top of page

Mwandishi:

Mhhariri

ULY CLINIC

ULY CLINIC

Jumanne, 25 Julai 2023

Kucheua tindikali

Kucheua tindikali

Utangulizi

Ugonjwa wa Gastroesofajio riflaksi(GERD) au kucheua tindikali hutokea pale endapo vilivyomo tumboni vinatoka nje ya tumbo kupitia mrija unaoingiza chakula ndani ya tumbo unaofahamika kwa jina la esophagus.

 

Je kucheua ni kawaida kwa binadamu?

 

Ndio kwa baadhi ya vipindi mtu mzima au mtoto mdogo au kichanga anaweza kucheua haswa baada ya kula chakula au kunyonya, vipindi hivi hutokea kwa muda mfupi na huwa haviambatani na maudhi makubwa kama ilivyo kwenye tatizo la kucheua tindikali (GERD) ambapo mrija wa esophgus huharibiwa kutokana na kuchomwa na tindikali zinazotokea tumboni.

 

Katika makala hii utajifunza kuhusu GERD kwa watu wazima tu

 

Dalili za kucheua tindikali

​

  • Kiungulia katikati ya tumbo na kifua (chemba ya moyo) haswa baada ya kula chakula, kiungulia hupanda na kuelekea kooni

  • Kucheua chakula

  • Kushindwa kumeza au maumivu wakati wa kumeza(maumivu mara nyingi yanakuwa katikati ya kifua)

  • Maumivu katikati ya kifua yanayochoma kama moto

  • Kushidwa kumeza au maumivu wakati wa kumeza(odynofagia)

  • Mabadiliko ya sauti, sauti kuwa kama ya farasi kwa sababu ya kuungua kwa misuli inayotengeneza sauti

  • Koo kuwa chungu mara kwa mara au kukohoa mara kwa mara

  • Kuhisi kitu kizito kooni au uvimbe hali hamna

  • Kichefuchefu na kutapika

 

Nini kinatokea wakati wa kucheua tindikali?

 

Mara unapokula chakula, chakula hicho hupita na kuingia kwenye tumbo kupitia mrija wa esophagus, mrija huu umetengenezwa na tishu mbalimbali pamoja na misuli ambayo hutanuka na kusinyaa ili kuweza kupitisha na kusukuma chakula wakati unameza. Mrija huu wakati unatanuka na kusinyaa hutengeneza mwendo kama wa mnyoo anavyotembea. Miishio ya mrija huu, sehemu inayounganika na tumbo la chakula, kuna misuli yenye umbo la mviringo inayotengeneza koki yenye jina la esophagial sphincter. esophagial sphincter hufanya kazi kama koki kwa kufunguka na kufungua nia ili kuruhusu chakula kiingie tumboni kisha hujifunga endapo hakuna chakula kinachoingia ili kuzuia usicheue chakula nje ya tumbo.

 

Hata hivyo baadhi ya nyakati, koki hii hulegea na kufunguka pasipo utaratibu na kufanya ucheue bila sababu, hutokea haswa baada ya kula na huwa kwa muda mfupi na kutosababisha dalili hata hivyo hali hii haitakiwi kutokea wakati wa usiku.

​

Baadhi ya watu kucheua tindikali huleta dalili sumbufu au majeraha kwenye umio, hali hii huitwa ugonjwa w akucheua tindikali (GERD). Umio linaweza kuharibiwa kwa kuunguzwa na tindikali endapo mtu anacheua mara kwa mara.

 

Vihatarishi vya kupata ugonjwa wa kucheua tindikali

 

Baadhi ya hali au vitu vinavyoweza kusababisha ugonjwa wa kucheua tindikali ni;

​

  • Henia kwenye tundu la hiatus

  • Uzito mkubwa kupita kiasi (ugonjwa wa obeziti)- tafiti hazijafahamu vizuri ni kwanini, lakini sababu zinaweza kuwa watu wenye uzito mkubwa huwa na shinikizo kubwa tumboni linalopelekea kucheua

  • Ujauzito- wanawake wengi wajawazito hucheua tindikali, hali hii huisha mara baada ya kujifungua

  • Mtindo wa maisha na dawa. Baadhi ya vyakula ikiwa pamoja na vyakula vyenye mafuta, chokoleti, pipi za minti au dawa za mswaki zenye minti, karafuu, pombe na sigara huweza kusababisha ugonjwa wa kucheua tindikali (GERD). Hata hivyo matumizi ya dawa pia haswa jamii ya NSAID kama aspirini, diclofenac, n.k huweza kusababisha kucheua tindikali.

 

Wakati gani uwasiliane na daktari?

  • Kama unashindwa kumeza au unapata maumivu wakati wa kumeza(mfano kuhisi chakula kinagoma kwenye koo)

  • Huna hamu ya kula au unapoteza uzito

  • Unapata maumivu ya kifua

  • Unajihisi kupaliwa

  • Una dalili za kutokwa damu kwenye mfumo chakula kama vile, kuonekana kwa damu kwenye matapishi, kupata choo cha kahawa au kinyesi cheusi

  • Kutapika kwa muda mrefu

  • Unapata maumivu ya tumbo na una umri zaidi ya miaka 60

 

Vipimo

Utambuzi wa tatizo la GERD hutegemea dalili na ishara na vihatarishi ulivyonavyo. Endapo una dalili ashiria ambazo ni kiungulia/kucheua, mtaalamu wa afya (daktari) anaweza kutambua tatizo la GERD kwa kutumia dalili tu bila kufanya vipimo. Katika kupindi hiki utashauriwa kutumia dawa, endapo dalili zitapungua, itafahamika tatizo kweli lilikuwa ni GERD.

 

Vipimo vya ziada vinavyoweza kufanyika ni;

Daktari wako anaweza kushauri ufanye vipimo vya ziada endapo;

 

  • Dalili hazitulii licha ya kutumia dawa jamii ya PPI

  • Huna dalili ashiria (kiungulia na kucheua)

  • Una dalili zinazoashiria tatizo kubwa

  • Una vihatarishi vya madhara ya kupata ugonjwa wa barrett's esophagus

 

Daktari atafanya hima kutofautisha tatizo hili na magonjwa mengine ya hatari mfano maumivu ya kifua kutokana na magonjwa ya moyo n.k

 

Endapo matatizo mengine ya hatari yamethibitishwa kuwa hayapo na ugonjwa wa GERD bado haujahakikishwa kuwa ndio kisababishi cha dalili,  daktari atafanya vipimo vingine vifuatavyo ili kuthibtisha tatizo la GERD.

​

  • Kipimo cha kamera (endoscope)- kinachoingizwa kwenye umio kupitia mdomo ili kuangalia tumbo na sehemu ya kwanza kabisa ya utumbo mwembamba kama kuna shida yoyote ile.

  • Kipimo cha utindikali (PH) wa kwenye umio kwa kutumia kitambzi maalumu. Kipimo hiki kitaonyesha kiwango cha tindikali kwenye mrija wa esophagus

  • Kipimo cha manometri ya umio- hupima shinikizo ndani ya mrija wa esophagus, hii itasaidia kujua shinikizo la koki ya chini kwenye mrija wa esophagus

 

Madhara ya GERD

  • Kuungua kwa mrija wa esophagus

  • Makovu kwenye mrija wa esophagus kutokana na michomo- hii huweza kupelekea kushindwa kumeza chakula

  • Ugonjwa wa barrett's esophagus

  • Magonjwa ya mapafu na koo- kutokana na michomo ya tindikali,mtu huweza kuhisi koo kavu, kukauka kwa sauti au kutoa sauti ya farasi

  • Magonjwa ya meno ikiwa pamoja na kuoza meno

 

Matibabu ya kucheua tindikali

Matibabu ya kucheua tindikali(GERD) huwa ni ya hatua mbalimbali, madhumuni yakiwa ni kudhibiti dalili na kuponya kuungua kwa mrija wa esophagus pia kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza. 

 

Matibahu huhusisha;
  • Kubadili mfumo wa maisha kwa kuzingatia aina ya chakula na muda wa kula

  • Kudhibiti uzalishaji wa tindikali tumboni kwa kutumia dawa  za PPIs au

  • Upasuaji wa kuondoa kucheua tindikali

 

Asilimia 80 ya wagonjwa wanaotumia dawa tatizo hudhibitiwa, asilimia 20 ya wagonjwa tatizo linaweza kuendelea au kujirudia licha ya kuwa kwenye dawa.  Ni muhimu kutambua wagonjwa hawa(asilimia 20) ili kuweza kuwapa matibabu yanayostaili kuzuia madhara yanayowez akujitokeza.

 

Tiba kubadili mtindo wa maisha

Matibabu haya huhusisha

​

  • Kupunguza uzito (kama una uzito mkubwa kupita kiasi au ugonjwa wa obeziti) soma kuhusu BMI kujua uzito gani unashauriwa kulingana na urefu wako kwenye Makala ndani ya tovuti hii

  • Acha  matumizi ya pombe, chokoleti, juisi chachu kama za machungwa n.k matumizi ya nyanya au mazao ya nyanya, minti, kahawa na vitunguu

  • Usile mlo mkubwa wa chakula kwa wakati mmoja- huongeza uzalishaji wa tindikali kwa wingi tumboni ili kumengenya chakula hicho

  • Subiria baada ya masaa matatu kupita kabla ya kulala kitandani baada ya kula chakula

  • Tumia mto wakati wa kulala ili kichwa kiwe juu- hii huzuia tindikali kutoka tumboni na kuunguza mrija wa esophagus

  • Kama ni mjamzito, zuia kuinamia  mbele, kula mlo kidogo, mara kwa mara na acha kula chakula masaa matatu kabla ya kwenda kulala iwe mchana au usiku

  • Vaa nguo zisizobana- Kuvaa nguo zisizobana zinazoongeza shinikizo tumboni na kukufanya ucheue

  • Endapo una dalili za kiasi unaweza kutumia dawa za kuzuia uzalishaji wa tindikali jamii ya PPI au histamine antagonist

 

Kumbuka kubadili maisha ni hatu muhimu na ya kwanza kwenye matibabu.

 

Tiba dawa

  • Dawa za kupunguza makali ya acid- Huweza kuzuia dalili zisizo kali, kunywa kila baada ya kula chakula

Dawa za H2 risepta antagonisti

Hutibu dalili za wastani za kuugua kwa mrija wa esophagus, wagonjwa wengi wanahitaji kuendelea na dozi endelevu ili kuzuia kujirudia kwa ugonjwa. Mfano wa dawa ni Cimetidine na  ranitidine.


Dawa za PPIs

Ni dawa zenye nguzu zaidi na zenye maudhi kiasi. Zipo dawa za aina nyingi katika kundi hili ikiwa pmaoja na omeprazole, pantoprazole n.k. soma Zaidi kuhusu namna zinavyofanya kazi kwenye Makala zilizo kwenye tovuti hii.

 

Tiba ya Upasuaji


Upasuaji hufanyika kwa

  • Walioshindikana kwa tiba dawa za PPI, au wagonjwa ambao wanataka kupona kabisa kwa upasuaji.

  • Kama mtu amepata madhara ya kuwa na barrett's esophagus

  • Kuwa na dalili zingine nje ya dalili za kuathiriwa kwenye esophagus kama vile, kukohoa, kifua kutoa miruzi, maambukizi kwenye masikio au pua kutokana na kuungua na tindikali, kuoza kwa meno

  • Endapo mgonjwa ana umri mdogo

  • Wagonjwa wasioweza kuzingatia kutumia dawa ipasavyo

  • Wanawake waliokoma hedhi na wanashida ya mifupa laini

  • Wagonjwa wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba,  au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii

Imeboreshwa,

12 Agosti 2023, 17:07:54

Rejea za mada hii:

1.National Institute of Diabetes and Digestive and Kidney Diseases. https://www.niddk.nih.gov/health-information/digestive-diseases/acid-reflux-ger-gerd-adults. Imechukuliwa 4.12.2020

2.The American Gastroenterological Association. http://www.gastro.org/info_for_patients/2013/6/6/heartburn-gerd. Imechukuliwa 4.12.2020

3. The American College of Gastroenterology. https://gi.org/topics/acid-reflux/. Imechukuliwa 4.12.2020

4. Giannini EG, et al. Management strategy for patients with gastroesophageal reflux disease: a comparison between empirical treatment with esomeprazole and endoscopy-oriented treatment. Am J Gastroenterol. 103(2):267-75. [Medline].

5. Katz PO. Medical therapy for gastroesophageal reflux disease in 2007. Rev Gastroenterol Disord. 7(4):193-203. [Medline]

6. Fass R, Sifrim D. Management of heartburn not responding to proton pump inhibitors. Gut. 58(2):295-309. [Medline].

7.. Fass R. Proton pump inhibitor failure--what are the therapeutic options?. Am J Gastroenterol.104 Suppl 2:S33-8. [Medline].

8. Heidelbaugh JJ, et al. Overutilization of proton pump inhibitors: a review of cost-effectiveness and risk [corrected]. Am J Gastroenterol.104 Suppl 2:S27-32. [Medline].
Murray L, Johnston B, Lane A, et al. Relationship between body mass and gastro-oesophageal reflux symptoms: The Bristol Helicobacter Project. Int J Epidemiol. 32(4):645-50. [Medline]. [Full Text].

9. Pandolfino JE, et al. Obesity: a challenge to esophagogastric junction integrity. Gastroenterology. 130(3):639-49. [Medline].

bottom of page