mwili wa binadamu una namna ya kujirekebisha kutegemea mazingira.
Uvutaji wa tumbaku au sigara
Uvutaji wa sigara husababisha chembe nyekundu za damu kubeba kabondayoksaidi kwa muda mrefu na hivyo mwili hutambua kama kuna upunfugu wa damu na kuamrisha ongezeko la uzalishaji wa damu.
Msongo
Msongo wa mwili pia husababisha kupungua kwa kiwango cha plasma, sehemu ya maji maji ya damu. upungufu wa majimaji kwenye damu husababisha mzunguko wa damu unaosafirisha oksijeni na virutubisho mwilini kuwa mdogo na hivyo figo huongeza uzalishaji wa homon erythropoietin ili kukabiliana nao. Hutokea kwa vijana wa umri wa kati wenye nguvu na shauku kuu na maisha.
Tatizo sugu la kuziba kwa mfumo wa upumuaji (COPD)
Ni mkusanyiko wa magonjwa ya imphizima, Bronchaitiz na bronnkiektasis. Ugonjwa huu hupelekea michomo kwenye njia za hewa inayozuia hewa ya oksijeni kusafiri vema na kuingia kwenye damu. hii hupelekea mwili kuhisi kiwang cha himoglobin hakitoshi na hivyo kuongeza uzalishaji wa damu.
Magonjwa ya moyo
Magonjwa ya moyo na mapafu yanayozuia uwezo wa mapafu kupumua au moyo kusukuma damu kwenda kwenye chembe hai, husababisha mwili hutambua upungufu wa oksijeni na hivyo kuongeza uzalishaji wa damu. mfano wa magonjwa ni fuferi kwa moyo.
Matumizi ya dawa erythropoietin
Kutumia homoni erythropoietin kama dawa bila kuwa na sababu maalumu hupelekea mwili kuzalisha damu kwa wingi. Kwa kawaida watu wenye upungufu wa damu kutokana na magonjwa ya figo au mapafu hupewa erythropoietin inayoamrisha mifupa kuzalisha au kupunguza uzalishaji wa damu. Endapo mtu atatumia bila kuwa na upungufu wa damu, hupelekea damu kuwa nyingi kuliko kawaida.
Magonjwa na saratani zinazozalisha homoni erythropoietin
Saratani ya figo, ini, kizazi na adenokasinoma huzalisha homon erythropoietin kwa wingi inayopelekea ongezeko la uzalishwaji wa chembe nyekundu za damu kupita kiasi.
Baadhi ya nyakati, magonjwa ya figo kama haidroneflosis na vifuko maji kwenye figo, huweza pelekea uzalishaji wa homon erythropoietin kwa wingi na hatimaye kusababisha tatizo la damu nyingi.
Uchunguzi na vipimo tambuzi
Mara nyingi wingi wa damu mwilini hutambuliwa kwa bahati mbaya pale daktari anapoagiza vipimo vya damu kuchunguza visababishi vya dalili ulizonazo. Hata hivyo kabla ya kuagiza vipimo, daktari atakuuliza historia ya tatizo lako kwa maswali mbalimbali ya kitaalamu kisha kukufanyia uchunguzi wa mwili wako na baadaye ataagiza kufanyika kwa vipimo mbalimbali kutokana na kisabababishi alichokishuku au anavyotaka kuvitoa kuwa si sababu.
Kipimo pekee cha kutambua kisababishi cha damu nyingi ni kipimo cha mabadiliko kwenye jeni JAK2
Endapo vipimo vingine vitaagizwa huwa pamoja na;
Kipimo cha picha halisi ya damu (FBP)
Kipimo cha kiwango cha homon erythropoietin
Kipimo cha ufanyaji kazi wa figo (RFT)
Kipimo cha ufanyaji kazi wa ini (LFT)
Vipimo vya ufanyaji kazi wa mapafu
Vipimo vya picha sauti ya Ini, figo)
Vipimo vya picha mionzi ya Ini, Mapafu au figo
Kipimo cha MRI au CT scan ya Mapafu, Ini, figo au moyo
Kumbuka vipimo vitategemea kisababishi ambacho kimeshukiwa kutokana na historia na dalili za tatizo lako zilizoonwa na daktari.
Matibabu
Matibabu ya damu nyingi hutegemea kisababishi, kuna matibabu ya dawa, upasuaji na kubadili mazingira au mfumo wa maisha;
Kubadili mazingira
Endapo kisababishi ni kuishi kwenye maeneo ya nyanda za juu, utahitaji kubadili mazingira, yaani kwenda kuishi maeneo ya usawa wa bahari au kukushauri uwe unapunguza damu kwa kutoa damu.
Kama unafanya kazi kwenye hewa ya ukaa (kabonmonoksaidi) unapaswa kuhama mazingira hayo au kutafuta kazi nyingine ili kuepuka tatizo hii
Matibabu dawa
Kuna dawa zinazotumika kuzuia uzalishaji wa damu nyingi jamii ya chemotherapi baadhi yake ni;
Chlorambucil
Radiophosphorus
Pipobroman
Anagrelide
Hata hivyo matumizi yake yanaambatana na madhara mengi hivyo wataalamu wengi huwa hawachagui matibabu hayo
Dawa mpya za kupunguza uzalishaji wa damu
Dawa mpya zinazoonekana kuwa na madhara kiasi nab ado zipo kwenye tafiti ni;
IFN-α
Ruxolutinib
Dawa za kupunguza madhara ya damu nyingi
Matibabu ya dawa za kupunguza uwezekano wa kupata madhara ya damu kuganda kama dawa za hydroxyurea, aspirin au dipyridamole huwasaidia sana wagonjwa.
Dawa za kutibu magonjwa sugu
Matibabu ya damu nyingi kutokana na magonjwa sugu ya moyo na mapafu huhusisha dawa zinazotibu tatizo husika. Mgonjwa unashauriwa kutimia vema dawa zako ili kuepuka tatizo la damu nyingi.
Kubadili mtindo wa maisha
Endapo una tatizo la damu nyingi unapaswa kubadili mtindo wa maisha kwa kuacha kuvuta sigara, kupunguza uzito na kufanya mazoezi pamoja na kula mlo wa kiafya unaoshauriwa kwa mgonjwa mwenye damu nyingi.
Matibabu ya upasuaji
Hufanyika kwa watu wenye tatizo la maumivu ya mara kwa mara ya bandama kutokana na kuziba kwa mishipa ya damu ya bandama.
Madhara
Kuwa na damu nyingi huongeza hatari ya kupata madhara yafuaatayo;
Damu kuganda inayoweza kupalekea kupata kiharusi, mshituko wa moyo, embolizimu ya palmonari na kifo
Mawe kwenye figo
Gauti
Saratani ya damu
Mayelofibrosis
Endapo tatizo ni saratani ya ini au figo, utapatiwa dawa za saratani ili kuzibiti uzalishaji wa chembe nyekundu za damu.
Magonjwa yanayofanana na polisaithimia vera
Magonjwa mengine yanayoweza kufanana na polisithemia vera
Thrombosaithemia ya awali
Leukemia sugu ya mayeloginaz
Agnogenic myeloid metaplasia
Mayelofaibrosis ya awali
Namna ya kujikinga
Ili kujikinga na uzalishaji wa damu nyingi kupita kiasi, inakubidi ufanya mambo yafuatayo;
Pata matibabu ya magonjwa ya mapafu na moyo
Acha kuvuta sigara
Jiepushe kukaa muda mrefu kwenye maeneo yenye gesi ya cabonmonoksaidi kama machimboni, kwenye miji yenye magari mengi yanayotumia mafuta ya petrol au dizeli, gereji au kufanya kazi za kurekebisha eksozi ya gari.
Ishi maeneo karibu na usawa wa bahari
Fanya uchunguzi wa vinasaba vya polisaithimia vera kabla ya kuamua kupata mtoto.