Mwandishi:
Mhhariri
Dkt. Mangwella S, MD
Dkt. Peter A, MD
Jumanne, 28 Desemba 2021
Kaswende
Kaswende ni ugonjwa wa zinaa unaoambukizwa sana kwa njia ya ngono zembe, tafiti zinaonyesha ugonjwa endapo hautatibiwa unaweza kusababisha matatizo makubwa mwilini. Ugonjwa wa kaswende hutibika kirahisi endapo mgonjwa yupo kwenye hatua za awali ambapo hana madhara makubwa ya ugonjwa huu.
Ugonjwa wa kaswende umegawanyika katika hatua mbalimbali kutokana na sifa ya ugonjwa huu, hatua ya kwanza, hatua ya pili ,hatua ya kujificha na hatua ya mwisho.
Katika kila hatua kuna dalili zinazoonekana
Hatua ya kwanza
Dalili za hatua ya kwanza ni;
Kupata kidonda kidogo, wakati mwingine vinaweza kuwa vingi na huwa sehemu ambayo ugonjwa huu umeingilia(mfano Uume au uke) na kidonda huwa kigumu, cha mviringo na hakiumi. Kwa sababu kidonda huwa hakiumi kinaweza kupotea pasipo mtu kugundua kwamba anatatizo na endapo kidonda kimepotea chenyewe ni sharti upate matibabu ili ugonjwa usiende hatua ya pili
Hatua ya pili
Katika hatua ya pili mgonjwa anaweza kupata ukurutu wa ngozi na vipele maeneo yanayoitwa ya ute ute yaani Myukosa (mdomoni, kwenye uke, ndani ya tundu la haja kubwa). Hatua hii inaanza na ukurutu/vipele katika sehemu moja au nyingi za mwili na huweza kuonekana vipele vya hatua ya kwanza vikiwa vinapona au wiki kadhaa baada ya hatua ya kwanza. Vipele hivi vinaweza kuwa kwenye viganja vya mikono na kwenye unyayo wa miguu na siku zote kama ilivyo kawaida ya ugonjwa huu, vipele hivyo huwa haviumi na mtu anaweza asivitambue
Dalili zingine ni;
Homa
Koo kuwa kavu
Kupoteza nywele
Kupungua uzito
Dalili za hatua hii huweza kupotea kama ukipata au usipopata matibabu na kama hujapata matibabu basi ugonjwa unaenda katika hatua ya tatu ambapo ugonjwa hujificha.
Hatua ya kujificha na ya mwisho
Katika hatua hii ugonjwa huwa umejificha na hauwezi kuonekana, endapo mtu atapima atakutwa na ugonjwa huu kwenye damu. Ugonjwa unaweza ukajificha kwa muda wa miaka mingi hata kufikia 10 hadi 30 na kisha mgonjwa anaweza kupata matatizo katika mfumo wa kutembea, kupooza, ganzi, upofu na magonjwa ya akili, haya yote yanatokea kwa sababu ugonjwa huu huwa unaenda kuathili mfumo wa fahamu. Baada ya hapa mgonjwa anaweza kuaga dunia kwa sababu ya madhara ya ugonjwa huu kuharibu mifumo mbalimbali ndani ya mwili.
Vipi ni vihatarishi vya kupata Kaswende
Kaswende huambukizwa kwa njia ya zinaa, endapo utakutana na mtu mwenye ugonjwa huu basi unaweza kuambukizwa. Maambukizi ya ugonjwa huu huweza kutokea endapo mtu anafanya ngono kwa njia ya uke, njia ya haja kubwa na mdomoni kwa sababu vidonda/ vipele vyenye vimelea vya ugonjwa huwa maeneo hayo. Endapo utagusana na kipele cha mgonjwa basi unahatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa huu.
Ugonjwa huu huweza kusafilishwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto pia akiwa tumboni au wakati wa kuzaliwa.
Kinga
Ili kujikinga na ugonjwa huu tumia kondomu unapokuwa unashirilki tendo la ndoa na pia unatakiwa uwe na mpenzi mwaminifu aliyepima.
Matibabu
Matibabu ya ugonjwa huu huhusisha kupewa dawa za antibiotiki ili kuua vimelea hawa. Mara nyingi kwa Tanzania dawa zinazotolewa hulenga kutibu aina zote za visababishi vya magonjwa ya zinaa.