top of page

Mwandishi:

Mhhariri

ULY CLINIC

Dkt. Mangwella S, MD

Ijumaa, 18 Juni 2021

Vajinosis ya bakteria (VB)

Vajinosis ya bakteria (VB)

Ugonjwa wa vajinosis ya bakteria ni hali inayoletwwa na ongezeko kubwa la bakteria waishio ndani ya uke hivyo kuwazidi bakteria walinzi ambao pia huishi ndani ya uke. Kupotea kwa uwiano wa bakteria hawa hupelekea kuonekana kwa dalili za vajinosisi ya bakteria.


Kuharibika kwa uwiano husababisha mwili kushambulia bakteria hao kwa kuamsha chembe ulinzi mbalimbali ukeni. Matokeo ya mpambano wa chembe ulinzi na bakteria hupelekea kutokea kwa michomo ya kinga za mwili ukeni na kuonekana kwa dalili mbalimbali zinazoashiria vajinosis ya bakteria.


Licha ya tatizo hili kuathiri sana wanawake walio kwenye umri wa uzazi, yaani miaka 15 hadi 45, linaweza kutokea kwenye umri wowote pia. Vihatarishi vya ugonjwa huu ni kuwa na mpenzi mpya au kushiriki ngono na wanaume wengi, kujisafisha uke sana na kemikali kali n.k.hata hivyo vajinosis ya bakteria si miongoni mwa magonjwa ya zinaa kwa sababu huwa hauambukizwi kwa ngono.


Matibabu ya vajinosisi ya bakteria yanapatikana na watu hutibiwa na kupona, hata hivyo tatizo linaweza kujirudia baada ya muda wa miezi kadhaa kupita.


Dalili


Wanawake wengi wenye ugonjwa wa vajinosis ya bakteria huwa hawaonyeshi dalili au ishara yoyote, hata hivyo endapo dalili zitatokea zinajumuisha;


  • Kutokwa na ute mwembamba, rangi ya kijivu au mweupe kama maziwa

  • Kutokwa na harufu mbaya ukeni mithiri ya harufu ya samaki haswa baada ya kujamiana

  • Hisia za kuungua, kuwashwa ukeni au maeneo yanayozunguka tundu la uke kwa nje

  • Maumivu wakati wa kukojoa( kuungua ukeni wakati wa kukojoa au majimaji yanapopita)


Visababishi


Visababishi vya vajinosisi ya bakteria ni kuzaliana kupita kiasi kwa bakteria waishio ukeni. Uke huwa na bakteria walinzi, na bakteria hawa hufaidika nao kwa kupatiwa chakula na makazi ukeni, bakteria hao huitwa lactobacillus. Mara nyingi idadi ya lactobacillus huwa kubwa kuliko bakteria wengine wanaoishi ukeni wenye jina la Gardnerella vaginalis.


Endapo bakteria Gardnerella vaginalis amepata upenyo wa kuzaliana, huzaliana kupita kiasi na kuzidi idadi ya bakteria lactobacillus na hivyo kuharibu uwiano wa bakteria hao. Uwiano unapoharibika, hupelekea kuamka kwa dalili za vajinosis ya bakteria.


Baadhi ya sababu zinazoweza pelekea kupungua kwa idadi ya bakteria walinzi yaani lactobacillus na hivyo kutoa upenyo wa kuzaliana kwa bakteria Gardnerella vaginalis ni kusafisha ndani ya uke na sabuni kali au au mara kwa mara n.k


Vihatarishi


Vihatarishi vinavyofahamika vinavyopelekea kupata tatizo la vajinosis ya bakteria ni;


  • Kuwa na wapenzi wengi au kushiriki ngono na mpenzi mpya

  • Kujisafisha ndani ya uke kwa kutumia sabuni au kemikali

  • Kuwa na uke usio au wenye idadi ndogo lactobacillus

  • Kusafisha nguo za ndani na sabuni au kemikali kali

  • Kujitosa mwili kwenye jakuzi(beseni) la maji yaliyotiwa viuaji vimelea wakati wa kuoga

  • Kutumia marashi ya kuweka ukeni

  • Kuvuta sigara


Matendo yasiyo hatarishi


Huwezi kupata ugonjwa wa vajinosis ya bakteria kwa;


  • Kuogelea kwenye bwawa

  • Kutumia choo cha kukaa

  • Kushika vitu

  • Kulala kitandani au kujifunika mashuka


Namna ya kujikinga na ugonjwa wa vajisosis ya bakteria


  • Acha kuwa na wapenzi wengi ili upunguze hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa

  • Tumia kondomu endapo unashiriki ngono na mpenzi mpya ili kuzuia kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa

  • Unapokuwa unasafisha uke, usitumie sabuni au visafisha uke kwa sababu uke una njia asili ya kijisafisha wenyewe. Tumia maji ya kawaida tu na epuka kujisafisha mara kwa mara bila sababu isipokuwa endapo umeshiriki ngono.

  • Usitumie pedi za kuchomeka zenye viua bakteria wa ukeni


Vipimo na uchunguzi wa vajinosis ya bakteria


Utakakuwa unaonwa na daktari, atakuuliza maswali mbalimbali kuhusu dalili na vihatarishi kisha atafanya uchunguzi wa uke na kuchukua sampuli ya majimaji ndani ya uke kwa ajili ya vipimo mbalimbali endapo vitahitajika ikiwa pamoja na kipimo cha PH.


Matibabu ya vajinosis ya bakteria


Matibabu ya vajinosis ya bakteria huhusisha matumizi ya dawa za antibayotiki zinazofahamika kutibu tatizo hili. Dawa zinazoweza kutumika ni za kumeza au kuchoma kwenye mishipa au kupaka ukeni.

Kusoma kuhusu dawa nenda kwenye makala ya ‘dawa za vajinosis ya bakteria’ ndani ya tovuti ya ulyclinic.


Matibabu ya pande mbili kwa wanaoshiriki ngono ya jinsia moja yanatakiwa?


Endapo unashiriki ngono ya jinsia moja yaani KE kwa KE, wote mnapaswa kupata matibabu kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi mapya kutoka kwake.


Endapo unashiriki ngono ya KE kwa ME, hakuna faida ya kumpatia matibabu ME kwa sababu ugonjwa huu huwa hauambukizwi kutokwa kwa mwanaume kwenda kwa mwanamke.


Je ugonjwa wa vajinosis ya bakteria unaweza kujirudia baada ya matibabu?


Ndio!

Ugonjwa wa vajinosis ya bakteria unaweza kujirudia miezi michache hadi mwaka baada ya matibabu. Endapo tatizo litajirudia, utafanyiwa uchunguzi na kupewa dawa aina nyingine.


Tafiti hata hivyo zinaendelea kuangalia kama tiba ya kuongezewa bakteria wa lactobacillus inaweza kuwa suluhisho la kutibu vajinosis ya bakteria inayojirudia ndani ya muda mfupi.


Madhara ya vajinosis ya bakteria


Madhara yamegawanyika kwenye makundi mawili;


  • Madhara kwa mama mjamzito

  • Madhara kwa mjamzito na mwanamke asiye mjamzito


Madhara ya vajinosis ya bakteria kwa mama mjamzito


Ugonjwa wa vajinosis ya bakteria unaweza leta madhara yafuatayo kwa mama mjamzito endapo matibabu hayatafanyika ipasavyo;


  • Kujifungua kabla ya muda hivyo kupata mtoto njiti

  • Kujifungua mtoto mwenye umri mdogo


Madhara ya vajinosis ya bakteria kwa mjamzito au asiye mjamzito


Ugonjwa wa vajinosis ya bakteria unaweza leta madhara yafuatayo kwa wanawake endapo matibabu hayatafanyika ipasavyo;


  • Kupata magonjwa ya zinaa kama UKIMWI, kisonono, kaswende, herpes, chlamydia n.k

  • Kuambukiza mpenzi wako VVU endapo tayari una maambukizi

  • Hatari ya kupata maambukizi kwenye kidonda cha upasuaji wa via vya uzazi au baada ya kusafishwa kizazi

  • Kupata ugonjwa wa PID

  • Ugumba endapo umepata tatizo la PID kwa muda mrefu bila matibabu


Wakati gani uonene na daktari haraka ukiwa na vajinosisi ya bakteria?


Onana na daktari endapo una ;


  • Tokwa na uchafu ukeni wenye harufu kali au kuwa na rangi isiyo ya kawaida au usio w akawaida kwako

  • Una wapenzi wengi na umepata mpenzi mpya na kwa sasa unapata dalili za magonjwa ya zinaa

  • Dalili zinaendelea licha ya kufanya juhudi binafsi za kujitibu mfano kutibu fangasi n.k

  • Mambo ya kutofanya ili kuepuka bacteria vaginosis


Usifaynye mambo yafuatayo ili kuepuka kupata bakteria vaginosis;


  • Kuoga muda mrefu kwa kujitosa kwenye beseni lenye maji ya moto

  • Kujitosa kwenye beseni lenye maji au sabuni kali kwa muda mrefu

  • Kujisafisha mara kwa mara ukeni au kujisafisha kupita kiasi

  • Kujisafisha kwa kutumia kemikali kali ndani ya uke

  • Kutumia mamukato ya kuweka ukeni


Majina mengine ya vajinosis ya bakteria huitwaje?


Baadhi ya majina mengine yanayoashiria vajinosis ya bakteria ni;


  • Bacteria vaginosis

  • Vaginal bacteriosis


Wapi utapata taarifa zaidi kuhusu Vaginosis ya bakteria?


Pata taarifazaidi kwenye makala za magonjwa zilizo ndani ya tivuti ya ULY CLINIC au kwa kutumia rejea ambazo zimeandikwa chini ya tovuti hii.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba,  au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii

Imeboreshwa,

26 Oktoba 2021, 21:04:11

Rejea za mada hii:

1. Bacterial vaginosis. CDC fact sheet. Centers for Disease Control and Prevention. https://www.cdc.gov/std/bv/STDFact-Bacterial-Vaginosis.htm. Imechukuliwa 18.06.2021

2. Bacterial vaginosis. Womenshealth.gov. https://www.womenshealth.gov/a-z-topics/bacterial-vaginosis. Imechukuliwa 18.06.2021

3. Charlene W. J. Africa, et al. Anaerobes and Bacterial Vaginosis in Pregnancy: Virulence Factors Contributing to Vaginal Colonisation. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC4113856/. Imechukuliwa 18.06.2021

4. Cleocin (prescribing information). New York, N.Y.: Pfizer; 2018. http://labeling.pfizer.com/showlabeling.aspx?id=627. Imechukuliwa 18.06.2021

5. Flagyl (prescribing information). New York, N.Y.: Pfizer; 2018. http://labeling.pfizer.com/ShowLabeling.aspx?id=570. Imechukuliwa 18.06.2021

6. Frequently asked questions. Gynecologic problems FAQ028. Vaginitis. American College of Obstetricians and Gynecologists. https://www.acog.org/Patients/FAQs/Vaginitis. Imechukuliwa 18.06.2021

7. S. E. Dover, et al. NATURAL ANTIMICROBIALS AND THEIR ROLE IN VAGINAL HEALTH: A SHORT REVIEW. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC2908489/. Imechukuliwa 18.06.2021

8. Sexually transmitted diseases treatment guidelines, 2015. Centers for Disease Control and Prevention. https://www.cdc.gov/std/tg2015/default.htm. Imechukuliwa 18.06.2021

9. Sobel JD. Bacterial vaginosis: Treatment. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 18.06.2021

10. Tindamax (prescribing information). San Antonio, Texas: Mission Pharma; 2018. https://dailymed.nlm.nih.gov/dailymed/drugInfo.cfm?setid=a0d01539-8413-4703-94cc-d221918630a1. Imechukuliwa 18.06.2021

bottom of page